SAID ABRAHMAN—PEMBA.
NAIBU Waziri wa fedha ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa Jimbo la Kojani Hamad Hassan Chande amekabidhi gari yenye thamani ya Tsh milioni 160 kwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Akikabidhi gari hilo huko katika kituo cha Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba, alisema kuwa hiyo ni ahadi yake kwa jeshi hilo ambayo aliiweka.
Chande alilitaka jeshi la Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba kulitunza gari hilo kwa namna yeyote ile ili liweze kuwasaidia katika harakati zao za kila siku.
Alifahamisha kuwa hiyo ni mwanzo tu kwani baada ya kumalizika kwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anatarajia kutoa gari 3 aina ya Noha kwa jeshi la Polisi, KMKM Kojani pamoja na Chuo cha Mafunzo Kangagani.
“Ninamshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk, Samia Suluhu Hassan kwa kutoa zawadi hii ya gari, kwani nilipoenda kumlalamikia kwa suala hili alinipa moyo na leo hii gari imepatikana,” alisema Mbunge Chande .
Alieleza mbali ya gari hilo lakini pia aliahidi kuwa baada ya kumalizika kwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania atakuja tena kukabidhi gari nyengine 3 kwa Jeshi la Polisi,KMKM Kojani pamoja na Chuo cha Mafunzo Kangagani.
Mapema akizinduwa vikundi vya ulinzi shirikishi ambavyo vimeundwa na waendesha boda boda wa jimbo hilo, aliwataka waendesha bodaboda hao kuifanya kazi hiyo kuwa ni kitega Uchumi kwao kwani ndiko wanapopata riziki zao.
“Lakini pia tunatakiwa tutambue kuwa sisi tunategemewa na familia zetu, hivyo tujitahidini sana kadri ya uwezo wetu kuepusha ajali zisizo za lazima,” alisema Chande.
Aidha Mbunge huyo aliwasisitiza waendesha bodaboda hao kukata Bima kwa lengo la kuwa salama muda wote, ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza wa kisheria baina yao na Vyombo husika.
“Katika ajali nyingi ambazo huwa zinatokea husababishwa na waendesha boda boda ambapo wengi wao katika ajali hizo husafirishwa kupelekwa Tanzania bara au hata nje ya Nchi, hivyo ni vyema tuwe na tahadhari kubwa sana,”alieleza Mbunge Chande.
Nae Katibu Tawala Mkoa wa Kaskazini Pemba Ali Khatib Bakar alimpongeza Mbunge huyo kwa juhudi zake kubwa anazozifanya katika Jimbo lake kwa ajili ya kuwahudumia wapiga kura wake kimaendeleo.
Ali alimuelezea Mbunge huyo kuwa amekuwa akijijitahidi katika kuwafikishia wananchi wa Jimbo lake maendeleo ya aina tafauti tafauti bila ya ubaguzi wa aina yoyote.
“Kwa kweli hapa tumepata Kiongozi ambae anajali sana wananchi wake, hivyo tuendelee kushirikiana nae ili yale ambayo ameyakusudia yaweze kutimia” , alisema Katibu Ali.
Nae Mkuu wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba ACP Juma Sadi Khamis alieleza kuwa hadi sasa Mkoa huo ni shuwari na hakuna tukio lolote kubwa la kushtua.
Alifahamisha kuwa changamoto kubwa ambazo zipo katika Mkoa huo ni wizi wa mifugo, lakini wanaendelea kupambana nayo ili kuhakikisha wanaofanya vitendo hivyo wanathibitiwa na kufikishwa mbele ya sheria.
Hata hivyo ACP Sadi alimpongeza Mbunge huyo kwa msaada alioutoa kwao na kumuahidi kuwa gari hilo watalitunza na kulitumia kama inavyotakiwa.
MWISHO.