Thursday, January 16

AMINA: Mlengwa kaya maskini sasa anaeishi kwa furaha

Amina: Mlengwa kaya maskini sasa anaeishi kwa furaha

  • Ana mifugo, keshajenga nyumba na anaendesha biashara ya nguo

NA HANIFA SALIM, PEMBA

“KABLA ya kuja kwa mpango wa kunusuru kaya maskini, hali yangu ya maisha ilikuwa ya kubahatisha hasa kujipatia mlo walu wa siku, ilikua kazi,’’

Ni maneno ya mwanzo ya mlengwa huyo wa TASAF, Amina Shaaban Shamte alipokuwa akizungumza nami, kwenye eno lake la malisho ya wanyama kijijini kwake Mgogoni Pemba.

Amina kabla ya kutuliwa na TASAF mikononi mwake, ilikuwa jambo la kawaida, kutimiza siku tatu bila ya mlo hata ule wa kumuwezesha kuishi.

“Kwanza niwashukuru viongozi ambao walileta huu mpango wa kaya maskini, mfumo huu umekuwa ni mkombozi mkubwa   kwetu sisi ambao tuna hali ngumu za maisha”, anasema.

Bi Amina anasema, kabla ya kuja kwa mpango huo wa kunusuru kaya maskini hakuwa na shughuli yoyote ya kujipatia kipato lakini baada ya kufikiwa na TASAF aliweza kujishuhulisha na biashara ya kuuza nazi na ndio safari yake ya kuona mwanga ilianzia.

Katika kipindi hicho ambacho TASAF haijamfikia, watoto wake kwenye suala la kusoma ilikua ni kwa njia ya kubahatisha, hali iliyopelekea siku moja mtoto wake alisitishwa masomo kwa ukosefu wa ada.

Kumbe sababu ya tukio, hilo ni baada ya mtoto wake kutotoa ada ya shilingi 10,000 ingawa kwa wakati huo nae ilimkwama kooni na kubakia nyumbani

“Kwa kipindi hicho kutokana na hali yangu ya kimaisha, shilingi 10,000 ilikua ni sawa na milioni moja, ingawa alirudi lakini baada ya dhiki na tabua iliyonitoa kijasho,’’anasema.

BAADA YA TASAF

Kwa mara ya kwanza ulipoanza mpango huo wa kaya maskini hakuamini, wakati sheha alipomwendea kwa kuanza kumuandikisha jina kwa ajili ya kufanyiwa usajili.

“Alikuja mwanamke ambae alitumwa na sheha akaniandika na kuniambia, kwa sababu ya ujane na watoto nilionao, kushindwa kujihudumia,’’anaeleza.

Anakumbuka kama leo, kwa mara ya kwanza alipokea shilingi 32,000, na alichukua hatua ya kuwanunulia watoto sare za skuli, mabuku na viatu.

Jengine alichokifanya ni kununua chakula pamoja na samaki mnene, na kwa mara ya kwanza alikula chakula cha mchana akiwa na furaha na watoto wake.

Kisha kwa miezi menngine mlengwa huyo wa kaya maskini, alifikiria namna ya kuanzisha biashara ambayo ana hakika inaweza kumtoa kimaisha.

‘’Nilianza na ununuzi wa nazi za shilingi 20,000, ambapo kila nazi kwa kipindi hicho nilinunua kwa shilingi 200 na baada ya kuuza kila moja kwa shilingi 500 na kujipatia faida ya shilingi 30,000,’’anasimulia.

Biashara ya nazi, iliendelea kumnogesha na kumuingia moyoni maana, kisha alijikuta na mtaji wa shilingi 150,000 unaotokana na biashara hiyo.

Baadae Amina, alifungua njia nyingine ya kujiongezea kipato, baada ya kuingia kwenye ununuzi wa nguo za mitumba za kitoto.

“Niliagizia kutoka Unguja roba moja la nguo hizo kwa shilingi 150,000 na kisha baada ya kuziuza nilijipatia faida ya shilingi 50,000 nilinogewa na kuendelea tena,’’anaeleza.

Maajabu na hamu ya kufanya biashara hiyo hasa aliyaona kwenye awamu tatu, pale alipochomoa shilingi 300,000 kujitupa tena Unguja, na safari hii akiingiza faida ya shilingi 150,000.

Kumbe Amina, pamoja na biashara yake hiyo, kisha alizaa fikra na hamu ya kununua mifugo, ili maisha yake ayatawale.

‘’Nilitumia shilingi 300,000 kununua mtamba wa Ng’ombe ingawa baada ya muda alizaa na kujipatia dume, ingawa nalo halikudumu nilimuuza baadae,’’anaeleza.

Hata mara ya pili, alibahatika Ng’ombe dume ingawa nilimuuza kwa shilingi 500,000 na hapo sasa hatua iliyofuata ni kutaka kuanzisha ujenzi wa nyumba ya kudumu.

Maana wakati huo anaendelea kupokea fedha za mpango wa kunusuru kaya maskini, Amina alikuwa akiishi kwenye nyumba ya tope tena ya kuazimwa.

Kwa sasa akiwa anaishi kwenye nyumba yake ya tofali yenye vyumba vitatu, kwa mchango wake wa hapa na pale, tayari ameshatumia shilingi milioni 5.

‘’TASAF imenitoa kwenye nyumba ya kuazimwa tena ya tope na makuti, na sasa naishi kwenye nyumba ya kifahari iliyoezekwa bati,’’anafafanua.

Sasa anajisifia kuwa ana uhakika wa maisha, achia mbali mlo wa mara tatu kwa siku, jambo ambalo anasema hakuwahi kuliota kwenye mbio zake za maisha.

 MPANGO WAKE WA BAADAE

Moja ni kumalizia kuizeka nyumba, na kutoa mlango maalum wa duka, ili sasa ahamie kwenye biashara ya nguo mpya (special) huku akiendelea pia na nguo za mtumba.

Alifahamisha, mpango wake mkubwa wa baadae ili kuona anaishi katika mazingira bora ni kumaliza kujenga nyumba yake na kueka duka la nguo mpya.

Malengo haya anaweza kuyafikia, maana pamoja na biashara zake hizo pamoja na ufugaji, Amina ni mwanachama wa ushirika unaojishughulisha na ufugaji.

Ushirika huo, uitwao ‘nia njema’ kwake anauona kama dhahabu, maana umekuwa sehemu ya kung’arisha maisha yake ya kila siku.

SHEHA

Sheha wa Shehia ya Mgogoni Said Hamad Khamis, anasema wakaazi wa shehia hiyo ni 4,326 kati ya hao waliomo kwenye kaya maskini ni 143 tokea mwaka 2014 akiwemo Amina.

Anasema, mpango huo wa kunusuru kaya maskini, umeibua miradi kadhaa ya maendeleo ndani ya shehia, ikiwemo ya ufugaji, ujasiriamali na kilimo cha mboga mboga.

‘’Kwa mfano pia ipo miradi ya jamii kama ule wa maji safi na salama unaowahudumia wananchi 4000 na uwepo wa kinu cha kusagishia nafaka unaosimamiwa na watu wenye ulemavu,’’anaeleza.

Jambo la kujivunia katika shehia yao ni kuona baadhi ya wananchi waliokuwemo kwenye mpango wa TASAF wamepiga hatua kimaendeleo kwa kujipatia kipato chao wenyewe.

Anasema, changamoto kubwa ambayo imekuwa ikijitokeza wakati wa upokeaji wa fedha za TASAF ni masafa marefu wanayotembea walengwa na ukizingatia wengine ni watu wazima wasiojiweza.

TASAF

Mratibu wa Mfuko wa maendeleo ya jamii Tanzania ‘TASAF’ Pemba Mussa Said Kisenge anasema, mpango wa kunusuru kaya maskini ni chachu ya kuleta maendeleo kwa wananchi.

Anasema walengwa 14,280 ndio wanaendelea kunufaika kupitia mpango huo wa kunusuru kaya maskini ata hivyo anasema, walengwa ambao wamefikiwa na mpango huo kwa Pemba kuanzia mwaka 2014 hadi 2019 ni 14,280 kupitia shehia 78, hadi sasa fedha zilizofikia mikononi mwa walengwa ni Billioni 14.4, ambapo kwa wastani kila mlengwa amepata shilingi 2,380/=.

                                                    MWISHO.