Monday, November 25

Watoto wenye matatizo ya mfumo wa mkojo na mifupa kisiwani Pemba wafanyiwa upasuaji.

NA ZUHURA JUMA, PEMBA

WAZAZI wenye watoto waliofanyiwa  upasuaji wa matatizo ya mfumo wa mkojo na mifupa kisiwani Pemba, wameishukuru Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuwaletea madaktari bingwa ambao wamesaidia kuokoa maisha ya watoto wao.

Walisema kuwa, ingekuwa Serikali haikufanya msaada huo wa kuwaletea wananchi wake madaktari, wasingeweza kwenda kuyafuata matibabu hayo kutokana na hali zao kimaisha na hatimae watoto hao wangemata ulemavu wa maisha na wengine kupoteza maisha.

Wakizungumza mara baada ya watoto wao kupata huduma ya upasuaji katika hospitali ya Chake Chake, wazazi hao walisema kuwa, wamefurahia sana huduma hiyo ambayo wasingeipata kutokana na ukosefu wa fedha za matibabu.

“Kwa kweli Serikali inawajali sana wananchi wake na ndio maana imefanya juhudi kubwa ya kuwatafutia huduma mbali mbali, ikiwa ni pamoja na kuwatuletea madaktari kutoka nje ya nchi kwa ajili ya kuja nchini kutufanyia matibabu”, walisema wazazi hao.

Mmoja wa wazazi hao, Maryam Abdalla Sultan mkaazi wa Wete alisema kuwa, ni jambo la faraja kuona kwamba madaktari hao wamekuja kuwasaidia kuwapa matibabu, kwani wasingeweza kuzimudu gharama za matibabu ya magonjwa hayo.

“Serikali inatusaidia sana kwa sisi tusio na uwezo wa kuifuata huduma nje ya nchi, kwa sababu tuliambiwa matibabu ya mjukuu wangu huyu ambae ana miezi 11 ni milioni nne, yeye miguu yake imepinda, lakini tunashukuru leo tumefanyiwa bure”, alisema.

Kwa upande wake mzazi mwenye mtoto aliefanyiwa upasuaji wa tatizo la mkojo mkaazi wa Mkanyageni Mkoani alisema, anashukuru kwa matibabu hayo kwani kila siku alikuwa anamfikiria mwanawe kuhusu ugonjwa wake na matibabu yake.

“Mwanangu alikuwa hana tundu ya haja ndogo na nilipokuja hospitali niliambiwa nisubiri afike miaka miwili, lakini nashukuru na yeye ni miongoni mwa watoto walio bahatika kupata huduma hiyo ya upasuaji”, alisema mama huyo.

Nae mzazi Hadia Kheir Vuai mkaazi wa Kengeja Pemba alisema, matibabu hayo wameyafurahia sana na kusema kuwa mtoto wake ambae amefanyiwa upasuaji wa mifupa anaendelea vizuri.

“Mwanangu mguu wake ulikuwa umepindana lakini kwa sasa nashukuru amefanyiwa upasuaji na natumai akipona atakuwa katika hali nzuri”, alisema mama huyo.

Mapema daktari Dhamana wa hospitali ya Chake Chake Abrahman Said Mselem alisema kuwa, wamepokea ugeni wa madaktari bingwa kutoka falme za kiarabu katika nchi za Saud Arabia, Misri na Sudan.

Alisema kuwa, kambi hiyo ya madaktari itakuwa kwa muda wa siku saba katika hospitali za Wilaya Chake Chake na Wete, ambapo kwa Chake Chake wanafanya upasuaji kwa wagojwa wa mifumo ya mkojo na mifupa ambapo Wete wanafanya kwa maradhi ya jumla yakiwemo ya akinamama na wenye kensa.

“Hapa hapa Chake tumeongeza kufanya upasuaji kwa wagonjwa wa jumla na mpaka sasa muitikio ni mzuri, ambapo kambi hiyo ya madaktari bingwa ilitanguliwa na upembuzi yakinifu, kwa hiyo wagonjwa walikuja kabla ya wiki tatu na kuwataarisha kwa ajili ya upasuaji”, alisema.

Alifahamisha kuwa, matibabu hayo yalianza Mei 8 mwaka huu, ambapo hadi kufikia jioni ya Mei 8 wagonjwa 13 wamefanyiwa upasuaji katika kada mbali mbali.

Daktari huyo alisema kuwa, huduma inaendelea kutolewa na hali inaendelea vizuri ingawa kuna changamoto zinazojitokeza hasa kwa wale ambao hawakupata taarifa za mwanzo.

“Taarifa zilitoka kwenye shehia zetu, mitandao na kwenye vyombo vya habari, lakini baada ya kuona watu wengi wanakuja tulikaa na hawa madaktari kuwaeleza na kusema kwamba watafanya tena upembuzi yakinifu kwa wale ambao wamekosa na tayari wagonjwa mbali mbali wanaendelea kupokewa hospitalini hapo”, alisema daktari huyo.

Daktari bingwa wa upasuaji wa mifupa kutoka katika kambi hiyo, Hisham Refae alisema kuwa, wamekuja Zanzibar kwa ajili ya kutoa msaada wa matibabu kwa wananchi ambao wanasumbuliwa matatizo ya mifupa, maradhi ya mifumo ya mkojo na magonjwa mengine ya jumla.

“Lengo letu ni kuwasaidia watu wenye matatizo mbali mbali ikiwemo matatizo ya mifupa na kuwafanyia upasuaji, tunashukuru sana muitikio ni mkubwa na tunandelea kuwapatia huduma”, alisema daktari huyo.

Kambi hiyo ya madaktari bingwa kutoka taasisi ya ‘Peleks’ ipo chini ya ufadhili wa shirika la Direct Aid.

MWISHO.