Tuesday, January 7

‘Donda Ndugu’ linalotibika!

 

Ni  kweli kuna  vidonda vinaweza kuacha kovu na vyengine kovu kufutika  kabisa madonda yako mengi, Baba yangu  aliwahi  kusema ‘donda la  tumbili , kila achapiapo  mti hujitonesha na kamwe haliwezi kupoa  alikua akinidhihaki tu na donda langu lisilopoa wakati huo  litapoa wapi na kila siku kufukuzana na kambare mtoni ,mechi za mpira wa chakacha  na kutoneshwa na wenzangu kwa makusudi chuoni !Utani wa kitoto

Kuna hili linaloitwa  ‘donda  ndugu’ , hata sijui udugu umetokea wapi pengine madhara yake ya   muda mrefu kwenye mwili huwafanya  ndugu kupokezana kwa kuuguza ndio maana likaitwa  ‘donda la ndugu’ linahitaji  ukoo mzima kulishughulikia huyu kaleta pamba,mwengine kaleta majani ya mpera , mjomba katumwa kivumbashi na shangazi   anatafuta   majani ya mnanaa ili  mradi  jeraha lipoe  ndio donda ndugu donda la ukoo.

Hili donda ndugu lazima liache kovu tena  lisilofutika na  mgonjwa kila siku anapoliangalia kovu , hataacha kusimulia machungu ya donda, mauvivu , pengine kero la uvundo  ama  hata jinsi ndugu zake walivyoteseka kuliuguza  donda la ukoo .Simulizi ya leo haitasimulia yaliyopita .Inatosha !.

Na sisi Zanzibar  tuna donda letu  la ukoo donda ndugu donda la msimu kama vile mchoo na masika   donda hunuka na kukera wakati wa kuuguzwa donda letu  ni la  hasara na faida kwa ukoo. wakati wa kuuguza donda, ndugu hugombana , Kondo ya asubuhi na jioni maskini donda hili limesababisha hata pingu za maisha kuvufunguka ndugu kubaguana, kusemana na  kutukanana ndugu kutafunana   wazima wazima ukoo hukoseshana fursa  na vibarua  lakini donda hili pia lina faida,  wale waliouguza  hufaidika na walionuna wakati wa kuuguza  imekula kwao, mgonjwa anapobesa wauguzaji hugonganisha gilasi wakapeana zawadi  na vyeo tena vyeo bila ya kuangalia ni nani muuguzaji na ni nani mtoneshaji makusudi wa donda ! Kula baba mkubwa na baba mdogo , wauguzaji wenza ,wauguzaji wasaidizi !

Kila baada ya  miaka  mitano kovu hili  la donda hugeuka  tena  donda ndugu  tunatonesha donda ,tunauguza  donda na tunalinda kovu bichi , wengine hudiriki kulitia pilipili donda , Hammadi ….. mgonjwa huwa tafrani

Mwenye kaya yake anasema  ,tusifukue makaburi  kwa yote yaliyotekea wakati wa kuuguza mgonjwa namuunga mkono lakini  tunapozika kaburi tuweke alama tupande mti wa kudumu tujenge vikuta  ama chambilecho zamani tunaandika jina la mfu marehemu kafa kwa kuuguzwa donda ,mauti yamemchukua akiwa kwenye foleni  ya  dawa aidai haki yake ,haki ya kuuguza  donda ndugu lakini daktari baada ya kumchoma sindano ama kumpa dawa ya kupunguza maumivu  tunaambiwa alikosea  akamchoma sindano ya sumu na kumnywesha   sumu ya panya.

Bahati mbaya donda letu hili ndugu huambukiza tena kama korona  wakati wa jereha  wapo wanaopona wapo wanaotangulia mbele ya haki Alhamdulilah tumeanza kusahau, wa  vizuka walionyolewa para nywele  zimeanza kuota huku familia zikitunza mayatima, wako wanaoguza majeraha , vitandani , hospitalini , wako  pia watakaobakia vilema kwa maisha yao  yote , Mungu  awasaidie  na awape  subra  , wako pia wanafunzi wa vile vyuo tunavyosema vinafunza amali njema kwa makosa yaleyale   ya mtihani  wa kuuguza donda ndugu , maskini  wakati huu tukishikana mikono kwa kufurahia nafuu ya mgonjwa  wenzetu hawa  wanaacha familia zao  wakishuhudia fashifashi na nduru za mwaka mpya wakifunzwa amali na tabia njema  na utii wa sheria bila shuruti , Mungu awasalimu salama ,wamalize warudi wakiwa raia wema na simulizi kama hizi miaka ijayo iwe ni hadithi za babu  zimwi

Tuwasamehe  wauguzaji na watoneshaji  donda ?Waliotia pilipili kwa makusudi?Waliomnywesha  mgonjwa sumu  ya panya   na hata waliotonesha kwa makusudi tuwasamehe ?Tuvumiliane,tusameheane , tuombane msamaha  kwani yaliyopita si  ndweli tugange yajayo, hayo yote yanawezekana

Leo tunataka kufuta  kovu la donda ndugu  kama tulivyofuta hapo  zamani  baada ya kikao cha  makubaliano cha ukoo, tunakumbushana  sisi ni ndugu wa ukoo mmoja, Shangazi kwa mjomba hatupaswi kugombania fito kwani tunajenga nyuma  moja ,nyumba hii si nyumba ya uyoga kama ni ya nguzo moja  ni nyumba ya watu wawili ,wauguzaji wakubwa  na wauguzaji  wadogo  wapo wanaojiona wana  hati miliki ya kiwanja ,  wapo waliojenga msingi , wa kunyanyua viambaza na wa kuezeka paaa  na wa kufanya matengenezo , nyumba hii ya ukoo ina mchwa pia wanaotafuna fito , makuti na makabati  ya nguo , panya  tunawafuga wenyewe  kwani paka alikua marafiki na panya wamekula waya za umeme, wamechimba mashimo na usufi na hata  kodoro tunalolalia, sasa tunalala  sakafuni

Wakati tunauguza donda kwa  mbali kovu imeanza kuota jeraha limepungua machungu  kwa mashirikiano ya mwenye nia ya dhati ya  kufuta kovu tunahubiri umoja ,amani ,umoja mshikamano ndugu waliogombana kwa  kuuguza mgonjwa leo wanashikana mikono,kula pamoja ,safarini pamoja .Kilio kinaweza kuwa furaha eti , mkisikizana na kusameheana , hatufukui kaburi ya kuuliza nani aliweka pilipili kwenye donda ,nani alimmywesha mgonjwa sumu  ya panya nani alitafuta majani ya kuponja mgonjwa, huu  ni uungwana   kwani muungwana nguo zikivuka huchutama, na kweli nguo zilikaribia kuvuka wauguzaji tukabakia watupu tukakaa utupu mbele ya wakwe na watoto ,aibu ya mkusanyiko wa kuuguza mgonjwa

Wakati  tunaponya jeraha hili  basi nyumba  tuijenge pamoja,  panya   wakamatwe , mchwa watiwe dawa tushirikiane kuinyanyua upya  nyumba hii  kwani ni vigumu kusema tumefika hatua gani ya ujenzi ukarabati ufanywe tuepuke yale ya jumba la maajabu  kuporomoka siku ya chrismasi . Makaburi yasifukuliwe lakini si vibaya kulijua kaburi la babu  tukalipalilia upya tukakata magumu tukaandika jina ili vilembwe vijavyo wamjue babu yao alikufa lini pengine hata bila ya kuwaambia kama alifariki  kwa maumivu ya donda linalotibika

Msimu wa kuuguza mgonjwa hauko mbali kiangazi hakiwezi kubakia kwa miaka minne ijayo inawezekana  kuzuia kila dalili  ya donda  ndugu jipya,  mapanga yazikwe  na  wale washika mapanga washikishwe adabu wajue vya kuyatumia, nwenye chokochoko za kusababisha ugomvi wakae pembeni waachwe wenye nia  njema,  wasiopenda umoja wa ukoo huu si muda  wao huu ni wakati  wa wenye huruma  wanaojua kuuguza mgonjwa,  wauguzaji wazalendo si wa kumtii baba tu kwa sababu ana nia ya dhati ya kuunganisha familia bali ni wa dhati kutoka mtima wa moyo .

Namalizia  simulizi hii ya donda ndugu kwa kisa cha mjomba alieuguza miezi minne  akiwa hospitali tatizo la mgonjwa lilikua  ni kutokua   na uwezo  wa kula basi muuguzaji akawa na kazi ya kula kila anacholetewa mgonjwa  .Mjomba akaanza kunenepa na baada ya miezi mitano puresha ikawa juu na yeye  akalazwa hospitali ikabidi auguzwe, mjomba alishindwa kula hata alicholetewa hospitali,  basi tuuguze kwa busara , hekima na huruma tukitambua kwamba akili ya mgonjwa ipo kwa muuguzaji.

Sisi tunaondika  habari aidha kwa umakini ama weledi  wa simulizi ya donda ndugu , tunaifahamu thamani ya nguvu ya ukoo na familia yenye upendo tunaweza kuishi kwa umoja , upendo na mshikamano simulizi hizi zinaungwa mkono na wenzetu wa Internews Tanzania ,ambao  sote tunaamini   amani ni  zao  la haki  na kila mmoja wetu anao muarubaini  wa kuponya gonjwa letu .

Tupendane  hili   donda  linatibika !