Wednesday, October 30

SMZ na SMT Kuimarisha Huduma za Afya ili Kufikia Hatua ya Kuazisha Utalii wa Tiba

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amezipongeza taasisi binafsi kwa juhudi zao za kuiungamkono Serikali katika kuimarisha huduma za jamii nchini.

Dk. Mwinyi alitoa pongezi hizo, Manispaa ya Kinondoni, Mkoa wa Dar es Salaam, alipofungua kituo cha kisasa cha afya cha Kairuki Green IVF cha hospitali ya Kairuki.

Alisema dhamira za Serikali za Mapinduzi ya Zanzibar na ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ni kuimarisha huduma za afya ili kufikia hatua ya kuanzaisha Utalii wa tiba kwa watu kutoka mataifa mengine kuja kufuata huduma za tiba, Tanzania.

Alieleza uwekezaji mkubwa unaofanywa na taasisi binafsi na Serikali wa kuimarisha huduma za afya nchini, dhamira hiyo inaanza kuonekana kwa sekta zote mbili za umma na binafsi.

Alisema hospitali ya Kairuki imekuwa tegemeo kwa Tanzania kutokana na huduma bora za afya wanazozitoa kwa wananchi zikiwemo huduma za matibabu bingwa pamoja na vipimo vya kisasa vyenye teknolojia ya hali ya juu.

Alieleza hospitali hiyo imekuwa ya kwanza Tanzania kutoa huduma kadhaa ambazo awali hazikupatikana kwenye hospitali nyengine zikiwemo vipimo vya “CT Scanner” vilipoanza kutolewa na hospitali hiyo tokea mwaka 1992, huduma za upasuaji kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya “Laparascopy” ambayo ilianza kutolewa hospitalini hapo mwaka 1996 pamoja na uanzishwaji wa Chuo Kikuu cha kwanza nchini cha binafsi cha Tiba

Alisema Chuo kimetoa mchango mkubwa kwa taifa katika kuandaa wataalamu wa fani mbali mbali za afya ambao sasa wanatumikia nchini na mataifa mbalimbali ya Afrika na kwengineko duniani.

“Leo tena tunashuhudia ufunguzi wa kituo cha kisasa kabisa cha Kairuki Green IVF ambacho ni mafanikio makubwa na mapinduzi katika kuboresha utoaji wa huduma za afya hapa Tanzania, Nakupongezeni sana” Dk. Mwinyi aliipongeza taasisi hiyo.

Aidha, aliwahakikishia taasisi hiyo kwamba Serikali zote mbili zitakuza ushirikiano nao kwa lengo la kuimarisha huduma za afya kwa Watanzania na kuyafikia malengo ya Kitaifa na Kimataifa kuboresha sekta ya afya nchini.

Dk. Mwinyi alisema huduma za afya zinazotolewa na hospitali ya Kairuki zinakwenda sambamba na Programu za Wizara ya Afya zikiwemo afya ya uzazi na watoto, mapambano dhidi ya UKIMWI, Kifua kikuu, Malaria na UVIKO – 19.

Alieleza huduma hizo ni mfano bora wa ubia baina ya Serikali na Sekta binafsi. Aidha, alitoa wito kwa taasisi binafsi kuendeleza ushirikiano wao na Serikali katika kuwatumikia Watanzania.

Hata hivyo Dk. Mwinyi aliitaka Wizara ya Afya Zanzibar kuona haja ya kuimarisha ushirikiano baina yao na taasisi hiyo kwa kuzingatia uzoefu mkubwa walionao.

 Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mtendaji Mkuu wa kituo cha Green IVF, Dk. Clementina Kairuki alisema, kituo kimeanzishwa kwa lengo la kutoa huduma ya kupandikiza mimba kwa wanawake na wanandoa walioshindwa kupata ujauzito kwa njia ya kawaida.

Alisema uanzishwaji wa huduma hizo ni mwendelezo wa maono ya Muasisi wa taasisis hiyo ya afya na elimu ya Kairuki, hayati Prof. Hubert Kairuki aliefariki miaka 24 iliyopita ambaye alitamani kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya afya Tanzania.

Kituo cha afya cha Kairuki Green IVF, kinatoa huduma ya kupandikiza mimba kwa wanaoshindwa kupata ujauzito kwa njia ya kawaida, kinamilikiwa na taasisi ya afya na elimu ya Kairuki “(Kairuki Health and Education Network – KHEN), kinasimamiwa na hospitali ya Kairuki, Kituo kipo Bunju ‘A’ Mianzini, Wilaya ya Kinondoni, Mkoa wa Dar es Salaam.

IDARA YA MAWASILIANO – IKULU, ZANZIBAR