Monday, November 25

DC awataka walimu na wazazi kuwekeza katika suala la elimu kwa watoto wao ili baadae kuwapatia maendeleo bora

 

NA ABDI SULEIMAN.

MKUU wa Wilaya ya Chake Chake Abdalla Rashid Ali, amewataka wananchi wa Wawi Wilaya hiyo, kutambua maendeleo yao hayatoletwa na mtu mwengine, badala yake kuwekeza katika suala la elimu kwa watoto wao ili baadae kuwapatia maendeleo bora. 

Alisema Skuli ya Wawi ni moja kati ya skuli iliyotoa Viongozi wakubwa wa nchi hii, ambao wamefanya mambo mengi ikiwemo Makamu wa Rais, Mawaziri, Wabunge, Wawakilishi na hata madiwani ambao sasa wanasaidia wananchi wao.

Mkuu huyo aliyaeleza hayo alipokua akizungumza na wazazi, walimu na wanafunzi wa skuli ya Wawi Msingi, katika hafla ya kukabidhi vifaa vya ujenzi wa banda la Vymba vinne vya kusomea, ikiwa ni utkelezaji wa ahadi ya mwakilishi wa jimbo hilo kupitia fedha za mfuko wa jimbo.

Aidha Mkuu huyo aliwataka walimu, wazazi na wanafunzi kuzishukuru neema hiyo waliopatiwa, kwa kuhakikisha wanaongeza ufaulu wa wanafunzi mwaka huu.

“Ili kufikia huko lazima wazazi na walimu tushirikiane kwa pamoja, katika kuhakikisha watoto wetu tunawahimiza kusoma na wanafikia maelengo,”alisema.

Alimshukuru mwakilishi huyo kwa kuunga mkono juhudi za serikali kwa kuimarisha sekta ya elimu, kwani elimu ndio kila kitu kwa sasa kwa watoto, kupitia miradi iliyofunguliwa hivi karibuni Wizara ya Chake Chake imepata darasa mapya 125 na vyoo 113.

Akizungumzia Changamoto ya madawati na barabara, alisema kwa sasa serikali iko mbioni kuhakikisha barabara ya wawi hadi mgogoni inatengenezwa kupitia ujenzi wa barabara za ndani mwaka huu, pamoja na kuwaomba wadau kusaidia katika suala la vikalio kwa skuli.

Kwa upande wake Mwakilishi wajimbo la Wawi Bakar Hamad Bakar, alisema changamoto ya madarasa ndani ya jimbo la wawi ni kubwa, hivyo atahakikisha banda hilo la vyumba vinne vya kusomea wanafunzi lina simama moja kwa moja na wanafunzi wanasoma.

Alisema atahakikisha jengo hilo linajengwa kwa ubora wa hali ya juu, kwani bajeti ya jengo ni kupitia fedha za mfuko wajimbo hilo la wawi.

“Leo hapa tumekuja kukbidhi saruji mifuko 140, matufali 3000, Mchanga gari, kokoto, nondo na vifaa vyengine vyote vikiwa na thamani ya shilingi Milioni 12, nitakua mkali katika kusimamia fedha hizi,”alisema.

Aidha alisema suala la maendeleo ndani ya jimbo hilo halikuanza sasa, tayari skuli ya maandalizi kibokoni imekamilika na wanafunzi wanasoma, suala la maji kutatuliwa katika baadhi ya maeneo, ukarabati wa barabara kwa hatua ya kifusi, ukarabati viwanja vya mpira.

Naye mwakilishi wa Afisa Mdhamini Wizara ya elimu na Mafunzo ya Amali Pemba, afisa elimu Wilaya ya Chake Chake Sekondari Khamis Mohamed Yahya, alisema WEMA inathamini sana mchano wa Viongozi hasa katika suala la elimu, ili kuona watoto wanasoma katika mazingira mazuri.

Aidha aliwataka wanafunzi kusoma kwa bidii na kufaulu kwa kiwango kikubwa, ili kuunga mkono juhudi za mwakilishi huyo kwenye sekta ya elimu.

Diwani wa wadi ya wara Kassim Juma Khamis, alisema maendeleo jimbo la wawi yasingekuwepo kama kusingekuwepo madiwani makini wanaofika moja kwa moja kwa wananchi kusikiliza kero zao na kuziwasilisha kwa viongozi wa majimbo.

Mwenyekiti wajimbo la wawi Suleiman Mussa, alisema jimbo la wawi likosalama na wananchi wanashirikiana kikamilifu katika harakati za maendeleo.

Mapema akisoma risala ya skuli hiyo Mwalimu Naima Hamad Shaame, alisema ujenzi wa jengo hilo litakua mkombozi mkubwa kwao, kutokana na jengo lililokuwepo lilikuwa bovu na lina vyumba vitatu, litaweza kupunguza mrundikano wa wanafunzi madarasani.

Aidha alisema jengo hilo litaondosha mrundikano wa wanafunzi kuingia mikondo miwili, kutokana na mazingira iliyopo skuli hiyo ni vigumu watoto wadogo kuingia jioni.

MWISHO