Sunday, November 24

MABADILIKO ya Tabianchi chanzo cha migogoro

NA ABDI SULEIMAN.

ATHARI za Mabadiliko ya Tabianchi nchini Tanzania, zinazoendelea kutokea zimekua zikipelekea migogoro baina ya wafugaji na maeneo yaliyohifadhiwa.

Miongoni mwa athari hizo ni ukame wa muda mrefu unaopelekea kukosekana kwa malisho ya wanyama, matukio ya moto, kubadilika kwa miongo ya mvua, hali inayowalazimu wafugaji kuvamia kwenye maeneo yaliyohifadhiwa na kupelekea migogoro.

Hayo yameelezwa mjini Dodoma na Afisa misitu mkuu na kiungo wa Mabadiliko ya Tabianchi Tanzania Dr.Freddy Manyika, wakati alipokua akizungumza na waandishi wa habari kutoka JET.

Alisema mabadiliko ya tabianchi hayabaguwi eneo lililohifadhiwa au halijahifadhiwa, tayari athari zake zimeshaonekana katika maeneo mengi, hali inayopeleka kuathiri mahusiano baina ya taasisi zinazohusika na uhifadhi na wananchi.

Alisema katika maeneo mengi yaliyohifadhiwa kuna bayonuai ambazo Tanzania inajivunia, mabadiliko hayo yanapelekea bayonuai hizo kupotea na kuenea viumbe vigeni vamizi.

Aidha afisa huyo alitolea mfano matukio ya mafuriko yanayotokea Jangwani, Ziwa Victoria mwaka 2020 maji kujaa na kufika katika mahoteli, maji kuvamia makaazi ya watu, ziwa Tanganyika maji yaliongezeka na kufunika mwalo ambao ulijengwa yote yanatokana na mabadiliko ya tabianchi.

Akizungumzia suala la nishati, alisema mabadiliko ya tabianchi yameathiri hata upatikanaji wa nishati ya kuni, kwani ukame wa mara kwa unapelekea mimea kukauka, miti ya kuni kutoweka hali inayopelekea wananchi kukata kuni katika maeneo yaliyohifadhiwa na kuibuka kwa migogoro baade.

“Sote tunafahamu kwamba Mlima wa Kilimanjaro umekua ukitajwa kupungua kwa barafu yake, kwa asilimia 80% tokea mwaka 1912 hadi sasa athari za yote ni mabadiliko ya tabianchi,”alisema.

Kwa Upande wa ukanda wa Pwani, alisema kuna maeneo yamehifadhiwa ndani ya bahari wenyewe, ikiwemo matumbawe ambayo ndio mazalio makuu ya samaki.

Alisema joto la bahari likipanda viumbe vilivyomo baharini vinapotea, maji yanaongezeka na kuathiri viumbe wengine zikiwemo fukwe kuliwa, baadhi ya visiwa kuanza kupotea.

Aidha alisema tayari serikali imeshatumia shilingi Bilioni 4.5 kwa ajili ya kujenga ukuta wa kuzuwia maji ya bahari katika mmaeneo ya Mtwara Mikindani na Sipwese kwa upande wa Zanzibar.

“Ukiangalia utaona eneo ni dogo lakini gharama zake ni kubwa zilizotumika, mfano Ocean Road pale na mwalimu Nyerere tulipata fedha kutoka mfuko wa kuhimili mabadiliko ya tabianchi karibu Bilioni 7, utaona mawe yaliyokua yakimiminwa wakati wa kujenga ukuta,”alisema.

Hata hivyo alisema ukuta mwengine ulijengwa Pangani na kugharimu Dola Milioni 1.5 na serikali pekee haiwezi, lazima iendelee kutafuta fedha kutoka kwa wahisani ili kuhimili mabadiliko ya tabianchi.

Alifahahamisha kuwa Tanzania mchango wake ni mdogo sana katika kuzalisha gesi joto, ambapo kila mtanzania anazalisha gram 0.22 kwa mwaka, wakati Mmarekani au mchina mmoja anazalisha tani 26 kwa mwaka.

Kwa upoande wake Mkuu wa Msafara huo wa waandishi wa habari, Mkurugenzi wa JET Tanzania John Chikomo, alisema JET imekua mstari wambele kuandika habari zinazohusiana na mazingira, uhifadhi na utalii kwa lengo la kuelimisha jamii juu ya athari zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi.

Aidha aliishukuru Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, kwa kkuwashirikisha zaidi wanapokua na masuala yanayohusiana na mazingira, ili jamii iweze kupata uwelewa kwa haraka.

Chama cha waandishi wa habari za Mazingira Tanzania (JET) kwa sasa inatekeleza mradi wa miaka mitano TUHIFADHI MALIASI TANZANIA, kwa ufadhili wa shirika la misaada la la watu wa Marekani (USAID).

MWISHO