NA ZUHURA JUMA, PEMBA
MTOTO mmoja amefariki dunia baada ya kujinyonga kwenye mti wa mpera huko Kinowe Jiso Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Mtoto huyo aliejulikana kwa jina la Nadhifa Talib Othman mwenye umri wa miaka 12 mkaazi wa Kinowe Jiso.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba Juma Sadi Khamis alisema, tukio hilo limetokea Aprili 24 mwaka huu majira ya saa 2:00 asubuhi.
“Mtoto huyo mwenye miaka 12 amejinyonga kwenye mti wa mpera kwa kutumia kamba ya nailoni, ingawa chanzo bado hakijajulikana”, alisema.
Alieleza kuwa, Jeshi la Polisi Mkoa huo linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo, ili kujua chanzo cha mtoto huyo kujinyonga.
Kamanda Sadi aliwataka wazazi na walezi kuwa karibu na watoto wao na kuwaasa mambo mema na kuwakataza mabaya, jambo ambalo litawasaidia kupata taarifa za watoto.
Mwili wa marehemu ulifanyiwa uchunguzi katika hospitali ya Micheweni na baadae kukabidhiwa jamaa zake kwa ajili ya mazishi.