NA ABDI SULEIMAN
MKUU wa Wilaya ya Chake Chake Abdalla Rashid Ali, amesema Zanzibar ni Visiwa na ardhi sio ile ile bali inaendelea kupungua, idadi ya watu wanaengezeka kwa kasi kubwa hivyo wananchi wanapaswa kuwa na matumizi sahihi ya ardhi iliopo ili kukidhi mahitaji yanayopangwa.
Alisema ardhi hiyo inatumika kwa shuhuli zote za kimaendeleo, hivyo jamii inapaswa kusimamia vyema ardhi na matumizi mazuri ili kuepuka kuhasimiana.
“Tunapoingia katika migogoro ya ardhi hatutokuwa na muda wakufanya shuhuli nyengine za kijamii na kiuchumi na kuwa changamoto, kwa kushuhulikia migogoro wakati mwengine inahitaji fedha nyingi kwa ajili ya ufuatiliaji”alisema.
Mkuu huyo wa Wilaya aliyasema hayo, wakati alipokua akifungua mkutano wa kamati za mashauriano za shehia katika kushirikisha suala la uhamasishaji wa haki za umiliki wa ardhi katika jamii, ulioshirikisha shehia tano na kuandaliwa na Jumuiya ya PECEO, kupitia utekelezaji wa mradi wa umiliki wa ardhi kwa wanawake.
Aidha alisema watu wote wanahaki sawa ya kupata ardhi ya Zanzibar, ikiwa mwanamke au mwanamme kwa upande wa serikalini na kidini wananamna yake ila mungu ameshaweka ikiwemo mirathi na kusimamiwa na Wakfu.
Hata hivyo Mkuu huyo alisema ardhi kwa sasa imekua ni chanzo kikubwa cha maendeleo, kwa namna moja au nyengine wanawake wamekuwa katika harakati za kimaendeleo na wamehamasika, hivyo migogoro ya ardhi kuitatua katika shehia na sio kuwenda kwenye sheria.
“Tusizuruhusu kesi nyingi kwenda katika mahakama na tunajaza msururu, vizuri kufuata suluhu na sio vyombo vya sheria kila mtu anafaidika kwa namna moja au ngengine tofauti na sheria mmoja anakosa,”alisema.
Hata hivyo alizitaka kamati za mashauriano kuendelea kuisaidia serikali, katika utatuzi wa migogoro na wenye haki za kupata ardhi wapate ardhi zao, kwani kila mtu anahaki sawa za matumizi ya ardhi ikiwa taratibu zitafutwa.
Aidha Mkuu huyo wa Wilaya alisema hapendi kuona migogoro ya ardhi inatokea tena kwa mwaka 2022, kwani kwa sasa wanamaliza kutataua migogoro ya ardhi iliyotokea miaka ya nyuma.
Akiwasilisha mada umuhimu wa kumiliki ardhi katika kumkomboa mwanamke, mwezeshaji kutoka Kamisheni ya Ardhi Pemba Yussuf Hamad, alisema kamisheni ya wakfu na Malia ya amana ndio yenye haki ya kurithisha kwa taratibu za kiserikali.
Aidha alisema lengo la serikali ni kusajili ardhi yote ya zanzibar katika shehia 388, ila zeozi la usajili linaenda kidogo kidogo kutokana na taratibu zilizopo, huku wakitambua kua ardhi ndio chanzo cha uchumi.
Kwa upande wake Afisa Sheria kutoka kamisheni ya wakfu na Mali ya amana Pemba Massoud Ali Massoud, alisema ni busara kwa wananchi kusajili au kurithishana mali zao ikiwemo ardhi kwa kufuata taasisi husika ili kuepusha migogoro inayoweza kutokea.
Akielezea lengo la mafunzo hayo katibu wa jumuiya ya PECEO Juma Said Ali, alisema wanatowa elimu kwa viongozi hao kwani wanaamini itafika haraka katika jamii.
Nao washiriki wa mkutano huo wameishauri kamisheni ya ardhi kupeleka mrejesho kwa masheha pale wanapofanya utambuzi na usajili wa ardhi katika maeneo yao.
Mafunzo hayo yametolewa na Jumuiya ya PECEO, kwa Ufadhili wa The Foundation for civil society na kufanyika mjini Chake Chake.
MWISHO