Monday, November 25

Watu wenye mahitaji maalumu wanamahitaji zaidi ya msaada wa kisheria-MWAKILISHI kutoka UWZ

NA ABDI SULEIMAN.

MWAKILISHI kutoka Umoja wa watu wenye ulemavu Zanzibar Shaibu Abdalla Mohamed (UWZ), amesema taasisi za watu wenye mahitaji maalumu, zinanafasi muhimu sana katika upatikanaji wa msaada wakisheria, kwa sababu wao ndio watetezi wa mbele kwa watu wa makundi yao.

Alisema makundi hayo yanahitaji sana elimu ya msaada wakisheria, hivyo katika makundi hayo zipo asasi zimejikita moja kwa moja, kuhudumia watu hao na ndio wanaowafahamu wapi walipo na wanahitaji nini na nini na vipi wanaweza kuwafikia.

Aliyaeleza hayo wakati alipokua akiwasilisha mada juu ya Upatikanaji wa msaada wa kisheria kwa watu wenye mahitaji maalumu na walio katika mazingira hatarishi, katika jukwa la Msaada wa Kisheria lililofanyika hivi karibuni.

Alisema watu wenye mahitaji maalumu wanamahitaji zaidi ya msaada wa kisheria, kutokana na sifa zao na kutokua na uwezo kabisa au kuwa na uwezo hafifu katika kutetea na kufikia haki na fursa zao.

Aidha alifahamisha kuwa msaada wa kisheria ni huduma na mkombozi katika mustawi wa maisha yao, kwani watu wenye mahitaji maalumu wanakuwa hawana uwezo madhubuti wa kujitetea na hivo kuzikosa haki zao kwa urahisi.

“Watu wenye mahitaji maalumu wanakosa utetezi kwenye jamii, kwa sababu ya hali zao na mitazamo ya jamii juu ya yao na kudharauliwa,”alisema.

Hata hivyo alisema watu hao ni rahisi kutenga na kusahauliwa, katika ushiriki na utoaji wa maamuzi ya mambo hata yale yanaowahusu moja kwa moja, lazima wajengewe uwezo na kushirikishwa kwa namna, ili mawazo yaweze kusaidia kungamua mambo mbali mbali yenye tija kwao.

Msaidizi wa sheria kutoka WEPO Kombo Ali Hamad, alisema watu wenye ulemavu wanamchango mkubwa katika serikali na mashirika, lakini hawashirikishwi ipasavyo ipasavyo katika taasisi zinazoomba msaada.

Naye Mwakilishi kutoka ZAPAO Ahmed Abdalla Mussa, alisema serikali imekua ikiwashirikisha ipasavyo watu wenye mahitaji maalumu, kwani imeweza kuwarudisha skuli watoto 10,000 kutokana na matatizo mbali mbali kati ya watoto 35,000.

Hata hivyo aliitaka LSF na Idara ya Katiba na Msaada wa kisheria Zanzibar, kuwa na mawasiliano ya moja kwa moja na watu wenye mahitaji maalumu ili kuona wanafikia malengo yao.

MWISHO