Thursday, January 16

Ushirikiano wa SMZ na Serikali ya Japan ni Wenye Manufaa Makubwa.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla akizungumza na Balozi wa Japan Nchini Tanzania Mhe. Yasushi Misawa, alipofika katika Ofisi za Makamu Vuga kwa mazungumzo hayo yaliyofanyika jana 10-1-2023.

 

Ushirikiano uliopo baina ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Japan ni wenye manufaa makubwa kwa wananchi wa pande zote mbili.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ameyasema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Japan nchini Tanzania Mhe. Misawa Yasushi aliefika kumsalimia Ofisini kwake Vuga Jijini Zanzibar.

Amesema suala la Serikali ya Japan kuunga mkono miradi mbali mbali ya maendeleo Zanzibar ni ushahidi tosha wa kukuwa kwa mashirikiano baina ya Nchi hizo na kuahidi kuendelea kuzidisha ushirikiano uliopo.

Amesema ujenzi wa Diko na soko la Samaki la Malindi lililozinduliwa rasmi na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambalo zaidi ya Asilimia Tisini ya fedha za ujenzi wa soko hilo zimetolewa na Taasisi ya Serikali ya Japan (JICA)ikiwa ni juhudi za kuunga mkono serikali ya mapinduzi ya Zanzibar katika kuinua uchumi wa buluu.

Mhe. hemed ameiomba serikali ya japan kuangalia namna bora ya kuendeleza ushirikiana uliopo katika sekta afya, elimu, uchumi wa buluu pamoja utamaduni.

Aidha Mhe. Hemed amemuomba Balozi huyo kutoa fursa mbali mbali za masomo za kuwajengea uwezo watumishi wa umma na viongozi wa serijkali katika kada za mipango, utawala, uongozi na biashara.

Nae Balozi wa Japan Nchini Tanzania Mhe. Misawa Yasushi amemuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuendeleza ushirikiano uliopo baina ya Nchi mbili hizo na kuahidi kuendelea kuisaidia Zanzibar hasa katika Sekta ya Elimu, afya, uchumi wa buluu na utamaduni.

Aidha katika kuimarisha utamaduni amemueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuwa Serikali ya Japan imeshaanzishia somo la Lugha ya Kiswahili katika Chuo kikuu cha Osaca ambapo mtaalamu wa somo hilo anatoka zanzibar hatua ambayo inaonesha upekee wa wataalamu wa lugha ya kiswahili fasaha ndani ya zanzibar na hii inaonesha kuwepo fursa za ajira kwa wataalamu hao katika Mataifa mbali mbali kupitia lugha ya kiswahili.