NA KHADIJA KOMBO.
Jamii Kisiwani Pemba imeshauriwa kufanya uchunguzi wa kiafya mara kwa mara ili kufahamu mwenendo wa afya zao pamoja na kuchukua hatua za haraka katika kupata matibabu iwapo watagundilika na tatizo.
Akizungumza mara baada ya kufanya upasuaji kwa wagonjwa wanaosumbuliwa na mtoto wa jicho huko Hospitali ya Wete Pemba Dr. Njau Senkondri amesema pamoja na kuwa matatizo hayo huwapata watu wenye umri mkubwa lakini pia kuna sababu kadhaa zinazoweza kusababisha tatizo hilo yakiwemo magonjwa ya kisukari na presha hivyo ni vyema kufika hospitali mapema na kuweza kuyashughulikia kwa haraka.
Aidha amewataka wagonjwa ambao tayari wameshafanyiwa upasuaji kufuata taratibu walizopewa na wataalamu ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza.
Kwa upande wake mratibu wa huduma za macho Zanzibar Dr. Fatma Juma amewataka wale wote waliofanyiwa upasuaji iwapo litajitokeza tatizo lolote lile wafike hospitali kwa haraka ili waweze kuangaliwa kwa karibu.
Zaidi ya watu 60 ambao walikuwa wakisumbuliwa na mtoto wa jicho tayari wameshapatiwa matibabu katika kambi maalum ya matibabu ya macho huko hospitali ya Wete, kambi kama hio kuendelea katika Hospitali ya Abdalla Mzee Mkoani.
MWISHO.
KUANGALIA VIDEO YA HABARI HII BOFYA HAPO CHINI