Thursday, January 16

Makala: VISIWA VYA NJAO NA KOKOTA VILIVYOKOSA UMEME KWA MIAKA 50

FUNDI wa shirika la Umeme ZECO Tawi la Pemba, akisaga maji ndani ya blenda mara baada ya umeme kuwashwa ndani ya Kisiwa cha Njao, ikiwa ni kuangalia ufanyaji kazi wa vifaa hivyo.(PICHA NA ABDI SULEIMAN)
BAADHI ya viyoo vinavyozalisha umeme wa jua katika kisiwa cha njao, vikiwa vimeshafungwa na kutoka huduma kwa wananchi wa kisiwa hicho.(PICHA NA ABDI SULEIMAN)
GUZO ya umeme ambayo imewekwa katika kisiwa cha Kokota, ambayo inasambaza umeme kwa wananchi kutoka katika mtambo wakuzalisha umeme wa jua kisiwani humo.(PICHA NA ABDI SULEIMAN)
BAADHI ya mitambo ya kuhifadhia umeme na kusambaza kwa wananchi, ikiwa imewekwa katika kisiwa cha Njao na kutoka huduma kwa wananchi wa kisiwa hicho.(PICHA NA ABDI SULEIMAN)

NA ABDI SULEIMAN.

APRILI 2022 historia mpya imeweza kuandikwa, kwa wananchi wanaoishi katika visiwa vidogo vidogo vilivyoko Wilaya ya Wte Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Nimwendo wa dakika 20 hadi 25 kama hali ya hewa ni nzuri, ikiwa sio nzuri ni mwendo wa dakika 30 hadi 35 kutoka Mtambwe Kivumoni hadi kisiwa cha Kokota, ni masafa ya dakika tano (5) hadi sita (6) kutoka Chokaani Gando hadi katika kisiwa cha Njao, kwa kutumia boti aina ya faiba.

Kilio cha miaka zaidi ya 50 kwa wananchi wa visiwa hivyo kimeweza kutatua, baada ya mradi wa umeme wa nishati ya jua kuanza kutoa huduma ndani ya visiwa hivyo.

Ni maendeleo makubwa kwa wananchi hao, sasa huduma ambazo walikuwa wakizikosa zitapatikana ndani ya visiwa vyao na sio kupoteza muda kuzifuata Gando au kivumoni.

Tayari Saa 12:30 za jioni, jua tayari limeshazama, usiku ukiwa umeshaanza kuingia wananchi wakiwa wamejawa na shauku kubwa ndani ya mioyo yao, huku wakisubiria kutimia kwa ahadi yao, ghafla kelele na vigeregere vikaanza kusikika baada ya ZECO kuwasha umeme wa Sola ndani ya visiwa hivyo.

Nilijawa na huruma na imani mwilini, baada ya kuona vibatari ambavyo awali vikitumika kwa kumurikia ndani ya majumba muda wote, kuvunjwa kwa siku moja baada ya nishati ya umeme kupatikana.

WANANCHI WANASEMAJE SASA

Tatu Bakari Ali(45) Mkaazi wa kisiwa cha Kokota, anasema fahamu zake kisiwa hicho hakikua na umeme zaidi ya kutumia vibatari, hali iliyopelekea kukumbwa na mafua, vifua mara kwa mara kutokana na moshi unaotoka katika taa hizo.

“hapa kama tunataka kuchaji simu zetu tuvuke hadi Ngambu, sasa hakuna tena kuvuka kila mtu anabonyeza tu ndani mwake,”amesema.

Anasema umeme umemuondoshea shida ya kununua mafuta, vipimo vitatu kwa silingi 600 tena anatumia siku mbili, saivi kila kitu kimepanda bei huku kwetu kipimo sasa 300.

Mtumwa Omar Juma mkaazi wa kokota, anasema kwa sasa mahitaji ya vitu baridi vyote vinapatikana ndani ya kisiwa, waliona uwezo wameweka hadi majokofu kwa ajili ya kuuza juisi shilingi 300 kifuko na kuhifadhia samaki.

Adam Khamis Adam (34) mkaazi wa Njao, anasema wamechoka kusikiliza mpira redioni, sasa umeme huo umewafanya kutizama moja kwa moja TV.

Anasema kabla ya kuwepo kwa umeme huduma za kuchaji simu, mabarafu ya kuhifadhia samaki lazima wayafuate Chokaani Gando, lakini sasa majokofu yamejaa ndani ya kisiwa chao.

WAVUVI WANASEMAJE WAO JUU YA UMEME

Ali Alawi Khatib mkaazi wa mbuyuni Njao, anasema umeme huo wameupokea kwa furaha, muda mkubwa wameusubiria sasa njao imekuwa ya kisasa.

Anasema kwa sasa hawataweza kuuza samaki, Pweza na Ngisi kwa hasara badala yake watawahifadhi katika majokofu ndani ya Kisiwa hicho.

”Sasa nyinyi munaotoka mjini Musahau kama mutaweza kupata vitu rahisi, hakuna atakaeweza kuuza samaki wake kwa hasara kama zamani tutawahifadhi humu humu visiwani,”amesema.

Khamis Makame Yussuf mkaazi wa Kisiwa cha Kokota, amesema wamefurahia huduma hiyo kuanza kuwaka ndani ya kisiwa chao, sasa watalazimika kuhifadhi vitu vyao kupitia majokofu.

Anasema uvuvi wao mkubwa watu wa visiwani ni Pweza, ngisi na makome, sasa bidhaa watauza kwa bei wanayotaka wako tayari kusafirisha kupeleka nje ya Pemba.

MANAHODHA WA WANAOVUSHA ABIRIA WANAYAPI WAO

Hamza Khamis Ali (29) anasema tokea umeme kuanza kuwaka biashara ya samaki na Pweza imebadilika, tafauti na miaka ya nyuma sasa kilomo moja ya Pweza imepanda kutoka 4500 hadi 5000,5500 mpka elfu 6000/= bei hiyo bandarini kwa mvuvi.

Anasema hivi sasa hata samaki nao wamepanda bei, wavuvu wengi wanamiliki majokofu wapo tayari wakawahifadhi hadi siku ya pili wawapeleke ng’ambu, kuliko kuuza kwa hasara kama ilivyokuwa zamani.

“Umeme umewasaidia sana hata kubadilisha maisha ya wananchi, nyumba zimebadilika muda wa usuku ni kungara, hakuna tena matumizi ya vibatari wala taa ya kandili,”alisema.

Juma Ali Khamis mkaazi wa Kisiwani Njau, anasema uwepo wa umeme kumepelekea mabadiliko makubwa ndani ya kisiwa, kwani sasa kila kilichokosekna kitakuwepo kufuatia uwepo wa umeme huo.

WASIMAMIZI WA HUDUMA ZA KIJAMII WANASEMAJE WAO

Abdalla Sharif Mshemga imamu wa skiti kisiwani Kokota, anasema umeme huo utapelekea ibada sasa kufanyika kwa kutumia vipaza sauti, ikiwemo darasa za usiku na hutuba za sala ya Ijumaa zitaweza kusikika ipasavyo.

“Umeme umepeleka furaha ndani ya kisiwa chetu, shida ndogo ndogo sasa zitaondoka adhana itasikika kikamilifu kwa kutumia vipaza sauti”amesema.

Yussufa Khatoro anasema hata wanafunzi sasa wataweza kudurusu masomo yao muda wa usiku, pamoja na kuwepo kwa masomo ya ziada.

VIONGOZI WA SHEHIA WANAYAPI WAO

Sheha wa shehia ya Mtambwe Kusini Othaman Ali Khamis, amesema kufikishwa kwa Umeme kisiwa cha Kokota ni faraja kubwa kwa wananchi wanaishi ndani ya Kisiwa hicho.

“Kwa sasa ni kaya 56 ambazo zinatumia umeme huo kati ya kaya 84 zilizomo ndani ya kisiwa hichi, niwazi maendeleo sasa yatakuwepo watu hata watoto watasoma hadi usiku na biashara zitafanyika muda wote,”alisema.

Naye Sheha wa shehia ya Gando Shaibu Kaimu Mambuji, ameishukuru serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kutimiza ahadi yake kwa vitendo kuwapelekea umeme wananchi wa kisiwa cha Njao.

Anasema sasa ni wakati kwa wananchi wa Njao kunufaika na matunda ya serikali yao, ikiwemo suala la zima la umeme ambao ni wa uhakika.

MAFUNDI WA MRADI WANASEMAJE WAO

Mhandisi wa mradi kutoka Kampuni ya Photons Energy Erick Kimambo, anasema umeme unaozalishwa na jua ni sawa na umeme unaotokana na vyanzo vya maji, utaweza kutumia vifaa vyote vinavyotumia umeme hata kama mafundi uwashi watakuwepo.

“Kinachotafautisha hapa ni nishati ya kuzalishiwa umeme, Tenesco na ZECO wanatumia maji ila huu wa visiwani unatumia vyanzo vya jua, lakini matumizi yake ni sawa sawa”alisema.

Anasema Umema huo utaweza kubadilisha maisha ya wananchi wa visiwa hivyo, kuongeza thamani gharama za vitoeleo vinavyovuliwa kwa kuhifadhiwa katika majokofu, kwani umeme huo ni wa uhakika na haukatikati ovyo kama umeme wa maji.

“Huu umeme unaozalishwa na jua baadae unaenda kuhifadhiwa katika betri na mwengine unaenda majumbani, usiku betri zinatoa hifadhi yao kwenda kwa wananchi, wala hauna mgao kama umeme wa maji na nisalama kwa mazingira,”amesema.

Anasema umeme huo utajitosheleza kwa muda wa miaka 10 hata kuwa na vifaa vya kisasa, kilowati 39 unazalishwa kijiji cha njao unajitosheleza hata kwa kaya 80 na mwengine unabaki.

Hata hivyo aliwakaribisha wawekezaji kuekeza ndani ya Visiwa hivyo, hoteli zinaweza kunufaika na umeme huo bila ya kuterereka, mfumo huo ni imara na hauna tatizo lolote.

WASIMAMIZI KUTOKA ZECO

Naye msimamizi wa mradi wa umeme huo, kutoka ZECO Pemba Ali Faki Ali, anasema umeme huo utawasaidia wanafunzi kujisomea, pamoja na kuimarisha shuhuli za uvuvi kwa wananchi wa visiwa hivyo.

Anasema mitambu hiyo sio ya ZECO bali ni ya kwao, ZECO ni dhamana tu kuharibika kwake kujua ni kuharibikiwa wao, lazima wachukuwe hatua katika ulinzi wa mitambu hiyo, kwani imegharimu fedha nyingi sana Dola laki 458,043.92 za Kimarekani.

“Uwezo wake kwa kokota ni Kilowat 85 zaidi ya wateja 150 unaweza kuwahudumia kwa wakati mmoja na sasa ni wateja 90, na njao Kilowati 50 kuhudumia zaiidi ya wateja 100 na sasa wateja 50, huu ni mradi wa kipekee kwa wananchi,”alisema.

Mradi umewaza kuwapatia wananchi balbu (matungi)6, pamoja na kuwaungia kwa shilingi elfu 50,000/= baada ya laki mbili (200,000/=), pamoja na kuwakopesha kwa wale wasiokuwa na fedha zote kwa kulipa elfu 30 tu.

MENEJA MKUU ZECO ZANZIBAR

Meneja mkuu wa Shirika la Umeme ZECO Mshenga Haidar Mshenga, anasema umeme huo wa jua hauna tafauti yoyote na unafanya kazi kama umeme mwengine, kwani unahimili vifaa vyovyote vya umeme ikiwemo hata viwanda vidogo vidogo.

“Huu meme wa njao na kokota haujatumika hata asilimi 3 mpaka sasa, serikali inawakaribisha hata wawekezaji kuwekeza katika umeme huo,”alisema.

Anasema sasa wanafikiria kuwaungia wananchi bure umeme na baadae waweze kulipa kidogo kidogo, ili tuone matumizi yake yanavyotumika kwa kujaza vifaa vya umeme.

Mjumbe wa Bodi ya wakurugenzi ya ZECO Azizi Said Ali, amesema uwekezaji wa umeme katika visiwa kwa umeme wa jua ni miradi mikubwa kwa ZECO, wananchi wameshaanza kunufaika na miradi hiyo.

Anasema tayari mikakati imeanzishwa katika uwekazaji wa miradi ya umeme wa jua Zanzibar wenye uwezo wa Megawati 18 huo utakuwa ni mradi mkubwa zaidi kabla ya 2025.

Njao na Kokota vilikuwa ni visiwa vya mwisho ambavyo havijafikiwa na Umeme, lakini serikali imelazimika kuvifikia na mikakati ni kufikia visiwa vyote vinavyoishi wananchi.

Tayari shirika hilo limeshafikisha huduma za umeme katika visiwa mbali mbali vidogo vidogo, Ikiswemo Kisiwa Panza, Makoongwe, Fundo, Uvinje, Kojani, Njao na kokota, ili wananchi waweze kunufaika na huduma hiyo.

MWISHO

Abdi Juma Suleiman

Journalist/Photographer

Zanzibarleo newspaper
Chake Chake -Pemba
+255774565947 or +255718968355