Saturday, March 1

Rais Dk Hussein Mwinyi akutana na Balozi wa Uganda nchini

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussin Ali Mwinyi akisalimiana na Balozi wa Uganda Nchini Tanzania Mhe.Fred Mwesigye (kushoto) alipofika Ikulu Jijini Zanzibar leo kwa Mazungumzo pamoja na kujitambulisha.[Pichana Ikulu] 03/10/2022.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussin Ali Mwinyi (kulia) akimsikiliza mgeni wake Balozi wa Uganda Nchini Tanzania Mhe.Fred Mwesigye wakati wa mazungumzo yao leo alipofika Ikulu Jijini Zanzibar kujitambulisha.[Pichana Ikulu] 03/10/2022.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussin Ali Mwinyi (kulia) akizungumza na mgeni wake  Balozi wa Uganda Nchini Tanzania Mhe.Fred  Mwesigye wakati   alipofika Ikulu Jijini Zanzibar leo   kujitambulisha.[Pichana Ikulu] 03/10/2022.


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussin Ali Mwinyi (kulia) akiagana na mgeni wake  Balozi wa Uganda Nchini Tanzania Mhe.Fred  Mwesigye baada ya mazungumzo yao leo wakati alipofika Ikulu Jijini Zanzibar leo  kujitambulisha.[Pichana Ikulu] 03/10/2022.

Zanzibar                                                                                       03.10.2022

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema kuna umuhimu mkubwa kwa wananchi wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kuendeleza uhusiano na ushirikiano baina yao kwa kuzingatia udugu wa kihistoria uliopo.

 

Dk. Mwinyi amesema hayo Ikulu Zanzibar alipozungumza na Balozi wa  Uganda nchini Tanzania Fred Mwesigye, aliefika kujitambulisha.

Amesema wananchi wa nchi za Jumuiya Afrika Mashariki wana udugu wa kihistoria, hivyo ni vyema kuwepo utaratibu wa kutembeleana na kushirikiana katika mambo mbali mbali.

Alieleza kuwa Zanzibar ni kisiwa ambapo Sekta ya Utalii imepewa kipaumbele na kusema  kuna maeneo mbali mbali ya kushirikiana.

Aidha, alisema kuna umuhimu wa kuendeleza mashirikiano ya  kibiashara kati ya Uganda na Zanzibar na Tanzania kwa ujumla, kwa viongozi kufanya mazungumzo ili kuwawezesha wafanyabaishara wa nchi mbili hizo kuendeleza biashara zao.

Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kumshukuru Rais Yoweri Museveni wa Uganda kwa mwaliko aliotuma kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu wa kuzuru nchi hiyo hapo baadae, ambapo Rais Dk. Mwinyi anatarajiwa kumwakilisha.

“Naomba unifikishie salamu zangu za dhati kwa Rais Museveni ……….. tunafahamiana kwa kipindi  kirefu sasa”, alisema.

Nae, Balozi wa Uganda nchini Tanzania  Fred Mwesigye alisema nchi hiyo inahitaji walimu wa kufundisha Lugha ya Kiswahili kutoka Zanzibar baada ya Serikali kufikia uamuzi wa kuanzisha somo la Lugha ya Kiswahili katika mitaala ya skuli zote nchini humo.

Alisema kupitia wadhifa wake wa Ubalozi, atatumia nafasi hiyo kuutangaza uzuri wa Zanzibar nchini humo, ikiwa hatua ya kuimarisha ushirikiano wa kibiashara kati ya nchi mbili hizo.

Aidha, alisema Uganda inathamini mchango mkubwa wa wananchi wa Serikali ya  Tanzania, hususna katika suala la Ukombozi wa Bara za Afrika pamoja na kuisaidia Uganda katika harakati za  kumpindua aliekuwa Rais wa nchi hiyo Dikteta Idd Amin Dada mnamo mwaka 1978.

Imetayarishwa na Idaya ya Mawasiliano

Ikulu Zanzibar.