Saturday, January 4

ZSTC kushuhulikia mifumo ya malipo ya fedha za wakulima

WAZIRI wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar Omar Said Shaaban, akichuma karafuu kuashiria uzinduzi wa msimu mpya wa zao hilo, aliyeshika pakacha ni Mkuu wa Wilaya ya Mkoani Khatib Juma Mjaja, uzinduzi huo umefanyika eneo la Kichunjuu Wilayani humo.
WATENDAJI kutoka Tigo Zantel kulia ni Kaimu Mkuu wa Tigo Pesa wateja na washirika Haidari Chamshama na kushoto ni Meneja Mauzo usambazi kanda ya Pemba Said Massoud Ali, wakichuma zao la karafuu wakati wa uzinduzi wa uchumaji wa zao hilo, uliozinduliwa na waziri wa biashara na maendeleo ya Viwanda Zanzibar, uzinduzi uliofanyika Eneo la Kichunjuu Wilaya ya Mkoani.
KAIMU Mkuu wa Tigo Pesa wateja na washirika Haidari Chamshama, akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa msimu mpya wa uvunjani na ununuzi wa zao la karafuu Pemba, hafla iliyofanyika katika ukumbi wa ZSTC Bandarini Mkoani
MKUU wa Wilaya ya Wete Dk.Hamad Omar Bakar, akizungumza kw aniaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, wakati wa hafla ya uzinduzi wa msimu mpya wa Uchumaji na ununuzi wa Zao la Karafuu Pemba, hafla iliyofanyika bandarini Mkoani

NA ABDI SULEIMAN.

WAZIRI wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar Omar Said Shaabani, amelitaka shirika la biashara la Taifa ZSTC kuhakikisha wanaiboresha mifumo ya malipo kwa njia ya mitandao, ili kuondosha changamoto wakati wa malipo kwa wakulima baada ya kuuza karafuu zao.

Alisema lengo la serikali ni zuri na serikali, itaendelea kusimamia msimamo huo wa malipo kwa njia ya mitandao, ila watendaji wa shirika hilo wanapaswa kuhakikisha mifumo yao inakuwa imara muda wote.

Waziri huyo aliyaeleza hayo wakati alipokua akizungumza na wakulima, kamati za ulinzi na usalama mikoa miwili ya Pemba, katika hafla ya uzinduzi wa msimu mpya wa ununuzi wa karafuu huko bandarini Mkoani.

Alifahamisha kuwa ZSTC inafanya kazi na Tigo-Zantel na PBZ katika suala la malipo kwa mtandao, kwani kilio kikubwa cha wananchi ni tokea serikali ilipoanzisha malipo kupitia mfumo huo.

“Wananchi wamekuwa wakieleza masikitiko yao kwa baadhi ya nyakati, juu ya kucheleweshewa kutiliwa kwa pesa zao kutokana na sababu mbali mbali, sasa hatutaki kuzisikia tena,”alisema.

Aidha Waziri huyo alisema serikali wataendelea kusimamia msimamo huo katika malipo, wanachatakiwa sio kuacha huo mfumo au utaratibu huo, bali ni kuboresha mfumo ili wakulima kupatiwa malipo yao mapema ndani ya muda mfupi.

Waziri huyo alisema wakulima wanafahamu kwa muda mrefu malipo ya mauzo ya zao la Karafuu yalikuwa yakifanywa kwa keshi(fedha mkononi), jambo hilo lilikuwa ni hatari na sio jambo zuri katika uwendeshaji wa shirika, kulikuwa na upotevu wa fedha, pamoja na usalama mzuri wa fedha katika vituo na wakulima.

Mapema akizungumza kwa niaba ya Afisa Mkuu wa Tigo pesa, Kaimu Mkuu wa Tigo Pesa wateja na washirika Haidari Chamshama, alisema zao la karafuu ni muhimu sana Pemba na linachangia kwenye uchumi wa visiwa vya Zanzibar.

Alifahamisha kuwa hadi kufikia Agosti 15 mwaka 2022, tayari wameshalipa Jumla ya shilingi Milioni 624 kwa wakulima wa zao la karafuu 324.

Alisema Zantel kupitia huduma ya Ezypesa walikuwa mstari wambele, kuhakikisha wakulima wanapata malipo yao kupitia simu ya Mkononi kwa wakati muwafaka baada ya kumaliza kuuza karafuu zake.

“Sasa Tigo na Zantel tumeungana na kuwa familia moja kubwa, hii inapelekea huduma za Ezypesa kupatikana kupitia Tigo Pesa itaweza kuwanufaisha wakulima wote,”alisema.

Alisema wafanyakazi wa TigoZantel Pemba wamekuwa mstari wa mbele kuhakikisha wanafanya kazi kwa karibu na wakulima wa zao la kafaruu.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Mkuu wa Wilaya ya Wete Dk.Hamad Omar Bakar, akiwataka wakulima kuendelea kuiyunga mkono serikali na kuwa waaminifu katika uzaji wa Karafuu zao.

Mkurugenzi Mwendeshaji wa ZSTC Bakari Haji, aliwataka wakulima kufuata maelekezo ya wataalamu wa ZSTC wakati wanapofikisha karafuu zao vituoni, pamoja na kuweka mazingira safi karafuu hizo.

MWISHO