Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amelipongeza Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU) kwa kuendeleza kutoa Elimu ya ufundi ili kurahisisha upatikanaji wa elimu ya ufundi Nchini.
Mhe. Hemed ameeleza hayo wakati akifungua jengo la Skuli ya ufundi ya JKU Mtoni ikiwa ni sehemu ya Shamrashamra za kutimiza miaka 59 ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar.
Amesema ujenzi huo ni hatua ya kupongezwa Jeshi hilo Chini ya usimamizi wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ kwa kusimamia vyema suala la upatikanaji wa elimu na kueleza kuwa jambo hilo linatofautisha kikosi cha JKU na Vikosi vyengine.
Aidha ameeleza kufurahishwa kwake kuona kuwa jengo hilo la ghorofa mbili limejengwa na mafundi wa JKU kuanzia mwaka 2018 na kukamilika kwake 2023 ambapo ni kielelezo tosha cha Jeshi hilo kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuwaletea maendeleo wananchi wake.
Sambamba na hayo Mhe. Hemed amefurahishwa na Mitaala ya Skuli hiyo kujumuisha masomo yanayohusiana na dhana ya Uchumi wa buluu, muhtasari wa somo la Uvuvi na Ubaharia hatua ambayo inakwenda sambamba na dhana ya Serikali ya Awamu ya nane kukuza uchumi wa Buluu.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ametumia fursa hiyo kuwaomba wadau wa maendeleo kuendelea kubuni miradi mbali mbali ambayo italeta tija kwa maslahi ya mapana ya wananchi.
Aidha amewasihi wanufaika wa Skuli hiyo ya ufundi kulinda miundombinu ya majengo ili libaki katika haiba yake pamoja na kutunza vifaa ili viweze kuwanufaisha vijana wengi.
Akizungumzia Mapinduzi matukufu ya Januari 1964 Mhe. Hemed ameeleza kuwa lengo la kufanyika kwa Mapinduzi ni kurekebisha hali za Wananchi kwa kuondosha ubaguzi na unyanyasaji uliokuwa ukifanyika kwa kuwakosesha haki wananchi ikiwemo Elimu, Fursa za kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Nae Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ Mhe. Masoud Ali Muhamed ameeleza kuwa ujenzi wa jengo hilo unaakisi azma ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar kujisimamia katika nyanja tofauti na kuhakikisha kuwa Wizara itaendeleza azma hiyo ili kuwaletea manufaa wananchi wa Zanzibar.
Aidha amemshukuru Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambae pia ni Kamanda Mkuu wa Vikosi na Idara Maalum za SMZ Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi kuendeleza kituo hicho kwa kukamilisha jengo hilo na kueleza kuwa wataendelea kuthamini juhudi hizo kwa hali zote.
Kwa upande wake Mkuu wa Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU) Kanal Makame Abdalla Daima ameeleza kuwa kuanzishwa kwa Skuli ya ufundi JKU Mtoni ni Kusaidia vijana walikosa sifa ya kujiendeleza na Taasisi za Elimu ya juu nchini ili kuwapatia ujuzi wa ufundi mbali mbali waweze kujikwamua kimaisha.
Aidha amesema jengo hilo litapunguza uhaba wa nafasi kwa wanafunzi ambao wataweza kupata ujuzi katika mazingira mazuri zaidi na kuiomba Serikali kujenga jengo kama hilo kisiwani Pemba kwa kuwarahisishia vijana wanaoishi kisiwani humo.
Abdulrahim khamis
Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar