NA HANIFA SALIM, PEMBA
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk, Philip Isdor Mpango amesema, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imedhamiria kuifanyia kazi changamoto ya uhaba wa madarasa, walimu wa masomo ya Sayansi na Hesabati, kwa kuhakikisha wanapatikana ili kukidhi mahitaji yaliyopo.
DK, Mpango alisema kuwa, Serikali imedhamiria kujenga miondombinu mengine kama vile maabara za sayansi, vyumba vya komputa, maktaba pamoja na kuongeza idadi ya Dakhalia ili kuwawezesha watoto kupata muda mzuri wa kupitia masomo yao.
Aliyaeleza hayo katika ufunguzi wa skuli ya msingi Kwale Wilaya ya Chake chake Kisiwani Pemba, ikiwa ni shamra shamra za maadhimisho ya miaka 59 ya Mapinduzi ya Zanzibar ambayo ilijengwa kupitia fedha za ahuweni za UVIKO.
DK, Mpango alisema, ujenzi wa Skuli ya gorofa ya msingi Kwale ni moja ya jitihada za Serikali katika kuhakikisha inatimiza azma ya
kuwapatia watoto wote haki ya elimu bora, ikiwa ni utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020-2025.
Alifahamisha kuwa, Mapinduzi yanahistoria pana hivyo ni vyema kizazi cha sasa kurithishwa historia hiyo ili wajue umuhimu wa kuyaenzi na kuyalinda, kwani wazee wao wakiongozwa na Mzee Abeid Amani Karume waliamua kufanya Mapinduzi ili kujikomboa na mazila ya kikoloni.
“Katika utawala wa kikoloni kulikuwa na unyanyasaji mkubwa kiasi kwamba hata uhuru wa kujiwekea maendeleo haukuwepo na ni watu wachache ambao walipata fursa ya elimu ubaguzi huu ulikuwepo hata kwa huduma mbali mbali za kijamii”, alisema.
Alieleza, kupitia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hadi mwaka 2022 takwimu zinaonesha skuli za msingi zinazotoa elimu ni 576 zikiwa na jumla ya wanafunzi (laki tatu, hamsini na saba elfu na tisini na tisa) jambo ambalo ni la kujipongeza kwa Wazanzibar.
Alifahamisha, Serikali ya Mapinduzi imedhamiria kuifanya elimu kuwa ni sekta ya kipaumbele, ambapo mara tu baada ya Mapinduzi imeweza kuongeza Skuli katika Mikoa yote ya Unguja na Pemba sambamba na kuboresha miondombinu.
Aidha alisema, kuna Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kuiunga mkono Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuwaletea wananchi wake maendeleo, hivyo aliwataka wananchi kushirikiana kuhakikisha haki ya mtoto inalindwa na kuchukua hatua
pale watoto wanaponyimwa haki zao.
Waziri wa elimu na mafunzo ya amali Zanzibar Lela Mohamed Mussa alisema, zaidi ya Bilioni 83 ilipatiwa wizara yake kupitia fedha za
UVIKO baada ya kuletwa Zanzibar, ambazo zilitumika kwa miradi mbali mbali ikiwemo ujenzi wa madarasa, skuli mpya, meza na viti.
Akitoa salamu za Mkoa mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Mattar Zahor Massoud alisema, kupitia sekta ya elimu Mkoa wake imefanywa kazi kubwa kwani kabla ya Mapinduzi ya mwaka 1964 kulikuwa na skuli nane lakini hadi sasa kuna jumla ya skuli 119.
Hata hivyo akitoa taarifa ya kitaalamu kuhusu mradi huo Katibu Mkuu wizara ya elimu na mafunzo ya amali Zanzibar Khamis Abdalla Said alisema, zaidi ya shilingi Bilioni 2 zimetumika kwa ujenzi wa Skuli hiyo ya gorofa mbili, yenye madarasa 21, ofisi ya Mwalimu mkuu, ofisi ya walimu, chumba cha kompyuta na vyoo 30.
MWISHO.