Sunday, November 24

KAMATI YAIPONGEZA TASAF KUSIMAMIA VYEMA FEDHA ZA MRADI

NA ABDI SULEIMAN.

KAMATI ya baraza la wawakilishi yakusimamia Ofisi za Viongozi wakuu wa Kitaifa Zanzibar, imesema imeridhika na utekelezaji wa mradi unaosimamiwa na TASAF Pemba, ya ukarabati wa madarasa Tisa na ujenzi wa ukuta wa skuli ya Piki Wilaya ya Wete.

Kamati hiyo imesema utekelezaji wa mradi huo umezingatiwa viwango bora na vya kisasa zaidi, huku wakiipongeza Tasaf Makao Makuu kwa kuleta fedha na uwezeshaji ambao unatekeleza shuhuli hizo.

Mwenyekiti wa kamati hiyo Machano Othaman Said, aliyaeleza hayo mara baada ya kumaliza ziara ya kutembelea mradi huo na kukagua hali iliyofikiwa, huko Piki Wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Mwenyekiti huyo pia ni Mwakilishi wa jimbo la Mfenesini, aliitaka TASAF kuongeza kasi ya uibuaji wa miradi mipya ili kuwasaidia wananchi na kuweza kufanya shuhuli zao za maendeleo.

Alisema kukamilika kwa ujenzi huo utatoa hamasa kwa wanafunzi, wananchi na walimu wa skuli hiyo katika kuekeza watoto wao katika suala la elimu, ambayo itaweza kuongeza hata ufaulu kwa wanafunzi wa skuli hiyo.

“Ipo haja sasa kufikiria ujenzi wa skuli ya gorofa kutokana na eneo kubwa bado limebakia, tutaishauri serikali kwa hili kwani vizuri kufanya hivyo ikiwa eneo lipo la kutosha,”alisema.

Naye Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo mwakilishi wa jimbo la Bumbwini Mtumwa Peya Yussuf, alisikitishwa na mwamko mdogo wa wananchi kujitokeza katika ujenzi wa skuli hiyo, kwani serikali imeamua kuwasaidia kwa hali ya juu.

“Lazima tunapoibua miradi kama hii lazima na sisi wenyewe tuwe tayari, pale panapohitajika nguvu zetu ili kufikia malengo yetu, kukamilika kwa majengo haya yataweza kutusaidia hata sisi wanafunzi wetu kusoma katika mazingira mazuri,”alisema.

Hata hivyo aliwataka wananchi hao kuwa tayari kujitolewa kwa hali na mali, pale serikali inapoamua kusaidia wananchi wake, katika suala la mendeleo.

Nao wananchi wa Piki wameipongeza serikali ya SMT na SMZ, kwa kuwapatia mradi huo wa skuli, kwani walikuwa na matatizo ya madarasa katika skuli yao jambo ambalo liliwafanya baadhi ya wanafunzi kuwa wengi darasa moja.

Walisema kwa sasa wanachohitaji ni kituo cha afya ambacho kitaweza kuwapunguzia mzigo wakufuata huduma za afya Kisiwani kwa binti abeid.

Mapema akisoma taarifa ya ukarabati wa madarasa hayo tisa,Ofisi na Stoo na ujenzi wa uzio wa skuli hiyo, Suleiman Omar Massoud alisema mradi huo hadi kukamilika kwake utagharimu shilingi 328,987,944.hadi sasa fedha zilizotumika ni shilingi 219,319,250 sawa na asilimia 67% ya fedha iliyotuma na fedha iliyobakia ni 109,668,694 fedha zilizotolewa na mfuko wa maendeleo ya jamii Tanzania (TASAF III).

MWISHO