NA ABDI SULEIMAN.
VYAMA vya Siasa Kisiwani Pemba, vimesema ipo haja kwa asasi za Kiraia kuwa tayari kushirikiana na vyama hivyo, katika suala zima la kutoa elimu kwa wanawake kushiriki katika kuwania nafasi za Uongozi.
Wamesema vyama hivyo vimekua na utamaduni wa kuweka wagombea wanawake katika nafasi mbali mbali, kuanzia udiwani, uwakilishi, ubunge na urais, kikwazo kikubwa bado nguvu ya wanawake ni ndogo kuwania nafasi za uongozi katika vyama hivyo.
Akiwasilisha kazi za kundi la vyama vya siasa, katika mkutano wa wadau mbali mbali wa wanawake, uliondaliwa na Jumuiya ya PEGAO Kisiwani Pemba na kufanyika mjini Chake Chake.
Mohamed Haji Kombo alisema ipo haja kwa vyama hivyo, kuhakikisha wanawafikia wanawake wengi katika kuhamasisha kuingia katika uongozi, ili uchaguzi unaokuja kuwe na mwamko mkubwa zaidi.
Aidha alisema bado uwelewa ni mdogo kwa wanawake katika kuwania nafasi hizo, hivyo ipo haja kwa vyama vya siasa navyo kupiga vita suala la rushwa ili kuwapa nafasi wanawake katika uongozi.
“Tumegundua hata katiba za vyama vya siasa zinatoa nafasi 30/70 kwa wanawake na sio kama inavyoelezwa 50/50, hata bunge na baraza la wawakilishi hazijatoa nafasi moja kwa moja ya 50/50”alisema.
Naye kiongozi chama cha ACT Wazalendo kutoka Yussuf Salum, alisema bado katiba za vyama vyao hazijajitosheleza, lakini bado wanawake wanaendelea kuwapatia nafasi wanawake katika kuwania nafasi za uongozi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha AAFP Taifa, Said Soud Said alizitaka asasi za kiraia kuwa tayari kuwashirikisha viongozi hao, katika kuhamasisha wanawake kuwania nafasi za Uongozi.
Alizishauri asasi hizo zinazotetea wanawake, kupendekeza kuwepo kwa mgombea mwenza katika jimbo awe mwanamke, ili mbunge au mwakilishi anapofariki au kujiuzulu wadhifa huo kuapishwa moja kwa moja na sio kurudia tena uchaguzi mwengine.
“Tunaporudia uchaguzi gharama nyingi zinatumika, ifike wakati tuwe na mgombea mwenza katika jimbo na awe mwanamke pale linapotokea la kutokea yeye ni kuapishwa tu na sio kuitishwa uchaguzi mpya”alisema.
Kwa upande wa kundi la wanasheria, mwakilishi wa kundi hilo Siti Habibu Mohamed alisema wamegundua kuwa sheria mbali mbali zinahitaji kufanyia mabadiliko, ili kuwapa nafasi wanawake kuwania nafasi hizo ikiwemo sheria za vyama vya siasa.
Naye shekhe Rashid Juma Suleiman kutoka kundi la viongozi wa dini, alisema uislamu unathamini na umempa hadhi kubwa mwanamke kuwa kiongozi ikiwemo kusalisha, kuendeleza drasa, shuhuli za mazishi, kuosha maiti na hata kusalia.
Mapema mkurugenzi wa Mradi wa SWIL kutoka PEGAO Hafidhi Abdi Said, aliwataka wawakilishi wa taasisi za kiserikali kila mmoja kuhakikisha wanayafanyia kazi kwa vitendo, changamoto zilizoibuliwa na wahamasishaji jamii katika maeneo waliofanyia kazi.
Alisema wahamasishaji hao wameweza kuibua changamoto nyingi zinazowakumba wananchi, ambazo zinahitaji kufanyiwa kazi ili kupunguza vilio vya wananchi hao.
MWISHO