Sunday, January 5

Vijana Pemba wataka maridhiano yaenziwe kwa vitendo, Wasema umoja, mshikamano, amani ndio silaha ya maendeleo

 

NA HAJI NASSOR, PEMBA

 

…..hii sio mara ya kwanza, kwa gwiji wa siasa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, kuwa Makamu wa Kwanza wa rais ndani ya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Kabla ya kufutwa matokeo ya uchaguzi mkuu wa 2015, Maalim Seif, kwa wakati huo akihudumu na Chama cha Wananchi CUF, alishika nafasi hiyo kutoka 2010 hadi 2015.

Wakati huo Dk. Ali Mohammed Shein wa Chama cha Mapinduzi (CCM), akiwa Rais wa awamu ya saba, akipokea kijiti hicho kutoka kwa muasisi wa maridhiono hayo Amani Abeid Karume.

Maalim, ameamua kurudi tena kuwa Makamu wa Kwanza, kwa sasa akiwa pamoja na rais wa awamu ya nane, wa Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi.

Kwa ustaarabu, uvumilivu, ukongwe wa kisiasa na kuweka mbele zaidi maslahi mapana ya wazanzibari, ndio maana Disemba 8, mwaka 2020, Zanzibar ilizaliwa tena upya.

Upya wake, unakuja maana licha ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, kuanzia mwaka 2010 kutaka kuwepo kwa serikali ya Umaja wa Kitaifa, ‘SUK’ lakini hitilafu za hapa na pale mwaka 2015 ‘SUK’ haikuwepo.

Leo hii tukiwa ndani ya ‘SUK’ ni furaha na mbwembwe za wazanzibari, kwa kule viongozi wetu wakiamua kufanyakazi pamoja tena bila ya kujali vyama vyao, kwa hakika hili ni jambo jema mno.

hapa sasa tunajufunza kuwa, Dk. Mwinyi ameshapandisha tanga la safari ya kuiongoza Zanzibar chini ya muundo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ‘SUK’ ukiwa unaendelea.

Ni punde tu, tangu taifa hilo lenye mamlaka ya ndani, kutoka katika uchaguzi mkuu, uliomazika mwishoni mwa mwezi Oktoba mwaka 2020.

Historia ya Umoja wa Kitaifa

Siasa za Zanzibar, daima huanza na moto mkubwa wa ushindani wa kisiasa na kisha kumalizika kwa maridhiano na maelewano makubwa.

Ndio maana, wazee walishasema wagombana nao ndio wapatanao, maana kwa Zanzibar kupatana ni pahala pake, kwa kule wananchi wake walivyoshiba demokrasia ya kwli.

Kumbe hata kabla ya Mapinduzi ya 1964, Zanzibar chaguzi zake zilikuwa za ushindani mkubwa, ambapo kisha baada ya kurudishwa tena kwa mfumo wa vyama vingi 1992 ushindani wa kisiasa, ukarudi kama awali.

Kwa wazanzibari, kama walivyo watu wa mataifa mengine, nao hukosana hapa na pale, ingawa wao hawawatumii wasuluhisi kutoka nje, bali wenyewe tu, basi na mwafaka hupatikana.

Moja ya jambo kubwa lililoafikiwa ni kuwepo kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, huku lengo kuu likiwa ni kuwaleta pamoja wazanzibari, ili waijenge nchi yao.

Ndio maana, hata Makamu wa Kwanza wa rais wa Zanzibar, Jemedari Maalim Seif Sharif Hamad, akasema kilichowasukuma kukubali kushirikiana na serikali, ni kuwaleta pamoja wananchi na sio chengine.

“Leo tumeshafungua ukurasa mpya wa umoja, mshikamano, maelewano kwa wazanzibari sote, bila ya kujali vyama vyetu vya ACT, CCM wala CHADEMA kilichopo mbele yetu ni kuwaleta pamoja wazanzibari,’’alisema Makamu wa Kwanza hivi karibuni.

Kila mmoja ni shahidi kuwa, uchaguzi mkuu wa vyama vingi ule wa mwaka 2010, na 2015 na huu wa 2020 ulifanyika kwa amani kubwa tena bila fujo lolote, kwa kule viongozi wakuu kufahamiana.

Uteuzi wa Maalim Seif umepokewa vipi?

Vijana wa kisiwa cha Pemba, wanasema kwanza ni jambo jema na zuri, kwa mkongwe huyo wa siasa kukubali kuingia ndani ya serikali ya Umoja wa Kitaifa ‘SUK’.

Wanasema kauli za Rais wa Zanzibar, Makamu wa Kwanza, Makamu wa pili katika kuendeleza mbele Zanzibar, lazima zienziwe na zitunzwe kwa vitendo na kila mmoja.

Omar Khamis Haji miaka 26 wa Mtambile anasema, wameyapokea vyema maridhiano hayo, na sasa kilichobakia ni kwa kila mmoja, na kwa nafasi yake ayatekeleze kwa vitendo.

Kama alivyo Omar, na hata Khamis Muhidini Juma 30 na Fauzia Kheir Hassan miaka 21 wa Kipapo, wanasema kilichobakia wao kama vijana, ni kuhamasishana ili kuendeleza mbele maridhiano hayo.

Hata Mohamed Khamis Juma miaka 34 wa Wete Limbani, anasema, maendeleo ya vijana hayatopatikana, ikiwa nchi haina maridhiano miongoni mwao.

“Sisi tunawategemea viongozi wetu, watusafishie njia za kutimiza ndoto zetu, sasa kama hakuna maridhiano, umoja na mshikamano ni vigumu kusimama,’’anasema.

Hata Siti Mohamed Omar wakati akizungumza kwenye kongamano la amani lililofanyika Wesha hivi karibuni, alisema wameridhishwa mno na uwepo wa serikali ya Umoja wa Kitaifa.

“Hii ni ishara kubwa kuwa, sasa ile Zanzibar yenye neema itafika pahala pake, maana matakwa ya Kikatib ya uwepo wa serikali ya Umoja wa Kitaifa yameshafanyika,’’anasema.

Mwenyekiti wa Jumuiya sauti ya Vijana Pemba Said Mussa Rashid, anasema vijana wako wazi kuona maridhiano hayo yanafanyiwa kazi.

Anasema, watahamasishana kama vijana, kuona kwanza umoja, mshikamano, amani na maridhiano hayo yanakuwa endelevu kwa maslahi mapana ya taifa.

Hivi karibuni, Naibu Mufti Mkuu wa Zanzibar sheikh Mahamoud Mussa Wadi, akifungua kongamano la amani kwa vijana, alisema wao wana nafasi kubwa ya kutunza amani na utulivu.

Anasema vijana ndio kundi kubwa na lisilotabirika katika nchi yoyote, sasa lazima waelewe nafasi yao, na kuhakikisha hawaitendei vibaya nchi yao.

“Sasa uchaguzi mkuu wa vyama vingi umeshamalizika, na viongozi wameshapatikana na serikali ya pamoja imeshaundwa, ni wajibu wa vijana sasa kusaka fursa,’’alieleza.

Kamanda wa Polisi mkoa wa kusini Pemba Ahmed Khamis Makarani, anasema lazima vijana wasikubali kutumiwa ovyo ovyo, hasa kwenye kuelekea kuyatia doa maridhiano na amani ya Zanzibar.

Kamanda huyo, aliwasisitiza vijana, kuwa wanapoilinda amani iliyopo, ndio mwenye kazi ya boda boda, kilimo, afya, uvuvi na usanii ataifanya kwa ufanisi.

“Sasa uchaguzi umeshamalizika, kila mmoja kwa nafasi yake na alipo, awe balozi mzuri wa kuilinda amani, maridhiano na hasa hawa vijana maana ni wepesi kuharibika,’’anasema.

Kwani hata rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi, katika hutuba zake mbali mbali amekuwa akirudia kuwa, katika mazingira ya sasa ya siasa za Zanzibar, muundo huo wa serikali utasaidia pakubwa.

Anasema, kwani neema ambayo aliwahidi wananchi kwenye kampeni, haitowafikia ikiwa, nchi hiyo wananchi wake hawako kwenye mshikamano wa kijamii na utulivu wa kisiasa.

“Ndugu zangu, lazima tuelewa kuwa, amani, maridhiano na mshikamano ndio jambo moja kubwa na la kwanza, katika kufikia maendeleo ya kweli,’’anafafanua.

Hata Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, baada ya kula kiapo kushika nafasi hiyo, alisema hatovumiliwa yeyote, ambaye ataleta chokochoko za kuwagawa wazanzibari na kurudisha uhasama miongoni mwao.

Amewataka wananchi visiwani Zanzibar, kudumisha amani na umoja uliopo na kuwabeza wale wote wanaopinga umoja uliopo nchini, ili kuipatia nchi ya Zanzibar maendeleo kwa haraka.

Amesema kuwa, kuwepo kwa Umoja na Ushirikiano kwa wazanzibari, ni jambo muhimu katika nchi na kuwataka watu waachane na itikadi za mambo ya kisiasa katika masuala ya kusimamia maendeleo yao.

“Kama tukiwa wamoja ni rahisi nchi yetu kupiga hatua kimaendeleo, katika nyanja zote na kuwa mfano wa nchi nyingi za bara la Afrika,”ameeleza Maalim Seif.

Sambamba na hilo, Makamu huyo wa Kwanza wa Rais amewataka wazanzibar, kuacha ubaguzi wa rangi au wa kisiasa, kwani mbora mbele ya Mwenyezi Mungu ni yule mchaji zaidi.

Pia Maalim Seif, amesema dhamira ya yeye na Rais wa Zanzibar, Dk. Husein Ali Mwinyi kufanya kazi kwa pamoja ni kuondoa yale madhaifu yote, ambayo hupelekea wazanzibari kutofautiana na kuleta chuki miongoni mwao.

Amesema, kuwepo kwa Serikali yenye muundo wa umoja wa kitaifa, ni njia moja ya kubaini sababu ya kupata dawa ya kuilinda Zanzibar, isirejee tena katika migogoro isio ya lazima.

Kundi jengine ambalo limekuwa lipewa tahadhari, ili mardhiano yasiingie doa pamoja na vijana, lakini pia waandishi wa habari na kalamu zao.

Na ndio katika kuhakikisha waandishi wa habari wanakuwa weledi katika kuandaa vipindi, makala na habari Klabu ya Waandishi wa Habari Pemba PPC, kwa kushirikiana na Internews liliendesha mkutano wa siku moja kwa waandishi w ahabari.

Kwenye mkutano huo uliofanyika mjini Chake chake, waandishi waliohudhuria mkutano, waliahidi kuwa wabunifu na weledi ili kuhakikisha maridhiano na amani inamea Zanzibar.

Meneja kituo cha redio cha Zenj FM na Zenj TV, Is-haka Mohamed Rubea alipongeza hatua ya PPC na Internews kukutana na waandishi wa habari.

Nae Khadija Mahmoud Chande mwakilishi wa Channel Ten, alisema ukumbusho na mbinu walizopewa zimewapa ufahamu mkubwa.

Akizungumza kwenye mkutano huo Mwenyekiti wa PPC Bakar Muss Juma, alisema wameamua kuwajengea uwezo waandishi, ili waandae vipindi na makala kwa uweledi.