NA ABDI SULEIMAN.
BENK ya watu Wazanzibar PBZ tawi la Pemba, imekabidhi vifaa mbali mbali vya kusomea wanafunzi vyenye thamani ya shilini Milioni 7.5 kwa taasisi ya MY hope Foundation, ikiwa ni utekelezaji wa ahadi walioitoa kwa taasisi hiyo.
Vitu vilivyotolewa ni pamoja na mabuku, penseli, rula, raba, kalamu, kwa lengo la kuwapatia wanafunzi ambao wanasoma skuli lakini hawana uwezo wa kununua vifaa hivyo.
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi msaada huo Meneja wa PBZ Pemba Mohamed Shehe Othaman, alisema wamelazimika kutekeleza ahadi yao walioitoa Machi 26 mwaka huu kwa taasisi hiyo.
Alisema hicho walichokitoa ni miongoni mwa faida zao wanazozipata, hulazimika kuzirudisha kwa wananchi kupitia misaada kama hiyo.
“Suala la elimu ni jambo la muhimu kwa mtu yoyote, hata kiongozi wetu wa dini alitakiwa kusoma kwanza, sasa wapo watoto wanasoma lakini hawamiliki vitendea kazi tumeona ni vizuri kuwasaidia kupitia taasisi hii ya My Hope Foundation”alisema.
Naye Mwenyekiti wa Taasisi ya My Hope Founation Kisiwani Pemba, ambae pia ni Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Mattar Zahor Massoud, aliishukuru PBZ kwa kkutekeleza kwa vitendo msaada huo kwa taasisi hiyo.
Alisema msaada huo umefika wakati mufaka kwao, huku akiahidi kuufikisha kwa walengwa waliokusudiwa ikiwa ni wanafunzi wanaohitasi vifaa hivyo ili kufikia lengo lao la kielimu.
Alifahamisha kuwa Wilaya ya Chake Chake inawanafunzi 3600, Wete 4000, mkoani 4000 na Micheweni 7000, huku akiahidi msaada huo wataanza na watoto 100 kutokana na misaada waliopokea haiwezi kukidhi hata kwa watoto 200.
“Sisi kupitia lile bonanza tuliweka wastani kusaidia wanafunzi 1000 Pemba nzima, lakini hali ya upokeaji wa michango mpaka sasa sio na watoto ni wengi wanaohitaji huduma”alisema.
Hata hivyo lengo la taasisi hiyo ni kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuona mtoto aliyefikia muda wakwenda skuli anakwenda skuli na kupata elimu.
Mwenye kiti huyo aliwataka wadau wa maendeleo na taasisi zenye uwezo kujitokeza kusaidia wanafunzi ambao wanasoma katika mazingira magumu, ili na wao waweze kutimiza ndoto zao kielimu.
Kwa upande wao baadhi ya wanachama wa taasisi hiyo, wameipongeza benk hiyo kutekeleza kwa vitendo ahadi yake, huku wakizitaka taasisi nyengine kujitokeza kusaidia watoto wenye mahitaji ya vifaa ya kielimu.