(PICHA NO:ABDI SULEIMAN, PEMBA)
NA HANIFA SALIM, PEMBA
WAZIRI wa Habari, vijana, utamaduni na michezo Zanzibar Tabia Maulid Mwita amemtaka mkandarasi wa uwanja wa michezo Gombani, kuhakikisha anafanya kazi kwa wakati na kwa mujibu wa ubora ambao umo katika mikataba yao waliokubaliana.
Waziri Tabia aliyasema hayo katika uwanja wa michezo Gombani Chake chake Kisiwani Pemba, mara baada ya kukagua uwanja huo ambao unaendelea na ukarabati mkubwa ambapo kwa sasa upo katika hatua za awali.
Alisema, lengo la kufanyiwa ukarabati wa uwanja huo ni kuona unachezeka na timu za kitaifa na kimataifa hivyo, alimtaka mkandarasi huyo kuhakikisha anafanyakazi kwa mujibu wa maelezo waliokubaliana.
“Kwa sababu tuna mashindano mengi lakini pia tunataka kuwa na mfumo wa kuendelea kualika vilabu na timu nyengine za kitaifa na kimataifa kutoka nje ya Zanzibar na Tanzania”, alisema.
Alieleza, Wizara ya habari, vijana, utamaduni na michezo itaendelea kusimamia majukumu yake ikiwemo kuendeleza miondombinu katika sekta hiyo, kwani alisema itakapopewa kipaumbele michezo, itaendelea na kuimarika.
“Katika paa la jukwaa kuu la uwanja mkandarasi lazima afanye utafiti wa kina kwani tunataka inapotokezea shughuli, katika kipindi cha jua kali au mvua isiweze kuingia kwenye eneo hili, tutumie utaalamu wetu ikiwa ni kuliinamisha ama kuliongeza”, alisema.
Aidha, aliwataka wananchi kufahamu kwamba uwanja huo ni mali ya wananchi wote na baada ya matengenezo hayo watapata fursa sawa ya kuutumia kwa mujibu wa taratibu na kanuni ambazo zitakua zimewekwa na wizara husika.
Hata hivyo, aliwasisitiza watendaji wanaosimamia sekta ya michezo akiwemo Katibu Mkuu wizara ya habari, vijana, utamaduni na michezo kuhakikisha wanakua ma mawasiliano ya mara kwa mara na wakandarasi wa uwanja huo.
MWISHO.