NA SAID ABRAHMAN, PEMBA
WATU wenye Ulemavu Kisiwani Pemba wameiomba Serikali kuwaangalia Kwa jicho la huruma katika suala zima la ajira.
Wamesema kuwa watu wenye Ulemavu wamekuwa hawaangaliwi Wala kupewa kipaumbele wakati wa kuomba ajira.
Hayo waliyaeleza wakati wa mkutano wa utoaji wa elimu ya haki za binaadam Kwa watu wenye Ulemavu uliyoandaliwa na Idara ya Msaada wa Kisheria huko Gombani Chake Chake Pemba.
Fatma Abdalla Ali (JUWAUZA) alisema kuwa watu wengi wenye Ulemavu wamekuwa na elimu yao lakini kutokana na Hali zao wamekuwa wakinyimwa nafasi za kazi (ajira).
Aidha Fatma alifahamisha kuwa jamii imeona kuwa watu wa kundi Hilo hawana uwezo wa kufanya kazi maofisini jambo ambalo sio sahihi.
“Kwa mfano Mimi binafsi niliweza kujitolea katika shirika la nyumba Kwa muda wa miaka 6 na nilikuwa kama sekretari msaidizi, lakini lakushangaza niliondolewa kama taka tu na hadi Leo sikupata ufumbuzi wowote,” alieleza Fatma.
Nae Hidaya Mjaka Ali alieleza kuwa tatizo kubwa ambalo linawakabili Wana jamii hiyo ni ajira jambo ambalo linawarudisha nyuma kimaisha.
Hata hivyo Hidaya aliiomba Serikali kuandaa mpango mzuri Kwa watu wenye Ulemavu wakati wanapotoa ajira ili na wao waweze kupata Haki kama raia wa Nchi hii.
“Serikali tunaiomba kutoa fomu Maalum Kwa watu wenye Ulemavu wakati wanapotangaza nafasi za ajira Kwa wananchi wake,” alisema Hidaya.
Mapema akifungua mafunzo hayo, Mkugenzi wa Idara ya Msaada wa Kisheria Zanzibar Hanifa Ramadhan Said aliwataka washiriki wa mafunzo hayo kuitumia vyema fursa waliyopata kwani Kuna wengi ambao walitamani kupata fursa hiyo lakini haikuwa bahati kwao.
Aidha Mkurugenzi huyo aliwashauri washiriki hao elimu waliyoipata kuitoa Kwa wenzao ambao hawakubahatika Kwa njia moja ama nyengine.
“Mafunzo ambayo mtayapata hapa ni wajibu wenu kuyatumia vizuri pamoja na kuwasambazia wengine ambao hawakubahatika kuwa nasi,” alisema Mkurugenzi Hanifa.
Sambamba na hayo Mkurugenzi huyo alifahamisha kuwa kazi za Idara ni kutoa elimu Kwa makundi mbali mbali, hivyo huo sio mwanzo kila Hali itakaporuhusu watahakikisha wanaendeleza kutoa mafunzo.
“Ombi langu kwenu,mukiona tumekaa kimya sana watumieni watu wa Msaada wa Kisheria ili wawe kutukumbushia na sisi hasa pale panapotokezea mabadiliko ya sheria,” alisema Hanifa.
Nae Juma Kombo Haji aliwataka jumuia ya msaada wa kisheria Kisiwani Pemba kuwa karibu na jumuia yao Ili kuweza kuwapatia elimu ya sheria.
“Ombi letu Kwa Wana sheria hasa hii jumuia ya msaada wa kisheria hapa Pemba wasituache mkono waendelee kutupatia elimu hii ya sheria kwani wengi wetu hatujui lolote,”alisema Juma.
Katika mafunzo hayo jumla ya nada mbili zilizungumzwa ikiwa ni pamoja “Haki za binaadamu Kwa Katiba” na Namna ya upatikanaji wa Msaada wa Kisheria Kwa watu wenye Ulemavu “
MWISHO.