Sunday, November 24

WANANCHI WASHIRIKISHWE KWENYE MASUALA YA UHIFADHI

NA ABDI SULEIMAN.

MKURUGENZI wa Wanyamapori, Kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii Dr.Maurus Msuha, amesema uhifadhi wa sasa wa wanyamapori unahitaji ushirikishwaji wa wananchi kwa kiasi kikubwa, na wananchi waweze kuukubali uhifadhi huo.

Alisema kutokana na idadi ya watu inazidi kuongezeka uhifadhi wauwezi kuwa kama ilivyokua kabla ya uhuru, kwani wananchi waliokua wakiishi maeneo ya uhifadhi walikuwa wachache.

Mkurugenzi Msuha aliyaeleza hayo, wakati alipokua akizungumza na waandishi wa habari za Mazingira na Uhifadhi, kutoka Chama cha waandishi wa habari za Mazingira Tanzania (JET) hivi karibuni  jijini Dodoma.

Alifahamisha kuwa sasa kila hifadhi imezungukwa na vijiji, ili tuweze kuwa na uhifadhi endelevu lazima ushirikishwaji wa wadau mbali mbali na wananchi wanaozunguka maeneo haya waweze kuwemo.

“Mipango yetu ya maendeleo na shuhuli nyengine za kibinaadamu, lazima zifanyike kwa kuzingatia mahitaji ya rasilimali, kwani zinamchango mkubwa kwa pato la taifa,”alisema.

Aidha alisema kupitia rasilimali za wanyamapori na utalii kabla ya UVIKO 19, Serikali ikipata asilimia 17% ya pato lataifa kutokana na utalii na sehemu kubwa inazungumzia wanyamapori.

Mkurugenzi Msuha, alisema mwaka 2018 baada ya kuona maeneo ya shoroba ni muhimu, serikali ilikuja na kanuni za shoroba 2008, na kuelezea utaratibu mzima wa namna gani wadau mbali mbali watashirikiana na serikali, ili kuhakikisha shoroba zinahifadhiwa na zinazokaribia kupoteza hadhi yake zinarudishwa katika mazingira ya asili yake.

“Ili kupunguza migogoro inayotokana na mwingiliano wa wanyamapori na binaadamu, lazima tuhakikishe wanyama hao wanaendelea kukua, na kuwa uhuru wakutembeleana kuruhusu ubadilishaji wa vinasaba,”alisema.

Akizunguzmia suala la changamoto iliopo, alisema ni ardhi iliyopo nje ya maeneo yaliyohifadhiwa rasmi, wanachokifanya ni kushirikiana na wadau mbali mbali kutambua umuhimu wake na kuwaomba wananchi waridhie, kufanywe mipango bora ya matumizi ya ardhi, ili sasa shuhuli zinazoenda kufanyika ziweze kuzingatia umuhimu wa wanyama kupita bila ya kuzuwiwa.

Alisema kwa sasa wameanzisha mchakato wakuzitambua sheroba zote, sio kazi rasihisi ni kazi endelevu zipo wanazozifahamu na wasizosifahamu, ili kuona wanaweza kuzihifadhi.

“Kutokana na changamoto za binaadamu mwaka 1964 Hifadhi ya Taifa ya Tarangire ilikua na Koridoo 9, kufikia 1983 ilikua koridoo sita, ikifikia 2011 zilibaki tatu, tafsiri ni kwamba nyengine zimezikwa inatokana na idadi ya watu kuongezeka,”alisema.

Hata hivyo alisema hawawezi kutekeleza usimamizi wa shoroba bila ya kushirikisha Wizara nyengine, kwani Wizara ya Maliasili na Utalii inahusu wadau wengi ndani ya serikali nan je ya serikali katika utekelezaji wake.

Aliongeza kuwa, kwa sasa wanahitaji kuwa mpango bora wa matumizi na sio kwenye shoroba, hata maneo ya nje pembezoni mwa hifadhi ili kuhakikisha wananchi hawaathiriki na matukio ya wanyama wakali na uharibifu.

Akitolea mfano maeneo ya makuyuni miaka 10 iliyopa, nyumba zilikua hazipo wanyamapori wakitoka Tarangire kwenda juu na kupita kwenye msitu, sasa lazima kuwe na mpango bora wa matumizi ya ardhi, ili mwisho wa siku wasiathirike na wanyama wakali.

Nao waandishi wa habari walimtaka Mkurugenzi huyo kuhakikisha maeneo ya hifadhi ya wanyamapori yanalindwa, ili kuwa ufugaji endelevu na wakisasa.

Mkurugenzi mtendaji wa JET John Chikomo, alisema tayari waandishi wameshatembelea baadhi ya maeneo ya hifadhi ya wanyamapori, ikiwemo kwa kuchinja na kujionea hali halisi ilivyo.

Chama cha waandishi wa habari za Mazingira Tanzania (JET) kwa sasa inatekeleza mradi wa miaka mitano TUHIFADHI MALIASI TANZANIA, kwa ufadhili wa shirika la misaada la la watu wa Marekani (USAID).

MWISHO