UJENZI NJIA ZA WANYANAMA PORI ‘SHOROBA’ KILOMBERO
-Wananchi waramba fidia walioathiriwa na ujenzi
‘STEP’ yawaanzishia vikoba 250 kubadili maisha yao
NA ABDI SULEIMAN, PEMBA
“HAIKUWA kazi rahisi, kuwaelimisha wananchi mapaka kukubali, kutoa maeneo yao, kwa ajili ya ujenzi wa njia za wanyama pori ‘Shoroba’ na sasa imeshajengwa,’’ anasem Meneja Mpango wa kuhifadhi Tembo kusini mwa Tanzania ‘STEP’ Joseph Mwalugelo.
Shoroba ni njia maalum, ambayo hupitwa na wanyama pori kutoka eneo moja kwenda jingine.
Kwa kwaida, wanyama wanapohama au kwenda kutafuta chakula au malisho, hujitengenezea njia zao maalum, iwe wakati wa kwenda ama kurudi.
Shoroba, ama njia za wanyama pori, zinaendelea kujengwa kwenye hifadhi ya Nyerere iliyopo wilaya ya Kimlombero hamlashauri ya mji wa Ifarakara mkoani Morogoro hadi kwenye hifadhi ya taifa ya milima ya Udzungwa mkoani humo.
Shoroa hiyo ambayo ina urefu wa kilomita 13 na upana wa mita 50 ni njia za wanyama wote pori hasa Tembo, lengo hasa likiwa ni kuwadhibiti wanyama hao na uharibifu wa mazao ya wannachi.
STEP inawashukuru wananchi wa vijiji vya Kanyenja, Sole, Katurukila na Mangula A, vilivyomo kwenye Halmashauri ya mji wa Ifakara.
STEP inasema juhudi nyingi zimechukuliwa katika kuhakikisha mnyama Tembo haharibu mazao ya wananchi, wala kutishia amani kwa wanavijiji muda anapotoka usiku.
Mratibu wa mradi wa kuboresha mahusiano kati ya Tembo na binaadamu kutoka taasisi ya ‘STEP’ Kim Lim, anasema lengo ni kuona mnyama Tembo anapotoka kwenye hifadhi hasababishi usumbufu kwa wananchi.
Hali iliyowalazimu kutafuta vijana kutoka katika vijiji sita, ambao ni maalumu kwa kuchukua taarifa za Tembo wanapotoka, wanapokwenda na kipi wanafanya kwa kutumia vifaa maalumu.
Kuanzia mwezi Januari hadi Sepetemba 2022 matukio ya Tembo kutoka, Kanyenja tembo wametoka sana, huku kijiji cha katulukila na magombela, Msola stasheni wanawasaidia kujua njia gani wanaweza kupunguza uharibifu wa mazao.
Kim anasema wanatumia njia mbali mbali za kudhibiti Tembo, ukiachana na ushoroba, ikiwemo njia ya fensi ya mizinga ya nyuki, ambapo wamefanya utafiti na wamejifunza kama Tembo wanaogopa nyuki.
Aidha anasema kijiji cha Kanyenja takwimu tokea 2019 hadi 2022, 2019 walipata matukio 167, mwaka 2022 walipata matukio 300, ndani ya siku unaweza kuwa na matukio zaidi ya moja,
“Tuna mizinga ya nyuki 450, kila fensi na idadi yake Njokomoni ipo Udzungwa inaurefu wa kilomita 1, fensi Mgombela ina urefu wa kilomita 2.6 inategemea kiujumla kuna fensi saba hadi sasa.
UZIO WA MAJARIBIO
Mratib wa mradi wa kuboresha mahusiano kati ya Tembo na binaadamu Kim Lim, anasema zipo njia tatu za majaribio kwa ajili kupunguza Tembo kuingia katika mashamba ya wakulima.
Njia ya kwanza ni Fensi ya Harufu, hii huchanganywa vitu mbali mbali ikiwemo pilipili, Vitunguu Soum, Tangawizi, uarubaini/mtunda, mayai, kinyesi cha ngombe au tembo na kuchemshwa kwa pamoja na kuhifadhiwa kwa wiki nne hadi sita.
Anasema baada ya kuoza huwekwa kwenye chupa za maji na kuzifunga kwenye fensi, Tembo hapendi harufu kwa muda inasaidia ila baadae wameizowea.
Njia ya pili ni taa za sola, hapa tunafensi mbili hadi sasa kuanzia Julai 2020 hadi Disemba 2022, wamejifunza fensi ya taa imefanyakazi kwa asilimia 74 Tembo wanaikwepa na kutafuta sehemu ambayo haina fensi wanaenda kuvuka.
Aidha njia ya tatu ni fensi ya Mabati, hii inatumiwa sana nchini Kenya na India, tunataka kuweka kwani Tembo hapendi kelele fensi hii inaweza kutusaidia.
UPANDE WA VIKUNDI
Anasema mpaka sasa wanafanya kazi na wakulima 250, wanawake 133 wanaume 126, ambao wanasajiliwa katika vikundi na baadae wanatengeneza fensi ya mizinga na kuvuna asali.
Mwaka 2021 walivuna lita 262.5 na mwaka 2022 walivuna lita 406, ambapo lita moja ya asali inauzwa shilingi 10,000, lakini sisi tunawauzia kwa shilingi 15,000 hadi 20,000 kwa lita.
“Shida kubwa ni soko kwa sasa wakulima wanauza asali kwa bei ndogo, kwa vile wanatusaidia kulinda Tembo na kuboresha mahusiano baina ya Tembo na watu, sisi tumechukua asali zao na kuuza kwa ebi ya juu,”amesema.
Anasema Vipo vikundi vimenunua mashamba ya miwa wanalima kama kikundi, wapo wamenunua viti na wanakodisha, ni wachache sana wanaotaka kugawana, wapo walioanzisha miradi ya sabuni.
VIKOBA
Vikundi vinakopeshana wenyewe kwa wenyewe pesa zao walizoweka, STEP nayo inatoa mikopo kwa vikundi na wanarudisha bila ya riba, wanaanza na shilingi 500,000 baada ya kuangalia maendeleo ya kikundi wanawape milioni, wapo waliokopa hadi shilingi milioni 3.
Mwaka 2021 mikopo ilikuwa 114 ilitolewa yenye thamani ya shilingi milioni 129.8, walikopeshana kupitia fedha zao na STEP walifanikiwa kutoa mikopo yenye thamani ya shilingi milioni 35 na mwaka 2022 ilikuwa ni mikopo 137 yenye thamani shilling milioni 22.54 na STEP kutoa shilingi milioni 700,000.
SUALA LA ELIMU
Anasema STEP inatoa elimu katika skuli mbali mbali juu tabia za Tembo kiekolijia na biolojia, katika kuboresha mahusiano baina ya tembo na watu na jinsi ya kuwa salama unapokutana nae.
“Tembo anakimbia kilomita 35 kwa saa, wakati binaadamu anaweza kukimbia kilomita 11, lazima wananchi na wanafunzi kupatiwa elimu,”amesema.
Mwaka 2021 ilizifikia skuli 15, zenye wanafunzi 6715 wanawake 3340 na wanaume 3375, huku mwaka 2022 skuli zilikuwa 19 zenye wanafunzi 7,124 wanawake 3754 na wanaume 3370.
Wananchi walipatiwa elimu kwa vitendo jinsi fensi za mizinga zinavyofanya kazi, pamoja na kuwapeleka kwenye hifadhi ya Mikumi na Udzungwa kujifunza kwa vitendo.
Mwaka 2021 walipeleka wanafunzi 48 Udzungwa, mwaka 2022 wanafunzi 143 wanawake 72 na wanaume 71, kwa upande wa Mikumi walipeleka wanafunzi 177 wanawake 92 wanaume 85.
Aidha anasema mwaka 2021 wametoa elimu kwa wananchi 2213, mwaka 2022 watu 2936, katika vijiji vya Mangula B, Mkula, Sola Stasheni, Kanyenja, Mgombela, Sole, Nyange.
UTALII
Anasema wanafanya utalii kupitia fensi ya mizinga ya nyuki, wanapokea wageni kutoka nje au ndani ya Tanzania, wanajifunza inavyofanyakazi na pesa zinaenda kwenye vikundi.
WANANCHI WANASEJEMAJE
Mfuatiliaji wa Tembo Juma Mahula kutoka kitongoji cha Milesa, anasema Shoroba ya Kilombero, imewasaidia kutokana na uharibufu waTembo, kwani taasisi ya ‘STEP ‘imeweka fensi na kuwasaidia wakulima.
“Kabla, matukio mengi ya Tembo yalikuwa yanatokea, sasa yamepungua baada ya uwepo wa njia zao maalum na wanapita mita 500 upande mwengine,”amesema.
Anasema lengo ni kuona wananchi wanalima mazao yao, bila ya kuharibiwa na Tembo, kwani sasa mradi umeweza kuwaokoa na kupunguza kasi ya uharibifu wa mazao.
Naye Mohamed Ali anasema tayari alishafanyiwa uharibifu na Tembo ekari 1.5 ya mpunga mwaka 2019/2020, mradi wa ushoroba umepokelewa vyema na jitihada za serikali bado zinaeleweka.
‘STEP’ wametushawishi kuunda vikoba na kutusaidia kwa kiasi kikubwa, wametupatia elimu na vitu mbali mbali wameweka kwa kuzuwia Tembo na kutokuharibu mashamba ya wakulima.
Kwa upande wake Mrashi Jumbe Dongwe mkaazi wa kijiji cha Sanjo kata ya Mkula, amesema kila mkulima alilipwa kulingana na mashamba yake na mazao yalilopo shambani.
Amesema fedha baada ya kupatiwa alitafuta eneo jingine kwa ajili ya kilimo, kwani taasisi ya STEP iliwasaidia elimu juu ya utafutaji wa miradi na uwekaji wa vikoba.
Meneja wa Shoroba, kutoka Mpango wa kuhifadhi Tembo kusini mwa Tanzania ‘STEP’ Joseph Mwalugelo, anasema vijiji vitatu vilivyopitiwa na mradi wa ushoroba vilepwa shilingi bilioni 1.7, baada ya wananchi kukubali kufanyiwa tathmini mwaka 2022.
“Baada kuidhinishwa tu kabla ya miezi sita tuliweza kulipa fedha zote, laiti kama ingechelewa ingekua hasara kwetu,”alisema.
Anasema tayari tathimini ya pili imeshafanyika na jumla ya shilingi milioni 261 zitalipwa kwa wananchi 52, lengo ni kuona wananchi wananufaika na Shoroba ya Kilombero.
“Shoroba ya hii ni kati ya maeneo muhimu sana Tanzania, kwani zipo zaidi ya 60, nyingi zimekua katika hali sio nzuri na nyingine zimeziba na kuwa maeneo ya makaazi ya wananchi,”anasema.
Naye Meneja ushirikishwaji wa sekta binafsi wa USAID Tuhifadhi Maliasili Dk. Eliakana Kalumanga, amesema maeneo yaliyohifadhiwa ambayo hutumiwa na wanyamapori, yanapaswa kuendelea kulindwa hata binaadamu maeneo hayo yanawasaidia.
Amesema maeneo ya Shoroba wanyama huyatumia kwa shughuli zao za kimaisha, kwa kujipatia chakula na mambo mengine, ambapo binaadamu nae hunufaika kwa asilimia kubwa.
“Baadhi ya maeneo ya misitu yanavutia watalii, yanafaida kiuchumi ikiwemo uwekezaji wa hoteli ya kitalii, mfano Shoroba ya kwakuchinja inaunganisha hifadhi ya Burunge, Tarangire na Ziwa manyara, Shoroba ya Kilombero inaunganisha hifadhi ya taifa ya Udzungwa na hifadhi ya Nyerere,”anasema.
WAANDISHI WA HABARI
Felsite Peter anasema shoroba ya kilombero ni moja ya shoroba inayowalengwa kuwalinda wanyama dhidi ya mauwaji kugongwa na gari au reli ya Tazara, baada ya ujenzi wa jia za chini ya barabara kukamilika.
“Shoroba hii kama itakamilika basi itakua ya mfano kutokana na juhudi zinazochukuwa na wasimamizi wake STEP na hatua walizofikia kwa sasa,”amesema.
Janeth Jovin anasema wananchi wa vijiji vilivyopitiwa na ushoroba wa kilombero, wanapaswa kuwashuhuru STEP kwa kazi kubwa walioifanya ya kwaelimusha juu ya umuhimu wa ushoroba na kuridhia kutoa sehemu zao za kilimo.
JET INASEMA JEE
Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha waandishi wa habari za Mazingira Tanzania ‘JET’, John Chikomo amesema kumekuwa na ongezeko la wanyamapori katika baadhi ya hifadhi, jambo ambalo limechangiwa kwa kiasi kikubwa na uhifadhi wa wanyamapori.
“Hata ongezeko la watalii wanaoingia nchini ni mafanikio yanayotokana na elimu ya uhifadhi wa mazingira na wanyamapori inayotolewa mara kwa mara kwa waandishi wa habari hapa nchini,” alisema.
Naye Mwenyekiti wa JET, Dk. Ellen Otaru amesema wakati sasa kwa vyombo vya habari, kujikitaka katika habari za uhifadhi na utunzaji wa mazingira, ili wananchi waweze kuona umuhimu wa utunzaji wa shoroba kwa maslahi ya taifa.
MWISHO
Abdi Juma Suleiman