NA HAJI NASSOR, PEMBA.
WANAWAKE wa kiislamu ambao wanachuma mali pamoja na waume zao, wametakiwa kufuatilia haki zao za kupatikana kwa mali, mara baada ya ndoa kuvunjika, kwani sheria ya Mahakama ya kadhi, nambari 9 ya mwaka 2017 imetoa haki hiyo.
Ilielezwa kwenye sheria hiyo, kifungu cha 5 (1) (f) kuwa, mwanamke aliyeachwa na ikiwa wamechuma mali pamoja na aliyekuwa mume wake, anaweza kulalamika mahakamani, kupata mchango wa kuanzia maisha.
Hayo yalibainika hivi karibuni, kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika ofisi ya PEGAO, Chake chake, wakati Mkurugenzi wa asasi hiyo Hafidh Abdi Said, alipokuwa akitoa taarifa kwa waandishi hao, juu ya utekelezaji wa haki za mwanamke.
Alisema, wapo baadhi ya wanaume wamekuwa wakichuma mali pamoja na mwanamke, ingawa baada ya ndoa kuvunjika, hajali na wala hazingatii suala la kumpa mchango wowote mwanamke, kwa ajili ya kuanzia maisha.
Alieleza kuwa, ndio maana wakati umefika sasa, kwa wanawake waliomo kwenye ndoa, na mara wanapoachwa na ikiwa kuna mali wameichuma na aliyekuwa mume wake, kuitumia mahakama ya kadhi kulalamika.
‘’Wapo wanandoa wanaishi zaidi ya miaka 10 au 25 kwenye ndoa, na wakati mwanamme anaoa hakuwa na mali, lakini baada ya muda na ustahamilivu wa mwanamke, anapoachwa hakuna hata mchango wowote anaopewa,’’alifafanua.
Alieleza kuwa, baada ya mwanamke kulalamika, mahakama huangalia uwiyano wa mali iliyochumwa katika uhai wa ndoa yao, na kisha nae kupewa chochote kwa ajili ya kuanzia maisha ya anapokwenda.
Mkurugenzi huyo alisema, uwepo wa sheria hiyo, ni kuondoa uonevu wa muda mrefu kwa wanawake, kuishi katika wimbi la umaskini, na hasa baada ya ndoa kuvunjika.
‘’Ingawa changamoto iliyopo kwenye sheria hiyo, haikuelezwa kuwa ni lazima, bali imeeleza kuwa ni mchango wa kumsaidia mwanamke, kwa ajili ya kuanzia maisha yake,’’alisema.
Kuhusu sheria ya Ajira namba11 ya mwaka 2005, Mratibu wa Chama cha waandishi wa habari wanawake Tanzania TAMWA-Zanzibar ofisi ya Pemba Fat-hiya Mussa Said, amesema imetoa ulinzi mzuri kwa mwanamke, na kinachotakiwa ni utekelezaji wake.
Alieleza kuwa kifungu cha 10 (2) cha sheria hiyo kuwa, mwajiri analazimika kuthibitisha malipo ya mishahara sawa, kati ya mwanamke na mwanamme, wenye elimu na ngazi zinazowiayana.
Aliekeza kuwa, ulinzi mwengine upo kwenye kifungu cha 11, kinakemea unyanyasaji wa kijinsia, kumtaka muajiriwa mwanamke kimapenzi, matumizi ya vitisho, lugha inayoashiria mapenzi kwa mtumishi huyo.
‘’Lakini pia ni kosa, kwa muajiri, kuacha kumuajiri mwanamke, kwa madai kuwa muda mwingi hatokuwepo kazini, kwa sababu ya kujifungua na kunyonyesha, kwani huo ni aina ya udhalilishaji,’’alisisitiza.
Katika hatua nyingine, Mratibu huyo wa TAMWA, alisema ulinzi mwengine alionao mwanamke ni kupata mapumziko ya siku 100, ikiwa amejifungua watoto mapacha, zaidi ya siku za kawaida anapojifungua mtoto mmoja.
Kwa upande wake, mwanaharakati wa haki za wanawake na watoto, Safia Saleh Sultan, alisema ulinzi mwengine wa sheria kwa wanawake, ni uwepo wa marufuku wa kuajiriwa kwenye mionzi na kemikali za sumu, zinazotishia usalama wake na mtoto.
‘’Kwenye sheria hiyo ya Ajira kifungu cha 83 (1) na kifungu cha 84 (4), kinakataza kumpa kazi mwanamke wakati wa usiku, katika shughuli za viwanda, na hasa ikiwa usalama wake uko hatarini kimazingira,’’alifafanua.
Wakili wa watoto wanaokinzana na sheria kutoka Kituo cha Huduma za sheria Zanzibar ‘ZLSC’ tawi la Pemba Siti Habib Mohamed, anasema sheria ya Elimu nambari 6 ya mwaka 1982, kifungu cha 19, kinaelezea ulazima kwa kila mtoto aliyefikia umri wa miaka 7 na hajafikia miaka 13 kuandikishwa elimu ya msingi.
‘’Kama wapo wazazi na walezi hadi leo hii, wanawazuia watoto wao wa kike, wasipate haki ya elimu, wanapingana na sheria hiyo na hawawatendei haki,’’alifafanua.
Hata hivyo wakili huyo alisema, ulinzi mwengine upo kwenye sheria ya Kuwalinda wari na mtoto wa mzazi mmoja, nambari 4 mwaka 2005 kifungu cha 5 (1), kinataka mwari, mtoto wa kike au mwanamke ambae hajaolewa anaweza kufungua kesi ya kudai ya matunzo mahakamani dhidi ya mtu aliyepma ujauzito.
Kwa upande mwengine, wakili huyo alisema pia wanawake wanalindwa kwenye sheria ya Adhabu nambari 6 ya mwaka 2018, kifungu cha 108 na 109 inayotoa ulinzi na adhabu ya kifungo cha mtu atakaepatikana na hatia ya ubakaji.
Mratibu wa mradi wa kuiwezeshaji jamii kudai haki zao za uongozi, siasa na demokrasia ‘SWIL’ kutoka PEGAO Dina Juma, ameziomba mamlaka husika, kusimamia utekelezaji wa sheria hizo, ili kundia la wanawake lipate haki zao.
Mwisho