Uchambuzi wa kina wa makala za takwimu za wanawake na uongozi umeanza rasmi leo ambapo jopo la wataalamu na wajuzi katika masuala ya habari watafanya kazi zao kwa muda wa siku tano hadi 10 (5-10) ili kuweza kupatikana mshindi wa tuzo za takwimu za wanawake na uongozi.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari mwenyekiti wa kamati ya maandalizi wa tuzo za umahiri wa takwimu za wanawake na uongozi Dk. Mzuri Issa ameyasema hayo mara tu baada ya kuzungumza na jopo la majaji walioteuliwa kupitisha kazi hizo kutoka vyombo vya habari mbali mbali; magazeti, redio, televisheni na mitandao ya kijamii.
Alisema mapitio ya majaji yanakuja baada ya kukamilisha kazi za ukusanyaji wa habari hizo tayari kuelekea kwenye siku ya utoaji zawadi inayotarajiwa kufanyika Februari 25, 2023.
Majaji hao watano watafanyakazi ya kupitia kazi na kuandika ripoti kamili inayoonesha mchakato pamoja na washindi wa kwanza hadi watatu kwa kila eneo.
Katika kuanza kuzipitia makala na vipindi vilivyowasilishwa kumefanyika matukio kadhaa ya kushajiisha waandishi wa habari kuandika na kuwasilisha makala zao ili kuweza kushiriki katika tuzo hizo.
“mchakato ulianzia tokea mwaka jana kwa kutoa elimu kwa waandishi wa habari pamoja na kuitangaza tuzo hiyo ili waandishi wengi zaidi waweze kushiriki”.
Mwenyekiti wa kamati ya tuzo hizo ambaye pia ni Mkurugenzi wa TAMWA Zanzibar Dkt. Mzuri Issa aliongeza kuwa makala zilizowasilishwa zilitakiwa kuwa tayari zimechapiswha au kurushwa hewani katika vyombo mbali mbali vya habari vikiwemo magazeti, runinga, redio na mitandao ya kijamii katika kipindi cha kuanzia Januari 1 hadi Disemba 31, 2022.
Vigezo zilivyotolewa awali ni pamoja na makala hizo kuzingatia mada husika lakini pia kuwepo kwa ubunifu wa mada, habari iliyokuwa na vyanzo tofauti vya habari pamoja na makala au vipindi hivyo kuzingatia masuala ya jinsia na makundi ya pembezoni.
“mada kuu ya makala na habari ni lazima iwe imelenga katika suala la takwimu na uongozi wa wanawake lakini pia kuzingatia ubunifu, lugha fasaha na kufuata maadili ya kazi za habari”.
Alisema vigezo hivyo vitatumika katika kuzichambua kwa kina makala zilizowasilishwa na waandishi wa habari na hatimae kupatikana kwa washindi kulingana na aina ya vyombo vya habari.
Alitoa wito mahasusi kwa majaji kuzingatia vigezo vya umahiri katika kuzifanyia uchambuzi makala zilizowasilishwa lakini pia kuzingatia usiri na uadilifu ili shughuli hiyo iweze kufanikiwa.
“hii ni shughuli ya taaluma hivyo vigezo vya kitaaluma havina budi kuzingatiwa kwa kina ili makala zitakazochaguliwa ziweze kuwa mfano wa kuigwa katika kuendeleza kada ya habari hapa nchini”, alifafanua.
Alitowa wito maalum kwa waandishi wa habari kuendelea kutumia kalamu zao katika kuandika makala ya takwimu za wanawake na uongozi ili kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa wanawake kuwemo katika nafasi mbali mbali za uongozi.
Kalamu za waandishi wa habari hazina budi kulenga katika kuinua wanawake ili waweze kushiriki katika uongozi ikiwa ni sehemu muhimu ya kuimarisha usawa na haki kwa wanawake na wanaume kama inavyoeleza katika katiba ya Zanzibar ya 1984.
“Nguvu ya vyombo vya habari haina budi kutumika katika kujenga jamii iliyo bora huku jinsia zote wanawake na wanaume wanapata fursa za kuwa viongozi katika nafasi za kitaaluma, kijamii, na kitaifa.”, aliongeza.
Tuzo hizo ambazo kauli mbiu yake ni “kalamu yangu, mchango wangu kwa wanawake”, ikiwa na lengo la kuhamasisha waandishi wa habari kutumia kalamu na vyombo vya habari katika kuelimisha umma umuhimu wa nafasi za wanawake katika uongozi.
Hii ni mara ya pili kufanyika kwa tuzo hizo za takwimu za wanawake na uongozi chini ya mradi wa kuwawezesha wanawake ambao unafanyika kwa pamoja na TAMWA Zanzibar , Jumuia ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA) pamoja na Jumuia inayojihusisha na Jumuia ya Mazingira,Usawa wa Kijinsia na Utetezi Pemba (PEGAO) kwa kushirikiana na Ubalozi wa Norway Nchini Tanzania.
Imetolewa na kitengo cha Habari
TAMWA-ZNZ