Friday, November 15

Waandishi fuateni mfumo wa kidigitali-Mdhamini Thabit.

NA ABDI SULEIMAN

WAANDISHI wa Habari Kisiwani Pemba, wametakiwa kuendana na wakati wa sasa wa mabadiliko ya kijiditali, katika ufanyaji wa kazi zao.

Hayo yameelezwa na Afisa Mdhamini Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa Serikali za Mitaa na Idara Maalumu SMZ Pemba Thabit Othaman Abdalla, wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari, ulioambatana na usafi wa fukwe ya Vumawimbi Wilaya ya Micheweni.

Alisema iwapo waandishi wataendana na mabadiliko hayo, hata ufanyaji wa kazi zao zitaweza kubadilika na kuwafikiwa watu wengi kwa wakati mmoja.

Alisema dunia sasa imebadilika kila kitu kinaenda kisasa zidi, hivyo nao niwakati wa kwendana na mabadiliko hayo yaliyopo duniani ya Teknolojia.

Mdhamini huyo aliwapongeza waandishi hao kwa kuunga mkono kauli ya Rais wa Zanzibar, katika uchumi wa Buluu na usafi wa mazingira, kwa kuamua kufanya usafi katika fukwe ya Vumawimbi.

“Ufanyaji usafi huu wa fukwe ni kutangaza mazingira ya utalii, pia ni eneo la uchumi wa buluu mambo yote yanenda sambamba kwa kuhakikisha mazingira safi watalii wanakuja na serikali inapata fedha,”alisema.

Akizungumzia uhuru wa habari, alisema uhuru wa habari Zanzibar upo, kwani waandishi wanafanya kazi zao bila ya kubugudhiwa na kutangaza bahari zao kikamilifu.

“Rais wa Zanzibar ameweka siku maalumu ya kuzungumza na waandishi wa habari, kila mwisho wa mwezi na huwakutanisha waandishi wote yote ni kuonyesha serikali inaunga mkono uhuru na vyombo vyao,”alisema.

Hata hivyo aliwataka waandishi kutambua dhima na thamani yao, kwa kuhakikisha wanaendana na maadili yao ya kazi katika kuandika habari zao na kuwapa wananchi.

Naye afisa Mdhamini Wizraa ya Utalii na Mambo ya Kale Pemba Zuhura Mgeni Othman, alisema waandishi wa habari wanafanya kazi kubwa sana ya kutangaza kazi zao wanazozifanya na kusikika kwa jamii.

Alisema ufanyaji wa usafi huo ni jambo muhimu sana katika kutangaza uzuri wa fukwe za Vumawimbi, hali itakayopelekea kuongezeka kwa watalii kutembelea Pemba.

Mapema Afisa Mdhamini Wizara habari Vijana Utamaduni na Michezo Mfamau Lali Mfamau, alisema hakuna uhuru kwa mwandishi usio na mipaka, hivyo wanapaswa kutambua mipaka yao na kujua thamani yao kwa jamii nan chi kwa ujumla.

Naye mwenyekiti wa Klabu ya waandishi wa Habari Pemba (PPC) Bakar Mussa Juma, alisema wamelazimika kudhimisha kwa kufanya usafi, kutokana na muhimu wa ufukwe huo katika kutangaza utalii wa kisiwa cha Pemba.

Kaulimbiu katika maadhimisho ya mwaka huu ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari ni:vyombo vya habari na changamoto ya kijiditali.

MWISHO