Saturday, January 18

Prof. Mbarawa aweka jiwe la msingi Hanga la Askari wa KZU,awapongeza kwa kuokoa fedha nyingi katika ujenzi huo.

 

WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi Tanzania Prof.Makame Mbarawa, akipata maelezo juu ya ujenzi wa Nyumba za askari wa Zimamoto na Uokozi huko Finya Wilaya ya Wete, kutoka kwa Mrakibu msaidizi wa Zimamoto Zanzibar Simai Machano Tona, ikiwa ni shamrashamra za miaka 59 ya Mapinduzi ya Zanzibar.(PICHA NA ABDI SULEIMAN,PEMBA)
BAADHI ya Askari wa kikosi cha Zimamoto na Uokozi Pemba, wakifuatilia hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi ujenzi wa Nyumba za makaazi kwa askari hao, huko Finya Wilaya ya Wete ikiwa ni shamrashamra za miaka 59 ya Mapinduzi ya Zanzibar.(PICHA NA ABDI SULEIMAN, PEMBA)
MKUU wa Mkoa wa Kaskazini Pembva Salama Mbarouk Khatib, akizungumza katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi nyumba za makaazi za askari wa Zaimamoto na Uokozi Pemba, huko Finya Wilaya ya Wete ikiwa ni shamrashamra za miaka 59 ya Mapinduzi ya Zanzibar.(PICHA NA ABDI SULEIMAN, PEMBA)
BAADHI ya wanafunzi na wananchi kutoka maeneo mbali mbali ya shehia ya Finya Wilaya ya Wete, wakifuatia hafla ya uwekeaji wa jiwe la masingi nyumba za makaazi za askari wa Zaimamoto na Uokozi Pemba, huko Finya Wilaya ya Wete ikiwa ni shamrashamra za miaka 59 ya Mapinduzi ya Zanzibar.(PICHA NA ABDI SULEIMAN, PEMBA)
WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi Tanzania Prof.Makame Mbarawa, akizungumza na wananchi wa finya na askari wa Zimamoto na uokozi Pemba, mara baada ya uwekaji wa jiwe la msingi ujenzi wa Nyumba za askari wa Zimamoto na Uokozi huko Finya Wilaya ya Wete, ikiwa ni shamrashamra za miaka 59 ya Mapinduzi ya Zanzibar.(PICHA NA ABDI SULEIMAN, PEMBA)

NA HANIFA SALIM, PEMBA

WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi wa serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Prof. Makame Mnyaa Mbarawa amesema,  ujenzi wa Hanga la Askari wa kikosi cha Zimamoto na Uwokozi (KZU) Finya Pemba umefikia katika hatua nzuri na wenye ubora unaokidhi viwango vinavyostahili.

Aliyasema hayo katika uwekaji wa jiwe la msingi Hanga la Askari wa Kikosi hicho huko Finya Wilaya ya Wete Pemba, ikiwa ni shamra shamra za maadhimisho ya miaka 59 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Alisema, uwekaji huo wa jiwe la msingi hanga la kulala wapiganaji hao ni utekelezaji wa vitendo malengo halisi ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964, ambapo muasisi wake marehemu Mzee Abeid Amani Karume alipenda kuona wafanyakazi wakikaa katika mazingira mazuri.

“Nawapongezeni sana (KZU) kwa kazi nzuri mlioifanya nimefarajika sana kwani kazi hii ingelazimika kupewa mkandarasi lakini mliamua muifanye wenyewe, ukweli mumeokoa fedha nyingi tujifunze utamaduni kama huu sio
lazima kila kazi kupewa mkandarasi”, alisema.

Aidha aliwataka Askari wa (KZU) litakapokamilika jengo hilo na kuhamia wawe majirani wema kwa wananchi wa Finya, ili iendelee kuwa sehemu salama zaidi pale ambapo watakuwa karibu nao.

Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Salama Mbarouk Khatib alisema, watu wengi walikuwa hawaoni  kazi zinazofanywa na kikosi hicho lakini kwa sasa wameweza kutambua lengo na azma ya Seriakli kuweka kikosi hicho.

“Tumekuwa tukiona athari nyingi zinazojitokeza ikiwemo majanga ya moto hasa katika kipindi cha mwaka 2022 lakini kujengwa Ofisi hizi karibu na wananchi zitaweza kuokoa mambo mbali mbali ikiwemo maisha ya watu”,
alisema.

Alieleza, kikosi hicho kuwa karibu na wananchi ni jambo la busara sana kwani, wananchi wa Finya pamoja na vitongoji jirani watakapotokezewa na majanga ikiwemo ya moto itakuwa ni njia rahisi ya kupatiwa huduma.

Akitoa taarifa ya kitaalamu Katibu mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa Serikali za Mitaa na Idara maalumu za SMZ Zanzibar Issa Mahfoudh Haji alisema, ujenzi huo ulianza Julai 22 mwaka 2022 na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa Februari mwaka huu.

Alifahamisha, ujenzi huo kwa sasa umefikia asilimia 60% ambapo baada ya kukamilika kwake wanatarajia kuanza ujenzi mwengine wa jengo jengine la Gorofa moja, ujenzi huo wa majengo yote mawili utagharimu
zaidi ya shilingi milioni 198 ambapo nguvu kazi ya waliojenga jengo hilo ni Maofisa na Wapiganaji wa kikosi hicho.

Alieleza  kwa upande wa wataalamu walilazimika kuchukuwa wa nje ya kikosi chao wakishirikiana na kikosi hicho jambo ambalo   limeweza kupunguza gharama za ujenzi kwa asilimia 40%, ambapo kukamilika kwa jengo hilo kutaongeza  ufanisi wa utendaji kazi.

Mapema Mwakilishi wa Jimbo Gando Maryam Thani Juma alisema, matarajio yake nikuona baada ya kukamilika majengo hayo changamoto zinazowakumba wananchi ikiwemo ajali za moto zinapotokea watakuwa mstari wa mbele kuwasaidia na kulinda mali zao.

MWISHO.