Thursday, January 16

Chwale kuacha tabia ya kuharibu miundo mbinu ya maji safi na salama

NA ZUHURA JUMA, PEMBA

WANANCHI wa shehia ya Chwale Wilaya ya Wete wametakiwa kuacha tabia ya kuharibu miundombinu ya maji safi na salama, ili idumu kwa muda mrefu na kuweza kuwanufaisha.

Akizungumza na mwandishi wa hizi sheha wa shehia ya Chwale… alisema, ni vyema wananchi wakashirikiana kulinda maeneo yenye vianzio vya maji, kwa maslahi yao katika shehia.

Alisema kuwa, kumekuwa na uharibifu katika shehia yake, ambapo baadhi ya wananchi hufunga mifugo yao kwenye vianzio vya huduma ya maji, jambo ambalo linaweza kusababisha uharibifu mkubwa na hatimae kukosa huduma hiyo.

‘’Najitahidi sana kuwaelekeza lakini bado hawajataka, wale ni wanyama kwa hiyo unapowafunga kwenye miundombinu ya vianzio vya maji wanaweza kuharibu kwa kupasua paipu’’, alisema sheha huyo.

Alisema kuwa, kuna haja kwa kila mwananchi kuthamini huduma hizo zilizowekwa, kwani zinawanufaisha wao, hivyo si vyema kufanya uharibifu.

‘’Serikali inapata gharama kubwa kuwafikishia huduma wananchi wake, hivyo waone kwamba watakapoharibu watasababisha huduma hiyo ikosekane na kuwapa dhiki wananchi wengine’’, alifahamisha.

Kwa upande wake mwananchi kutoka shehia hiyo Ali khatib alisema kuwa, uharibifu wa miundombinu ya maji upo, ambao hufanywa na watu wazima na watoto.

‘’Kuna sehemu maeneo ya Likoni kule, watoto wameenda kupika kwenye paipu kubwa ya maji na wazazi wao wamewaona lakini hawakuwakataza, paipu hiyo imeungua kidogo’’, alisema mwananchi huyo.

Alieleza kuwa, ingawa paipu hiyo haijatoboka lakini ni rahisi sasa kuweza kutoboka, hali ambayo inaweza kuja kuleta athari ya baadae na watu kukosa maji safi na salama.

Aidha alieleza kuwa, kuna baadhi ya wanajamii wanafua chini ya vianzio vya maji ya kisima, ambapo ni kuhatarisha usalama wa afya ya wananchi, kutokana na kuwa maji machafu yanaingia kwenye visima hivyo.

‘’Maji ya visima bado tunatumia hasa yanapofungwa maji ya mfereji, lakini wananchi wetu, wanafanya uchafu chini ya kisima na maji tunatumia kwa kunywa na kupikia, hivyo wanaweza kutusababishia maradhi ya mripuko’’, alisema.

Nae Afisa Uhusianao wa Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) kwa upande wa Pemba, Suleiman Anas Massoud alisema kuwa, wamekuwa na utaratibu wa kutoa elimu kwa kuweka mikutano ya shehia, ili wananchi watunze miundombinu ya vianzio vya maji safi na salama, ingawa baadhi yao wanapuuza.

‘’Hatujapata taarifa ya kuungua kwa paipu hiyo, lakini tutakwenda kukagua na kutoa tena elimu kwa sababu kuna watu pia wanalima kwenye paipu za maji jambo ambalo halitakikani’’, alisema.

Afisa huyo aliwaomba wananchi hao kushirikiana na ZAWA katika kulinda na kutunza miundombinu hiyo sambamba na kufika kwenye mikutano yao, ili waelewe madhara yanayoweza kutokea iwapo watafanya uharibifu.

MWISHO.