Thursday, February 27

FAMILIA ZENYE WATOTO WENYE ULEMAVU PEMBA WAKUMBUSHWA JAMBO

NA HAJI NASSOR, PEMBA.

WAZAZI na walezi kisiwani Pemba, wamekumbushwa kuwa, sio haki watoto wenye ulemavu kukoseshwa haki zao za msingi, kama elimu na kuchanganyika na wenzao, kwa sababu ya ulemavu walionao.

Hayo yameelezwa na Mratibu wa Idara ya watu wenye ulemavu kisiwani humo, Mashavu Juma Mabrouk, wakati akizungumza na wazazi, walezi na wanafunzi wa madrssa za Umi ya Vikunguni na ile ya Annajah ya Machomane Chake chake, kwenye ziara iliyoandaliwa na Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria Zanzibar.

Alisema, bado baadhi ya wazazi na walezi, wamekuwa wakijenga dhana kuwa, mtoto mwenye ulemavu anahiari ya kumpatia elimu, na asiyekuwa na ulemavu ndio mwenye haki kamili.

Alieleza kuwa, dhana hiyo isiwapitikie wazazi hata siku moja katika maisha yao, na badala yake wawe na haki sawa watoto wenye ulemavu na wengine, ili kutimiza matakwa ya kisheria.

Mratibu huyo alisema, suala la uwep wa changamoto kwenye sekta ya elimu kama vile uhaba wa vifaa visaidizi kwa watoto wenye ulemavu, isiwe sababu ya kuwafungia ndani na kuwakosesha haki hiyo.

Alieleza kuwa, sera ya elimu inataka watoto wote wenye umri wa kupata elimu, wawepo kwenye mfumo wa elimu, ili zinapotokea changamoto, ziwakuwate wakiwa madarasani.

‘’Ipo tabia ya baadhi ya wazazi, wakiona wamepata mtoto mwenye ulemavu, ameshapata kichaka cha kumtopeleka skuli au madrassa, akifikiria kuwa hawezi na atachekwa na wenzake, hilo sio sahihi,’’alieleza.

Hata hivyo amewataka wanafunzi waliomo kwenye mfumo wa elimu, kuendelea kuwashawishi wazazi na walezi wao, ikiwa kuna wenzao wenye ulemavu wamefungiwa ndani, nao waandamane nao kutafua elimu.

Katika hatua nyingine Mratibu huyo wa Idara ya watu wenye kisiwani Pemba Mashavu Juma Mabrouk, ameitaka jamii kuendelea kupanga mikakati madhubuti, ili kuwalinda na udhalilisha watoto wenye ulemavu.

‘’Watoto wote wanakabiliwa na hali mbaya ya kufanyiwa vitendo vya ukatili na udhalilishaji, ingawa sasa wabakaji wamekua wakikimbilia zaidi kwa watoto wenye ulemavu, wakidhani hawawezi kueleza chochote mahakamani,’’alieleza.

Hata hivyo alisema wazo la Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria Zanzibar, kuandaa ziara ya kuwapitia wanafunzi, ili kuzungumza nao juu ya namna ya kukabiliana na matendi hayo, ni nzuri.

 Kwa upande wake Mwakilishi wa Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria Zanzibar ofisi ya Pemba Mohamed Massoud Said, alisema, moja ya dalili ya mtu anaetaka kumdhalilisha mtoto, huanza kwa kumuonesha picha za ngono, kumnunulia zawadi, kumpa fedha, na kuendelea kwa maneno ya ushawishi juu ya udhalilishaji.

Hata hivyo, amewataka wanafunzi, waalimu, wazazi na walezi kuitumia Idara hiyo, kwa kutoa taarifa za matukio hayo, au uwepo wa watu wanaojaribu, kuzifanyia sulhu kesi za udhalilishaji.

Mkurugenzi wa Jumuiya wa wasaidizi wa sheria wilaya ya Chake chake Pemba ‘CHAPO’ Nassor Bilali Ali, amesema kama jamii haikushirikiana katika ulinzi wa watoto, kusitarajiwe matendo hayo kupungua.

Akizungumza kwenye ziara hiyo, Mratibu wa Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar ‘ZLSC’ tawi la Pemba Safia Saleh Sultan, aliwataka wanafunzi hao, kutomruhusu mtu yeyote, kuuchezea mwili wake.

‘’Sehemu zako za siri ni mali yako, usimuonesha mtu mwengine wala usikubali kuguswa kama hakuna sababu inayokubalika, maana huo ndio mwanzo, wa udhalilishaji unapoanzia,’’alieleza.

Hata hivyo amesema, lazima ulinzi kwa watu wenye ulemavu uimarishwe mara mbili, ili wawe huru na matendao ya udhalilishaji wa kijinsia.

Mwalimu mkuu wa Almadra-ssatul-Annajah Imani Ali Mohamed, alisema ziara hiyo kwao ni faraja, katika kuwakumbusha wanafunzi juu ya kujikinga na matendo hayo.

Kwa upande wake Msaidizi mwalimu mkuu wa Almadra-ssatul-Umi ya Vikunguni Zubeda Yussuf Mohamed, alisema bado wazazi hawajaona umuhimu, wa kushirikiana na waalimu, katika malezi ya watoto.

Ziara hiyo ya kutoa elimu ya kupambana na makosa ya udhalilishaji na ukatili wa kijinsia, ni muendelezo ya mikakati ya Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria, katika kuhakikisha kundi la wanawake na watoto, linaishi pasi na ukatili.
Ripoti ya Jeshi la Polisi Zanzibar, inaonesha, kwa mwaka 2021, kulikuwa na matendo 1,222 ya wanawake na watoto kudhalilishwa Unguja na Pemba.

Aidha ripoti nyingine ikaonesha kuwa, kulikuwa na matukio 610 ya aina hiyo, kwa kipindi cha miezi mitatu mitatu ya mwaka 2021 na 2022.

                     Mwisho