DODOMA.
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amekutana na Wawekezaji wa Kampuni ya Black River kutoka nchini Switzerland wenye lengo kuwekeza katika biashara ya hewa ukaa.
Akiwa Jijini Dodoma Dkt. Jafo amesema Serikali inawakaribisha wawekezaji hao na kuahidi kushirikiana na wadau wa Mazingira katika kuhakikisha Tanzania inanufaika na biashara ya hewa ukaa,
Amesema katika Mkutano wa ishirini na sita wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP 26) uliofanyika jijini Glasgow, Uskochi mwishoni mwa mwaka jana miongoni mwa agenda kubwa iliyopewa msukumo madhubuti ni pamoja na namna ambavyo nchi inaweza kufaika na biashara ya hewa ukaa
“Tunaweka misingi mizuri ya kuhakikisha sasa Tanzania inanufaika na biashara ya hewa ukaa kwa kukamilisha mwongozo wa biashara hiyo” Dkt. Jafo alisisitiza
Kufuatia ujio huo timu ya wataalamu kutoa Ofisi ya Makamu wa Rais, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wizara ya Fedha na Ofisi ya Maliasili na Utalii wameagizwa kuchakata andiko litakalo wasilishwa na Kampuni ya Black River ndani ya wiki mbili
“Ni matumaini yangu kuwa biashara ya hewa ukaa itaweza kusaidia katika bajeti kubwa ya Serikali, kuelekea bajeti ya mwaka 2023/24 nchi inufaike na biashara hii huku tukilinda mazingira” Alisisitiza Dkt. Jafo
Pamoja na ukweli kwamba Tanzania siyo miongoni mwa nchi zinazozalisha gesi joto kwa wingi duniani, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imechukua hatua za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi zikiwemo kujenga uwezo wa kitaasisi, kutoa elimu kwa jamii na; kuhimiza shughuli za kilimo, ufugaji na uvuvi zinazostahimili mabadiliko ya tabianchi.
Kwa upande wake Bw. Cedric Biart Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni Black River amesema Kampuni yake iko tayari kuweza nchini, kunufaisha wananchi kupitia makubaliano na ushirikiano baina ya Serikali kuu, Serikali za Mitaa na wananchi wanaozunguka hifadhi za misitu katika jitiihada za kuhifadhi mazingira.
Ahadi ya Tanzani katika Jumuiya ya kimataifa kuhusu Mchango wa Taifa katika kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (Nationally Determined Contribution) ni upunguzaji wa uzalishaji wa gesi joto kwa asilimia 30-35 kutegemeana na uwezo kiuchumi itakapofika mwaka 2030