NA ABDI SULEIMAN.
MKUU wa Mkoa wa Kusini Pemba Mattar Zahor Masoud, ameitaka Wizara ya Kilimo kuendelea kutoa elimu kwa wakulima wa karafuu, kwa kuwapatia elimu bora ya upandaji wa miche ya mikarafuu.
Alisema wakulima wengi wanapatiwa miche hiyo, lakini wanashindwa kuwa na elimu ya upandaji wa miche kisasa zaidi na kuweza kupata mavuno mazuri baadae.
Mkuu huyo aliyaeleza hayo kwa nyakati Tafuti, wakati alipokua akizungumza na wakulima na wadau wa karafuu wa Wilaya ya Mkoani na Chake Chake.
Alisema Zao la Karafuu sio zao la kibiashara tu kwa Zanzibar, bali pia ni zao linaloitangaza Zanzibar kiutamaduni na linapaswa kuendelezwa kwa vizazi vinavyokuja.
Aidha alisema wakulima wanapaswa kutambuwa zao hilo ni chakula muhimu kwa mwanadamu, hivyo wanapaswa kulithamini na kulijali na kulianika katika mazingira mazuri na safi muda wote.
“Wenzetu duniani wanalitumia zao hii kama chakula, kwa kutumika katika vyakula mbali mbali, linatengenezewa madawa mbali mbali ya binaadamu, lazima tuliweka katika mazingira mazuri”alisema.
Hata hivyo aliwataka wakulima kutambua kuwa zao hilo, linaipatia serikali fedha nyingi za kigeni ambazo zinasaidia katika kuwahudumia wananchi.
Kwa upande wake mkuu wa Wilaya ya Chake Chake Abdalla Rashid Ali, aliwashukuru wakulima wa zao la karafuu kwa kumaliza msimu bila ya kuwepo kwa magendo ya za hilo mwaka msimu uliopita na zao hilo kuliuza katika shirika la ZSTC pekee.
“Wakulima msimu uliopita tulienda vizuri kwa asilimia kubwa, vizuri na msimu unaofuata tukaenda kama msimu uliopita bila ya kutokezea kwa matataizo yoyote katika suala zima la karafuu,”alisema.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa ZSTC Zanzibar Bakar Haji, aliwataka wakulima wa zao hilo kuwa wazazi kutoa maeni na changamoto zao zilizojitokeza katika msimu uliopita ili msimu unaokuja changamoto hizo zitokee tena.
Kaimu kamanda wa ZAECA Mkoa wa Kusini Pemba Mustafa Hassan Issa, aliwataka wakulima wa karafuu Mkoa huo kutokujihusisha na magendo ya karafuu, kufanya hivyo ni kuhujumu uchumi wa nchi.
Aidha aliwasihi wakulima hao kuachana na kufanya udanganyifu kwa kuzichanganya karafuu na vitu vyengine, kwani kufanya hivyo ni kuondoshea hadhi na tahamani zao hilo na kupelekea kuitia doa taifa.
Akichangia katika mkutano huo Mkulima wa Zao hilo, Aboubakar Mohamed Ali, aliitaka Wizara ya kilimo kuhakikisha miche ya mikarafuu wanawapatia wakulima wenyewe moja kwa moja na sio kuwapatia masheha.
Aidha aliishauri ZSTC kubadilika katika msimu mpya wa karafuu, kwa kuachana na utumiaji wa Mashine za kupimia za zamani na badala yake kwenda kisasa kwa kua na mezani na kieletroniki.
Mkulima Mohamed Nassor Kahlafan, alisema ZSTC inapaswa kuwa makini wakati wa utoaji wamiche ya mikarafuu kwani wapo watu wanapatia miche hiyo na wala sio wakulima na baada kuiweka majumbani bila ya kuitumia.
MWISHO