NA ZUHURA JUMA, PEMBA.
WANANCHI wa Wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba wamesema, kuna kesi nyingi za udhalilishaji hufutwa mahakamani hasa za watoto kuanzia miaka 15 hadi 17 kutokana na kukataa kutoa ushahidi, jambo ambalo linasababisha matukio hayo kuongezeka.
Wakizungumza na Zanzibarleo kwa nyakati tofauti katika vijiji vya Wilaya hiyo wananchi hao walisema, kuna haja ya kudhibitiwa sababu ambazo zinachangia watoto hao kukataa kutoa ushahidi ili kuona kwamba wanakuwa mstari wa mbele kutoa ushahidi kwa lengo la kuwatia hatiani watendaji wa makosa hayo.
Mmoja wa wananchi hao Time Ali Bakar mkaazi wa shehia ya Kiungoni alisema, sababu ambazo zinachangia watoto hao wasitoe ushahidi ni shinikizo la wazazi wao kwani baada tu ya kujulikana mtoto amefanyiwa udhalilishaji, wanawambia wasitoe ushahidi ili kuharibu kesi.
“Wakisharudi Polisi, wanaambiwa wasitoe ushahidi, ili wasije kugombana familia au majirani, hivyo kwa hali hiyo mtoto hata umuwekee kisu shingoni hasemi ukweli”, anaeleza.
Kwa upande wake Bakari Suleiman Juma mkaazi wa Kambini alisema, sababu kuwa ni rushwa muhali iliyotawala kwenye jamii, kwani hawaangalii ukubwa wa kosa bali wanaangalia ukaribu wao na mtuhumiwa tu.
“Wazee wanaweza kukaa pamoja kusuluhisha, lakini pia vitisho anavyopewa mtoto kutoka kwenye familia ya mwanaume vinaweza kumsababishia aogope kutoa ushahidi”, alieleza.
Nae Bikame Aki Othman wa Kambini mwenye umri wa miaka 55 alisema, inawezekana ikawa wameshapanga mambo yao ya utu uzima, hivyo akashindwa kusema ukweli kwa sababu ikiwa sio kugundulikana angekaa kimya na kuendelea kufanyiwa kitendo hicho kila siku.
Mtoto mwe umri wa miaka 17 Maryam Faki Ali mkaazi wa shehia ya Minungwini alisema, watoto wenye umri huo hawapendi kutoa ushahidi kwa sababu huwa kuna makubaliano baina yake na mwanaume.
“Vijana wengi siku hizi hawapendi kuwa ‘single’, kwa hiyo anaweza kukwambia ikiwa unanipenda tufanye mapenzi ili unithibitishie na lazima watafanya, hivyo mwanamke atakapopelekwa mahakamani hatoi ushahidi”, alieleza.
“Wakati mwengine anatishiwa kwa kuambiwa, iwapo atasema, atamfanyia kitu kibaya ajute katika maisha yake yote, hivyo anajiona yupo hatarini atakapotoa ushahidi”, alieleza Salma Hamad Omar mwenye umri 19 mkaazi wa kijiji cha Patini ya Mzambarau Takao.
Mratibu wa wanawake na watoto shehia ya Mzambarau Takao Fatma Hamad Nassor alisema, sababu ya watoto wenye umri huo kukataa kutoa ushahidi kuwa aghalabu tukio linatendeka kwenye familia.
“Siku ya kwanza atatoa maelezo mazuri Polisi lakini akirudi tu nyumbani kwao anawekwa kitako na familia yake kuambiwa asiseme, hivyo mtoto hubadilisha ushahidi anapoitwa tena”, alieleza.
Mkuu wa Idara ya Ustawi wa Jamii Pemba Omar Mohamed alisema, wamekuwa wakikosa ushirikiano kwa watoto wenye umri huo wanapofikishwa mahakamani, ima kwa kutishiwa na wale wanaowabaka au kutokana na kuwalinda wapenzi wao, hivyo wanaogopa kufungwa.
Mratibu wa TAMWA Pemba Fat-hiya Mussa Said alifahamisha kuwa, watoto hao wana changamoto kubwa ya kukataa kutoa ushahidi mahakamani au kukataa ushahidi ambao wameshautoa vituo vya Polisi kutokana na kutokujielewa.
“Huku tunakotoka hatujawafundisha watoto masuala ya kujiamini, kujithamini, kujitathmini, ili waweze kufikia ndoto zao, sasa wanakwenda kujingiza kwenye mambo mabaya na wanapodhalilishwa wanashindwa kusimulia haki yao”, anasema.
Hali hiyo inapelekea kuwa na kiasi kidogo cha kesi zilizo amualiwa hadi mwisho, kwani takwimu za Jeshi la Polisi Wilaya ya Wete Pemba zinaonyesha kwa kipindi cha mwaka 2020 na 2021 jumla ya kesi 58 ziliripoitiwa zinazohusiha watoto kati ya umri wa miaka 15-17, ambapo kesi nane tu washatikiwa walihukumiwa ukilinganisha na kesi 43 zilizofutwa ama mahakamani na katika vituo vya Polisi.
Hakimu wa mahakama maalumu ya kushughulikia kesi za udhalilishaji Mkoa iliyopo Wete, Ali Abdulrahman Ali anataja kesi za kubaka ambazo zimefikiwa mahakamani kuanzia mwaka 2020 hadi 2021 ni 49 huku za watoto kati ya umri wa miaka 15-17 zikiwa 19, ambapo nne washtakiwa wamefungwa, mbili wametozwa faini na kesi 13 zimeongolewa (kufungwa).
MWISHO.