NA ABDI SULEIMAN, KILOMBERO.
KUWEPO kwa njia za chini za mapito ya wanyama katika barabara ya Kilombero hadi ifakara na reli ya Tazara kilombero, kutaweza kupunguza vifo vya wanyamapori katika njia hizo.
Hayo yameelezwa na Meneja wa Shoroba, kutoka Mpango wa kuhifadhi Tembo kusini mwa Tanzania (STEP) Joseph Mwalugelo, wakati akizungumza na waandishi wa habari wa uhifadhi wa wanyamapori na utalii kutoka JET, kupitia mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili, katika ziara ya siku nne ya kutembelea shoroba ya Tembo ya Kilombero hifadhi ya milima ya Udzungwa na Hifadhi ya Taifa ya Nyerere Wilaya ya Kilombero halmashauri ya mji wa Ifakara.
Alisema kuwepo kwa njia hizo kutasaidia kupunguza vifo vya wanyamapori hususani Tembo, ambao wamekuwa wakipoteza maisha kila uchao kwa kugongwa na Treni au gari barabarani.
Alisema barabara ya kilombero hadi ifakara imekua kubwa, wanayama hutoka hifadhi moja kwenda nyengine na kukatiza katika barabara au njia ya treni, wakati wanapopita kwenda kutafuta malisho au wanarudi hifadhini.
“sisi kama STEP tumekua tukishirikiana na viongozi wa vijiji, kata na serikali ya Wilaya ili kuona wanyama wanapata nafuu katika kupita kwao ikiwemo kujengwa kwa uzio utakapopeleke kupita kwenye ushoroba wao,”alisema.
Akizungumzia idadi ya wanyama waliopoteza maisha, alisema Tembo sita (6) wamepoteza maisha kuanzia mwaka 2021 hadi 2022, huku watu saba (7) nao wakipoteza maisha kutoka katika kata tatu ambazo ni Mangula, Mangula B na Mkula kuanzia 2018 hadi 2022.
“Kwa upande wa barabara tayari njia ipo ya kupita wanyama, huku juhudi zikiendelea kufanywa, ili kupatikana kwa njia ya kupita kwa wanyama upande wa treni, ambapo kwa sasa iliyopo inahitaji kuongezwa ukubwa wa mita nne,”alisema.
Naye Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi kutoka hifadhi ya Taifa ya Udzungwa Abel Peter, alisema hifadhi ya Udzungwa ni moja ya hifadhi yenye viumbe hai adimu duniani, ikiwemo miti, wanyama na baadhi ya bionuai.
Alisema kumekuwa na matukio mengi ya Tembo kugongwa na treni, hivyo kuwepo kwa njia za chini za kupitia wanyama kutasaidia kupunguza au kuondosha kabisa vifo vya Tembo kwa kugongwa na treni.
“Tembo wanne (4) waligongwa na Treni ya Tazara kwa pamoja wala haikusimama, tayari juhudi za kunusuru vifo vya tembo zimeanza kuchukuliwa ikiwemo kujengwa kwa njia hizo,”alisema.
Muhifadhi huyo alifahamisha kwamba, Kenya tayari wameshajenga njia hizo na Tembo na wanyama wengine wanapita katika eneo hilo wameshazowea, na Udzungwa pia watazowea kupita baada ya kukamilika kila kitu.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Chama Cha Waandishi wa habari za Mazingira Tanzania (JET) John Chikomo, alisema lengo la ziara hiyo kwa waandishi wa habari ni kujua faida mbali mbali zinazotokana na uhifadhi zinazopatikana katika hifadhi ya Udzungwa.
Alisema wananchi wataweza kupata uwelewa juu ya umuhimu wa koridoo inayopatikana katika eneo la hifadhi, na kutokuwaona tembo kuwa ni aduwi wao mkubwa.
Kwa upande wake mmoja ya mwananchi wa kijiji cha Kanyanja Isaya Fabian Utambule, alisema Tembo wanaumuhimu mkubwa kwa Serikali na Taifa kwa ujumla, kwani wamekuwa wakiingizia nchi fedha za kigeni kupitia wageni mbali mbali wanaotembelea hifadhi mbali mbali.
MWISHO