NA HANIFA SALIM, PEMBA
MKUU wa Mkoa wa Kusini Pemba Mattar Zahor Masoud amewataka wazazi na walezi washirikiane kuwarejesha vijana ambao wametoroka skuli ili wajipatie haki yao ya msingi ya kielimu.
Alisema, mashirikiano ya pamoja vijana hao wataweza kurudi skuli kujipatia elimu na kuepukana na kujiunga katika makundi maovu yatakayowawezesha kujihusisha na matendo ya udhalilishaji, wizi na utumiaji wa madawa ya kulevya.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa Wilaya ya Chake chake Abdalla Rashid Ali alipokua akizungumza na wananchi kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huyo, katika uzinduzi wa skuli ya Bakar maandalizi shehia ya Kibokoni Vitongoji, iliyojengwa kupitia mfuko wa mwakilishi wa jimbo la Wawi.
Alisema, mwakilishi wa Jimbo la Wawi aliyoyafanya kwa kipindi cha muda mfupi kwa wananchi hayawezi kusimuliwa, hivyo aliwataka wananchi waendelee kumuunga mkono mwakilishi huyo ili aweze kutekeleza majukumu yake aliyojipangia.
“Nawapongeza wananchi kwa kuzaa rai ya kuanzisha skuli mkifahamu kwamba elimu ndio mkombozi wa kila kitu, hamasa hii ambayo mnayo tuiboreshe ili tufike mbali zaidi, alisema.
Alisema, kutokana na changamoto ambazo zipo zitatatuliwa ikiwemo upatikanaji wa huduma ya maji ambayo aliahidi kuitatua wao kama sehemu ya serikali ili usafi uweze kupatikana na kujikinga na maradhi mbali mbali.
Aidha aliwataka wananchi kushirikiana na serikali katika kutokomeza matendo ya udhalilishaji wa kijinsia sambamba na kuwanasihi kujitokeza kuhesabiwa ifikapo Agosti 23 katika zoezi la sensa ya watu na makaazi.
Hata hivyo aliwataka wananchi waboreshe mapato ya serikali kwa njia ya kuuza bidhaa zao watoe risiti na wanaponunua wadai risiti ili pato liongezeke na wananchi wafaidike kwa kujengewa barabara, hospitali, skuli na mengineyo.
Mwakilishi wa Jimbo la Wawi Bakar Hamad Bakar alisema, skuli hiyo itakua ni mkombozi kwa wananchi wa shehia ya Kibokoni kwani kwa kipindi kirefu watoto wadogo walitembea masafa marefu kufuata elimu ya maandalizi.
“Mvua, jua pamoja na hali zote zinazotokea wakitembea kufuata elimu maeneo ya mbali ukizingatia ni watoto wadogo ambao wanaweza hata kufanyiwa matendo ya udhalilishaji na baadhi ya watu wabaya, wazazi watakua watulivu na wenye imani na watoto wao wanapotoka nyumbani,” alisema.
Afisa Mdhamini wizara ya elimu na mafunzo ya amali Pemba Mohamed Nassor Salim alimpongeza mwakilishi huyo ambae anashirikiana kwa hali na mali na sekta ya elimu, hivyo aliahidi wananchi wa Kibokoni kupitia wizara yao kujenga madarasa ya msingi katika eneo hilo pamoja na kutatua changamoto ya vikalio.
Mapema Akisoma risala ya uzinduzi wa skuli hiyo ya maandalizi Maryam Said Abdulla alisema, ujenzi huo ulianzishwa na nguvu za wananchi kwa kuchimba misngi mwaka 2018 na kumalizika mwaka huu kupitia mfuko wa mwakilishi wa jimbo la Wawi unaosimamiwa na Baraza la mji Chake chake.
Alieleza, skuli hiyo licha ya kukamilika kwake lakini inakabiliwa na changamoto ikiwemo ya umeme, barabara na malengo ya wananchi wa Kibokoni ni kuengezewa madarasa ya msingi ili skuli hiyo iweze kutoa elimu zaidi.
Skuli ya maandalizi Bakar ya shehia ya kibokoni iliyojengwa kupitia mfuko unaosimamiwa na baraza la Mji yenye vyumba viwili, vyoo na ofisi ya walimu, ambayo imegharimu zaidi ya shilingi milioni 47 hadi kukamilika kwake.