Monday, November 25

Asma Mwinyi Foundation kwa kushirikiana na PBZ wasaidia  Hospitali ya Micheweni.

NA HANIFA SALIM, PEMBA.

MKUU wa Wilaya ya Micheweni Mgeni Khatib Yahya ameziomba taasisi na jumuiya mbali mbali kujitokeza kuwasaidia katika Hospitali ya wilaya hiyo, pamoja na maeneo mengine ambayo yanatoa huduma muhimu kwa jamii.
Aliyasema hayo katika hafla ya kukabidhi vifaa vya mama na mtoto vinavyotumika wakati wa kujifungua vilivyotolewa na taasisi ya Asma Mwinyi Foundation kwa kushirikiana na benki ya PBZ, huko katika ukumbi wa Hospitali ya Wilaya ya Micheweni Kisiwani Pemba.

“Nazishukuru hizi taasisi ambazo zinaendelea kutusaidia ikiwemo Asma Mwinyi Foundation, vile vile benki ya watu wa Zanzibar PBZ na taasisi nyengine ambazo zinakuja kutusaidia ndani ya Wilaya yetu ya Micheweni”, alisema.
Alieleza kuwa, amefurahishwa kuona jamii inaendelea kuwasaidia ndani ya Wilaya yao ya Micheweni, kwani alisema wananchi watakapofika katika hospitali huduma zinakua zinapatikana kwa wepesi na bila usumbufu wowote kujitokeza.
Hata hivyo alisema, taasisi hizo kuwapatia vifaa njia moja ya kuisaidia serikali kwani ni jukumu lake kutoa huduma kwa wananchi, lakini kupitia taasisi hiyo imeweza kuongeza nguvu kwa kutoa vifaa hivyo muhimu.
Mjumbe kutoka taasisi ya Asma Mwinyi Foundation Abdalla Omar alisema, taasisi hiyo imejikita kuwasaidia akina mama, watoto wenye mahitaji maalumu pamoja na watu wenye mazingira magumu kwa kushirikiana na benki ya PBZ.
“Asma Mwinyi hii sio mara ya kwanza kufika Micheweni tulishawafikia wananchi wa Maziwang’ombe, tumeshatoa msaada kama huu Makunduchi Unguja, Mwananyamala Dar es salam, ni matumaini yetu kwamba msaada huu utawafikia walengwa”, alisema.
Nae, Meneja wa Benki ya watu wa Zanzibar PBZ tawi la Chake chake Mohamed Sheha Othman alisema, vifaa hivyo vitasaidia kuokoa maisha ya mama na mtoto, kwa kulinda maisha yao na watoto wao ambapo lengo lake ni kupunguza vifo.
“Pamoja na kuwa hospitali zipo nyingi lakini tumeichagua Micheweni na kwetu ni faraja kubwa kuchangia vifaa hivi ambavyo uhai wa mama wajawazito na watoto watakaozaliwa”, alisema.
Akitoa neno la shukurani Daktari dhamana wa Hospitali ya Wilaya ya Micheweni Mbwana Shoka Hamad alisema, taasisi hiyo imelenga ambapo serikali ya awamu ya nane inayoongozwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Hussein Ali Mwinyi inapambania kuhakikisha vifo vya mama na mtoto vinapungua.
“Waliochangia hivi vifaa tunawashukuru sana wamefanya jambo kubwa kwetu ambalo ni kwa muda sahihi unaohitajika, tunawaomba wafadhili wengine ambao bado hawajafikia Micheweni wajitolee kutusaidia tunawakaribisha sana”, alisema.
Kwa upande wake Muuguzi Mkuu wa Hospitali hiyo Rehema Hamad Salim alisema, vifaa hivyo vitarahisisha utoaji wa huduma kwani baadahi ya wakati katika hospitali yao hukabiliwa na changamoto ya upungufu wa vitendea kazi.
                           MWISHO.