Thursday, January 16

Serikali imekuwa ikifanya juhudi mbali mbali kuimarisha Biashara na Uwekezaji pamoja na kuvutia Wawekezaji katika sekta ya Uchumi wa Buluu.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi (kushoto) akitoa hutuba ya ufunguzi wa mkutano wa 26 wa utafiti uliofanyika leo Golden Tulip Hotel Kiembesamaki,(kulia)Mkurugenzi Mtendaji Taasisi ya Sera na Utafiti(REPOA) Dr.Donald Mmari,Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mhe.Zubeir Ali Maulid na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena Ahmed said.[Picha na Ikulu]

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali imekuwa ikifanya juhudi mbali mbali kuimarisha Biashara na Uwekezaji pamoja na kuvutia Wawekezaji katika sekta ya Uchumi wa Buluu.

Mwinyi amesema hayo katika Ufunguzi wa Mkutano wa 26 wa utafiti uliofanyika katika Hoteli ya Golden Tulipo Airport Zanzibar, uliobeba kauli mbiu ya  ‘uendelezaji biashara  kwa kuzingatia  mabadiliko ya Tabianchi ili kujenga uchumi shindani’.

Amesema Serikali  imekuwa ikifanya juhudi kubwa kuimarisha Biashara na Uwekezaji kwa lengo la kuinua uchumi wake pamoja na kuvutia Wekezaji ili kuwekeza katika sekta za Uchumi wa Buluu unaohusisha Uvuvi, Utalii, mafuta na Gesi pamoja na safari za Baharini.

Alisema juhudi hizo pia zimekuwa zikifanyika kuvutia Wawekezaji katika sekta ya Kilimo, ICT, viwanda sambamba na Serikali  kuimarisha Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume pamoja na Nbandari ya Malindi ambpo ni milango mikuu ya Biashara na Utalii.

Dk. Mwinyi alisema Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania inatekeleza mpango wa maendeleo wa kujenga ushindani wa Uchumi wa Viwanda na maendeleo ya watu, ambapo miongoni mwa vipaumbele vyake ni kuimarisha uwekezaji na biashara.

Alisema kutokana na mabadiliko ya Tabianchi, Tanzania inashuhudia kushuka kwa kiwango cha mazao ya kilimo, upatikanaji wa samaki, mazao ya mwani pamoja na mifugo.

Alisema pamoja na hatua mbali mbali zinazochukuliwa na Serikali, bado mahitaji ay tafiti ni muhimu ili kuiwezesha Serikali kupanga sera mbali mbali.

Alipongeza REPOA, CRDB  pamoja Wizara ya biashara na maendeleo ya Viwanda kwa kuja na  kauli mbinu ya ‘Uendelezaji wa biashara kwa kuzingatia mabadiliko ya tabianchi ili kujenga uchumi shindani’ na kusema imekuja kwa wakati muafaka na kusema  mkutano huo uliowashirikisha watafiti na wansayansi utajadili hoja nzito.

Alizpongeza taasisi za REPOA, CRDB pamoja na wadau wote walioshiriki katika mkutano huo , akibainisha matumaini yake ya kuendeleea kuinga mkono Serikali zote mbili katika dhamira ya kukuza uchumi wa nchi.

Nae, Waziri wa Nchi (OR) Uwekezaji Soraga kwa niaba ya Waziri wa Biashara, Maendeleo ya Viwanda  alisema REPOA, CRDB  pamoja Wizara hiyo zimeandaa mkutano huo ili watafiti kubaini fursa na changamoto mbali mbali zinazotokana na mabadiliko ya tabia nchi ili kuziwezesha taasisi na wadau kuwa na uzalishaji wenye tija.

Aidha, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Abdulmajid Nsekela alisema rasilimali fedha zinahitajika katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi, ikiwemo suala la uwekaji wa miundo mbinu.

Alisema mabadiliko ya tabia nchi huathiri sekta mbali mbali ikiwemo za kibiashara pamoja na kilimo na hivyo kupunguza tija katika uzalishaji, kuleta usumbufu pamoja na kupunguza mitaji na kubainisha umuhimu wa wadau kupata fursa ya kujadiliana.

Alieleza kuwa CRDB ikiwa sekta ya fedha imehakikisha inatimiza wajibu wake kwa kuja na Programu maalum kuhusiana na uimarishaji wa mazao ya chakula kwa Watanzania wote wa Bara na Zanzibar.

Alisema Programu hiyo inatarajiwa kuwafikia Watanzania wapatao Milioni sita, lengo likiwa ni kuwawezesha  wakulima kwa kuwapatia mikopo.

Nsekela alisema CRDB iko tayari kushirikiana na kufanya kazi pamoja na Wawekezaji wote weye lengo la kuwekeza kupita mradi huo.

Aidha, Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU) nchini Tanzania Manfredo Fanti alisema Umoja na Ulaya na Tanzania zinafanya kazi kwa pamoja ili kufikia malengo ya kuongeza uzalishaji wa mazao kulinganna na ubora na ongezeko la mazao kwa kuzingatia mabadiliko tabia  nchi.

Mkutano huo wa 26 wa kila mwaka, umeandaliwa kw apamoja kati ya Shirika REPOA, CRDB na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ukiwashirikisha watafiti, wanasayasi pamoja na wadau mbali mbali.

Imetayarishwa na Idaya ya Mawasiliano

Ikulu Zanzibar.