NA ABDI SULEIMAN.
MKUU wa Wilaya ya Wete Dr.Hamad Omar Bakar, amesema suala la amani ndio msingi wa maendeleo, kwani bila ya amani hakuna maendeleo yoyote yatakayofanyika au kupatikana.
Alisema Congo ni nchi yenye mali nyingi katika ukanda wa Afrika, kila siku vita na kupigana hakuna kitu kilichofanyika kutokana na amani kutoweka.
Mkuu huyo aliyaeleza hayo wakati akifungua mafunzo kwa Masheha, viongozi wa dini, watu mashuhuri, maafisa ustawi, viongozi wa Bodaboda, Tax na wakuu wa madiko, kupitia maradi wa AMANI MIPAKANI unaotekelezwa na CYD, kwa ufadhili wa Ubalozi wa Canada Tanzania kutipia Mfuko wa Maendeleo ya Kijamii (CFLI), huku katika ukumbi wa baraza la mji Wete.
Alifahamisha kwamba kuna viashiria vingi kwenye mipaka vinavyotaka kupelekea au kuvuruga amani, hivyo tunapaswa kuwa makini na kuweka mbele uzalendo wa nchi ili kuepuka kuishi kwa hofu.
“Lazima tusimamie amani hii tulionayo vizuri kwa kutoa taarifa kwa wahusika, serikali itakuja kufuatilia kila mmoja kuchukua hatua kwa nafasi yake katika kusimamia suala la amani,”alisema..
“Hakuna mbadala wa amani iwapo itachafuka, kila mtu kuwa mlinzi mkubwa wa amani ya nchi, boda boda, madereva tax, wakuu wa madiko, sote ni walinzi wa nchi katika maeneo yetu,”alisema.
Mkurugenzi mtendaji wa CYD Hashim Pondeza, alisema lengo la mradi ni kuhakikisha jamii nzima inaelewa umuhimu wa amani na kila mtu anachangia suala la ulinzi wa amani, kwani wapo wageni wanakuja wakiwa na nia nzuri na wengine hawana.
Alisema dunia nzima wananchi ndio wanaojuwa mwanzo mambo yanayotokea, vizuri sasa kila mtu kuwa tayari katika kutoa taarifa pale yanapotokea matukio.
Naye katibu tawala Wilaya ya Wete Mkufu Faki Ali, alisema Wilaya ya Wete kila inapopatiwa mafunzo juu ya masuala ya amani mipakani inabadilika, kwani tayari taarifa zimekuwa zikitolewa huku akitolea mfano Kisiwa cha Fundo.
Naye katibu Tawala Wilaya ya Ndogo ya Kojani Makame Khamis Makame, aliwashuhuru CYD kwa kuja na mradi wa Amani Mipakani ambao umewasaidia wananchi wa Kisiwa cha Pemba kutokana na kuwa na bandari bubu nyingi.
“Sisi hapa tunafuga watu mpaka wanaowa na mwisho wa siku ndio tunawajuwa kama hawakua wenzetu, tunaushahidi tosha wa matukio yaliyotokea,”alisema.
Kwa upande wake mkufunzi kutoka Jeshi la Polisi Insekta Hashim Ali Hashim, alisema pemba ni kisiwa na kimezungukwa na bahari huko kwenye mipaka ya bahari kuna mambo mengi yanafanyika, kwani kuna mipaka rasmi na isiyo rasmi na watu wanaingia.
Alisema Wilaya ya Wete inabandari bubu zisizopungua 80, lazima tuweke ulinzi kwa kulinda usalama wetu wenyewe kupitia sisi wananchi wa maeneo hayo.
MWISHO.