NA ABDI SULEIMAN
WAANDISHI wa Habari nchini wametakiwa kutumia taaluma zao, kuvunja mifumo yote kandamizi kwa wanawake inayopelekea kuwanyima fursa za kugombania uongozi.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Mtendaji wa Chama Cha Wandishi wa habari Wanawake Tanzania Zanzibar (TAMWA) Dr Mzuri Issa, wakati akifungua mafunzo ya siku tatu kwa waandishi 60 Zanzibar, Unguja 40 na Pemba 20 kwa njia ya mtandao ZOOM,
Dr Mzuri alisema kuna baadhi ya mifumo inawakwaza wanawake, kufikia maendeleo yao ikiwemo suala zima la kuwania uongozi, jambo linalorudisha nyuma jitihada na ndoto zao.
Akizungumzia suala la mila potofu, alisema zipo baadhi ya mila na tamaduni zinakwaza maendeleo ya mtoto wa kike, hivyo waandishi wa habari wanaweza kuweka uaswa kati ya wanawake na wanaume katika habari na kazi zao wanazozifanya.
“Tunapaswa kuona katika vyombo vyetu vya habari, wanawake tunawapa sanafasi kubwa kama ilivyo kwa wanaume, hapo tutakuwa tumeweka usawa katika kazi zetu,”alisema.
Hata hivyo aliwataka waandishi kuhakikisha wanaondosha mifumo yote kandamizi kwa wanawake, sambamba na kuwapa nafasi ya kugombani nafasi zauongozi mbali mbali zinapotokea.
Kwa upande wake Maratibu wa TAMWA Pemba Fat-hiya Mussa Said, alisema lengo ni kuwajengea uwezo waandishi wa habari kuandika habari za uchambuzi, kushawishi jamii na mamlaka mbali mbali kubadili mielekeo na mitazamo kuhusiana na mwanamke na ushiriki wake katika siasa na kupata haki za demekrasia.
Alisema lengo jengine ni kufikia 50 kwa 50 katika kuelekea uchaguzi mkuu ujao, kwa kuona wanawake wamehamasika zaidi kuwania nafasi za uongozi.
“Tupo hapa katika kuwajengea uwezo waandishi wa habari, kuhusiana na masuala ya jinsia na uongozi, kupitia mradi wa kuongeza ushiriki wa wanawake na uongozi katika masuala ya demokrasi na uongozi na kuwezesha jamii kudai haki zao,”alisema.
Alisema waandishi wataweza kundika habari ambazo zitaibua hamasa, kwa wanawake kujitokeza kugombania nafasi za uongozi, kwani hata dini haijamkataza mwanamke kugombania nafasi za uongozi, na kuwataka viongozi wa dini kutumia nafasi vizuri kusimamisha wanawake.
Akiwasilisha mada ya Jinsia na Maendeleo, Mwandishi wa habari Haji Nassor Mohamed, alisema bado mifumo dume inaendelea kuwakosesha wanawake haki zao za msingi ikiwemo za uongozi.
Alisema suala la uongozi linahusu wananchi wote, hivyo ipo haja kwa wanawake wenye sifa kuhamasishwa kujitokeza kugombani nafasi hizo.
“Mfumo dume ni hali ya kuwaacha nyuma wanawake jambo ambalo limeshapitwa na wakati, ni wakati sasa kwa wanawake kujitokeza kwa wingi kuwania uongozi,”alisema.
Akichangia katika mkutano huo mwandishi wa habari kutoka ZBC Pemba Mchanga Haroub Shehe, alisema harakati hizo za kumtambulisha mwanamke kuwa kiongozi zilianza zamani, lakini bado changamoto zipo zinazowakaza ikiwemo umasikini, wanawake kujinyanyapaa wenyewe na kuona tabua kushindana na akashinda.
Alisema wanawake ili waweze kuwa viongozi, wanapaswa kujitambu na kujiamini kuwa wanaweza kufanya lolote ili kuona wananufaika na kuwania nafasi za uongozi.
Naye meneja wa Redio Jamii Micheweni Ali Massoud Kombo, aliwataka waandishi kutumia aya za dini kuelezea nafasi zawanawake katika kuwania uongozi, kwani dini haijamkataza mwananke.
Mafunzo hayo ni mwendelezo wa utekelezaji wa mradi wa kuongeza ushiriki wa wanawake katika masuala ya uongozi, unatekelezwa kwa pamoja kati ya TAMWA Zanzibar, ZAFELA na PEGAO kwa ufadhili wa Ubalozi wa Norway nchini.
MWISHO
Abdi Juma Suleiman
Journalist/Photographer