NA ABDI SULEIMAN, PEMBA
KILA ifikapo Juni 25 ya kila mwaka, dunia huadhimisha siku ya bahari ulimwenguni.
Moja ya rasili za asili zenye matumizi lukiki, basi ni bahari iwe kwa usafiri, uvuvi, chanzo cha maji ya kunywa na dawa.
Wapo wanaoitumia bahari kuwa ndio chanzo chao kikubwa cha kuwapatia kipato, kutokana na shughuli zao mbali mbali ikiwemo uvuv.
Wakati juzi Juni 25, dunia iliadhimisha siku ya bahari, tunapaswa kujiuliza wale walioamua kujiingiza katika shughuli za ubaharia wako hali gani.
Ubaharia ni kazi kama zilivyo kazi nyengine, husikii baharia kugoma au kususia kazi kwa sababu moja au mbili tatu kutokea.
Miaka yote kazi ya ubaharia ilionekana ni kazi ya wanaume pekee, ingawa kwa sasa hali imekua ikibadilika na hata kwa wanawake kujiingiza.
MABAHARI WANASEMAJE JUU KAZI HIYO
“Kwa sasa maisha yamebadilika, ubaharia ni kazi kama zilivyo kazi nyengine, chamsingi ni mtu mwenyewe kujiheshimu na kujitunza hapo utafanikiwa,”amesema bahari Zainab.
Zainab Ali Abrahaman mwanamke wa kwanza Zanzibar kuingia katika fani ya ubaharia wa meli, licha ya kazi hiyo kuwa ngumu aliweza kusema na moyo wake.
“Nilifanya kazi katika meli mbali mbali kama vile Ukombozi II, Mapinduzi II na hata Sea star, nilifika mafia kwa shughuli hizi za ubaharia wa meli,”anasema.
Shemsa Rajab Ali anasema kazi ya ubahari ni kazi kama zilivyo kazi nyengine, vizuri kufuata taraibu na kulinda thamani na kuthamini kazi husika.
KIPI KILIWAVUTA KWENYE UBAHARIA
Zainab anasema ni mapenzi na marafiki aliokuwa nao na kumitia moyo, na kuona anaweza kwaenda kufanya kazi kama mhudumu wa kawaida.
Baada ya mwezi mmoja na wiki tatu alikwenda kusomea mambo ya ubaharia (bahari) na uhandisi wa meli chuo cha ubaharia Dar es-Salam (DMI).
Shemsa anasema alikuwa akifanya kazi katika hoteli, baada ya kuona mafanikio madogo aliamua kwenda kusomea ubaharia, hii nikazi kama zilivyo kazi nyengine.
“Unaweza kufanya kazi miaka 20 ila kama haikua moyoni kuna siku utaiacha, ubaharia upo ndani ya moyo wangu na niliomba mungu siku moja kutimia ndoto yangu hiyo na imetimia,”amesema.
CHANGAMOTO GANI WANAKUMBANA NAZO
Shemsa anasema hakuna kazi ngumu kama ubaharia, waajiri bado wanaendelea kusimamia mishahara midogo, mpaka sasa wanalipwa shilingi 300,000 kwa mwezi.
“Vyumba vya kulala mabaharia wanawake kwenye baadhi ya meli ni shida, kutokana na kuwa vichache, ukichukulia maumbile ya mwanamke huwezi kumchanganya na baharia mwanamme,”amesema Shemsa.
“Baadhi ya meli vyumba ni sita au saba, wafanyakazi wengi ni wanaume unajikuta unalala chumba kimoja, meli ya Mpainduzi tu ndio mazingira mazuri kwa wanawake yalikuwemo,”amesema.
Zainab anasema mikataba ya kazi ni miezi sita au mwaka, hakuna kazi ya kudumu hiyo ni kawaida kwa mabaharia, ndio maana ikawa ngumu, kwa vile unatafuta maisha lazima ukubali tu.
“Fani yangu kwenye mashine ni vitu vinavyohitaji nguvu zaidi, ukiomba msaada kwa mwanamme unakumbana na masharti wewe ni mwanamke, nyundo nzito na lazima upige na unajikuta unachoka haraka lazima upambane nayo,”amesema.
MWAMKO WA WANAWAKE UKOJE KATIKA UBAHARIA
Kwa sasa mabaharia wanawake wameongezeka, wengi wameamua kusoma ubaharia katika chuo cha ubaharia ‘DMI’, Zanzibar wapo zaidi ya 16 ambao wamejiingiza katika ubaharia.
Kwa sasa wanawake wapo nje hakuna aliyepo kazini, ni wazi Zanzibar bado hakujawa na uwelewa kujua umuhimu wa sekta ya bahari, hatujaitendea haki wengi wanaona ubaharia ni uhuni tu.
Aidha amewasihi wanawake na jamii kuachana na dhana potofu iliyozoeleka, kuwa kazi ya ubahari ni uhuni, akisema popote jambo hilo linaweza kufanywa au kuepukwa.
USHAURI GANI KWA WANAWAKE
Wanawake wanapaswa kufahamua uchumi mkubwa ni bahari, wasitengemee kukaa nyumbani, na kumtegemea mume ama baba.
Aidha amewataka wazazi kuwasomesha watoto wao fani ya ubaharia, ni kama zilivyo nyengine, ili kazi hiyo isije ikavamiwa na watu kutokana nje ya Tanzania.
WANAUSHAURI GANI KWA SERIKALI
Wanasema kilio chao kikubwa ni serikali kuwaacha mkono mabaharia, wakati ndio sekta muhimu sehemu yoyote duniani.
baharia ndio wasimamizi wakubwa wa mizigo ndani ya meli baada ya kupakiwa kutoka sehemu moja kwenda nyengine, mfano dawa na chakula
Kuwaangalia kwa jicho la huruma mabahari wanawake kwa kuwasaidia, fani ya ubahari sio kama nyengine, vyeti vyao kila baada ya miaka minne wanatakiwa ukasome tena ili viweze kutumbulika.
MAMLAKA YA USAFIRI BAHARINI ZANZIBAR (ZMA)
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri Baharini, (ZMA), Sheha Mohamed, amesema mabaharia wana mchango mkubwa katika kuchangia maendeleo ya kiuchumi na kijamii duniani.
Uchumi wa nchi unategemea usafiri wa baharini kwa kiwango kikubwa, hivyo ipo haja ya kuonekana uwepo wao na kuthaminiwa.
ZMA imekusudia kuleta mageuzi ya kiutendaji kwa mabaharia, ili wawe ni sehemu ya kuitangaza Zanzibar vyema wakati wanapotekeleza majukumu yao ndani na nje ya nchi.
Anasema mabaharia wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo, kukosa fursa za kielimu na kiuchumi hivyo hawana budi kushikana mikono.
‘’Tayari tumekua na mabaharia wanawake ambao wameonesha umahiri mkubwa katika kazi yao, tayari tumewaagiza wamiliki wa meli kuweka vyumba maalumu kwa ajili ya mabaharia wanawake,’’anasema.
CHUO CHA UBAHARIA TANZANIA (DP/PEA)
Makamu mkuu wa Chuo cha Ubaharia Tanzania Dk.Tumaini Shamban Gurumo, mabaharia wanapaswa kuthaminiwa kwani wanaitangaza vyema nchi yao, hivyo wanapaswa kujiongeza kielimu ili kufikia malengo zaidi.
“Niwakati wenu kujiongeza katika eneo moja kwenda jengine, kulingana na mabadiliko yaliyopo hivi sasa duniani,”amesema.
TAASISI YA WANAWAKE WANAOFANYA KAZI BAHARI AFRIKA MAHSARIKI NA KUSINI (WOMESA)
Mwenyekiti wa ‘WOMESA’ Fotnata Makoyi Kwakaya, amewataka wanawake kutokujiweka nyuma na kutumia fursa zilizopo katika bahari ili kushiriki ipasavyo kama ilivyo wanaume.
Ameitaka jamii kuwahimiza watoto wa kike kujiingiza katika sekta ya ubaharia, kwani dunia imebadilika kulingana na teknolojia kwani wanawake wanaweza kufanya kazi hizo kama ilivyo wanaume.
Mhandisi wa meli Farida Shambani, amesema sekta ya bahari ni pana zaidi zamani wanaume walikuwa wengi, ila sasa dunia imebadilika hata wanawake wamo.
Anasema mwanamke yoyote anaweza kufanya kazi kama mwaname, inategemea na uwezo wa mwanamke wenyewe na jinsi gani alivyokubali na kuikubali mwenyewe.
“Fursa zipo nyingi meli nyingi zinajengwa, bado mabahari wanawake ni kidogo na mahitaji ni mengi, kila siku meli zinafanya safari,”amesema.
katika kipindi cha COVID 19 mabaharia walijitolea na kuweka roho zao rehani, ili kuhakikisha mahitaji yanapatikana duniani licha ya kuwepo mazuilio katika mipaka.
TASAC INASEMAJE
Mwenyekiti wakala wa shirika la meli Tanzania (TASAC), Kepten Mussa Hamaza, anasema Tanzania ndio nchi pekee vyenye mabaharia wazuri katika meli za kimataifa, hivyo wanapaswa kuendelea kulinda heshima na tahamani yao wanapokua duniani katika harakazi zao za kazi.
Amesema mwaka 2019 dunia ilikubwa na ugonjwa wa COVID 19, lakini mabaharia waliendelea kufanya kazi zao duniani kote ili matifa yaendelee kupata huduma mbali mbali ikiwemo vyakula.
“Mabaharia waliacha familia zao na kuendelea kutoa huduma duniani, meli zilisafirisha dawa, vyakula hata misaada kwa nchi zilizokubwa na janga la Covidi 19, hii ni kuonyesha kuwa bado mabahari,”amesema.
VIONGOZI WA SERIKALI WANASEMAJE JUU YA UBAHARIA
Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Mattar Zahor Masoud, amesema usafiri wa baharini ni muhimu katika kufikia uchumi wa viwanda, hivyo mabaharia wanapaswa kuthaminiwa na kuheshimiwa kutokana na kazi yao wanayoifanya kila siku.
Amesmea bado wanawake ni changamoto katika ubaharia, lazima taasisi husika zitowe nafasi kubwa kwa wanawake kuingia katika fani ya ubaharia kwani nifani kama zilivyo fani nyengine.
Waziri ujenzi na Uchukuzi Tanzania Profesa Makame Mbarawa Mnayaa, amesema asilimia 90 ya usafirishaji wa bidhaa duniani hutumia usafiri wa baharini, Zanzibar tayari imeshaanza ujenzi wa bandari ya kisasa itakayorahisisha usafiri.
Kujengwa kwa bandari ya Mangapwani, itaweza kubadilisha maisha ya uchumi wa Zanzibar kupitia baharini.
Amesema sekta ya bahari mara nyingi wafanyakazi wake ni wanaume, ila anaamini wanawake wanauwezo mkubwa na wanaweza kwani wanapoingia huko wataweza kuhamasisha na wanawake wenzao.
MWISHO