MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, amesema kuwa Zanzibar International Marathon ni Tangazo muhimu la kuutangaza Utalii wa Nchi, mbele ya mataifa ulimwenguni.
Makamu huyo ameyasema hayo wakati akiongoza Mbio za Tigo-Zantel Zanzibar International Marathon, huko Forodhani, Mkoa wa Mjini-Magharibi Unguja.
Amesema kuwa Zanzibar inayo hazina kubwa ambayo ni urithi wake wa asili, bali kwa mnasaba wa kufanyika kwa Mbio hizo kunaashiria uwepo wa hali njema ya amani, umoja, utulivu na mshikamano, ambayo inazidi kupamba uzuri na mandhari bora ya visiwa vya Unguja na Pemba.
Hivyo ameeleza kuwa Mbio hizo za Kimataifa ni fursa muhimu ya kuitangaza Zanzibar, ambayo ni Nchi yenye historia kubwa na vivutio vilivyopambwa na utamaduni bora unaogusa asiili za watu wa Mataifa mengi ulimwenguni.
Aidha, Mheshimiwa Othman ametoa changamoto kwa Mamlaka kutumia fursa hiyo ya kila mwaka kuitangaza Zanzibar na Vivutio vyake, ukiwemo Mji Mkongwe wa Asili ambao pia ni sehemu ya Hifadhi ya Kimataifa, huku akitoa wito kwa Waandaaji ambao ni Zanzibar International Marathon, kufanya maandalizi mapema ili kufanikisha Marathon ijayo kuwa na ufanisi zaidi.
Pamoja na kushiriki Masafa ya Kilomita 5 ya Mbio hizo, Mheshimiwa Othman amekabidhi zawadi kwa Washindi pamoja na kuwavisha Medali.
Viongozi mbali mbali wameungana na Makamu wa Kwanza wa Rais katika mbio hizo, ambao ni pamoja na Mstahiki Meya wa Jiji la Zanzibar, Mhe. Mahmoud Mohamed Mussa, Wairi wa Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar, Mheshimiwa Simai Mohamed Said, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanziibar, Mhe. Ali Abdulghulam Hussein na Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja; Mhe. Idris Kitwana Mustafa.
Naye, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanziibar, Mhe. Hamza Hassan Juma, amesema kuwa Michezo hiyo ni muhimu katika mwelekeo mzima wa kuitangaza Sekta ya Utalii na Nchi kwa ujumla wake.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Tigo-Zantel, Bw. Innocent Rwetabura ameishukuru Serikali ya Zanzibar kwa kutoa fursa hiyo ya kukuza vipaji ambavyo ni mlango wa kuitangaza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania michezoni, katika medani za kimataifa.
Amesema hilo limethibiti hivi karibuni ambapo Mshindi wa Tigo Kili Half Marathon iliyopita, Mtanzania Felix Simbu, ameipatia na kuitangaza Nchi baada ya kutwaa Medali ya Fedha, katika Mashindano ya Jumuiya ya Madola, yanayoendelea Jijini Birmingham Nchini Uingereza.
Tigo-Zantel Zanzibar International Marathon 2022, iliyohusisha pia Mbio za Baiskeli, Riadha kwa Watoto na Watu wenye Ulemavu, imewajumuisha washiriki kutoka Mataifa mbali mbali ya Jirani mwa Tanzania na Nje ya Bara la Afrika.