NA HANIFA SALIM.
ZAIDI ya shilingi Milioni 45,000,000/= zimetolewa na taasisi ya Ifraji Zanzibar Foundation, kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya kusambazia huduma ya maji safi na salama kwa kijiji cha Tundauwa Wilaya ya Chake chake Pemba.
Akizungumza katika makabiziano ya vifaa hivyo, Meneja wa Taasisi ya Ifraji Zanzibar Foundation Pemba Abdalla Said Abdalla, alisema vifaa hivyo ni pamoja na mipira yenye urefu wa kilomita tatu, paipu za nchi mbili na tatu na viungo vyake vya kufungia.
Alisema Ifraji ni taasisi yao ndogo imedhamiria kusaidia jamii kwa kiasi kikubwa, ambao lengo lake ni kuhakikisha wananchi wote hasa maeneo ya vijijini wanapata huduma ya maji safi na salama.
Alieleza, maji ni kitu muhimu kwa binaadamu hata miti, ambapo Ifraji imekipa kipaumbele chake kimoja, ikiwa mwaka huu zaidi wameelekeza miradi yao kwa upande wa Mkoa wa Kaskazini kuifikia Wilaya ya Wete na Micheweni.
“Chake chake tumesaidia kupeleka mnara wa maji katika skuli ya Ngagu Ndagoni, kijiji cha Mabaoni ambacho kilitumia zaidi ya shilingi milioni 26 kupeleka mradi wa maji, kijiji cha Papani zaidi ya shilingi milioni tisa, lengo letu ni kuleta ufanisi,’’ alisema.
Aidha alisema, ni matumaini yao mradi huo utakapokamilika utaleta ufanisi kwa wananchi wa Tundauwa, huku akiwataka wananchi hao kuwaunga mkono kwa kutia nguvu zao pale zinapohitajika ili malengo yaweze kufikiwa.
Akizungumza mara baada ya kukabidhi msaada huo Mkuu wa Wilaya ya Chake chake Abdalla Rashid Ali aliipongeza taasisi ya Milele na Ifraji kwa jitihada zao wanazozifanya kwa kuiunga mkono serikali yao.
Alisema, anazifahamu juhudi za taasisi hizo kwa kuweza kuboresha maisha ya ustawi wa jamii kupitia nyanja tofauti hivyo, aliwataka wananchi wa Tundauwa kuzithamini na kujali fedha ambazo zimekua zikitolewa kwao.
“Itakapotokea kunahitajika kuchimbwa misingi tujitokeze kwa wingi hizi bomba ziweze kuzikwa maji yapatikane malengo ya Serikali na Milele yatakua yametimia,’’ alisema.
Nae Afisa kutoka mamlaka ya maji Zanzibar ZAWA Pemba Juma Omar Khamis alisema, awali walipata malalamiko ya wananchi kutokana na ukosefu wa huduma ya maji safi na salama ambapo mamlaka iliwataka waunde kamati ambayo ipeleke malalamiko kwa taasisi hiyo ya milele kupitia Ifraji.
“Tulitakiwa sisi tupeleke makisio pamoja na ununuzi wa vifaa, tulipata fedha kwa ajili ya kununua mipira yenye urefu wa kilomita tatu na vifaa vyake vya kuungia bomba hizi,” alisema.
Sheha wa shehia ya Kilindi Nassor Mohamed Khamis, alimpongeza Mkuu wa wilaya kwa kuwakabidhi vifaa hivyo ambavyo vitaondosha changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi wa Tundauwa.
Nao wananchi wa shehia ya Tundauwa waliishukuru Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar kwa juhudi zao ambazo wamekua wakizichukua kwa wananchi wake siku hadi siku.
Walisema sasa Ifraji imefuta kilio chao ambacho walikua nacho kwa muda mrefu, hivyo wameahidi kushirikiana nao bega kwa bega ili kuhakikisha zoezi la uchimbwaji wa misingi na shughuli za kukamilisha mradi huo unakamilika kama ilivopangwa.
MWISHO.