NA ABDI SULEIMAN.
KAIMU Mratibu wa Tume ya Ukimwi Pemba Ali Mbarouk Omar, amesema watakahikisha wanaelimisha jamii katika mikesha ya Mwenge wa uhuru utakapokuwepo Kisiwani Pemba, ili kuzuwia tabia hatarishi zitakazopelekea kuwepo kwa maambukizi mapya ya VVU.
Alisema katika mikesha uwepo kwa viashiria vingi, hivyo vijana wanapaswa kushiriki katika mikesha kwa salama na amani na kusitokee maambukizi mapya.
Kaimu Mrataribu huyo aliyaeleza hayo wakati alipokua akizungumza na waandishi wa habari, huko Ofisini kwake Mjini Chake Chake Pemba.
Aidha alishauri kuwa mikesha hiyo itakapofanyika isizidi saa nne za Usiku, ili kutokuwapa nafasi vijana na baadala yake kamati za ulinzi na usalama kudhibiti maeneo hayo.
Alisema ZAC itahakikisha inaweka mabanda katika maeneo yote ya mikesha, kwa kutoa huduma za upimaji wa hiyari pamoja na kutoa elimu kwa jamii na uonyeshaji wa filamu ili kusaidia kujikinga na maambukizi mapya ya VVU.
“Tusipochukua tahadhari kwa hali ya juu basi tunaweza kusababisha maambukizi mapya kwa vijana, ikizingatiwa takwimu bado zinaonyesha kundi hilo ndilo lilit=hatari zaidi kupata maambukizi hayo”alisema.
Alisema bado maambukizi mapya yapo na katika mwaka 2021 Pemba watu 115 wamepata, hivyo vijana wanapaswa kutambua thamani yao kwani wao ndio nguvu kazi ya taifa.
Hata hivyo aliwataka wananchi kila mmoja kuchukua tahadhari kwa nafsi yake, ili tuendelea kuwa na mazingira salama ambayo kijana hatopata magonjwa ya kujamiana.
Kwa mujibu wa kitabu cha hutuba ya bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar 2022/2023, iliyosomwa na Waziri wa Wizara hiyo Harous Said Suleiman, imesema jumla ya vijana 5,576 walipata huduma katika vituo rafiki ikiwemo upimaji wa VVU ambapo kati ya vijana 2,314 walipomwa na tisa waligundulika wameambukizwa VVU.
Kwa upande wa kampeni Kijana kata UKIMWI kundi la vijana la miaka 15-24 katika wily azote za Zanzibar zilifanyika, kupitia mabonanza, mashindano ya mpira wa miguu, mashindano ya chemsha bongo kwa skuli 12 na uchoraji wa picha.
Ambapo vijana 5,620 walifikiwa na elimu kupitia vielelezo vya elimiu na maarifa juu ya VVU na UKIMWI, na afya ya Uzazi katika vijana 3194 waliopimwa wanaume 1873 na wanawake 1036 huku mwanamke mmoja aligundulika kuwa na VVU.
MWISHO