Monday, November 25

UTPC yawapiga msasa waratibu wa klabu za habari Tanzania

Na mwandishi wetu.
WARATIBU wa klabu za Waandishi wa habari Tanzania wametakiwa kufanya kazi kwa bidii na kuwa Kiungo Bora kati ya klabu hizo na  umoja wa klabu za waandishi wa habari Tanzania( UTPC) na kutekeleza kwa ufasaha  mkakati mpya wa UTPC wa “from Good to Great”.
Hayo yamesemwa Leo na Rais wa Umoja wa klabu za Waandishi wa habari Tanzania (UTPC),Deogratius Nsokolo alipokuwa akifungua mafunzo ya siku tatu ya waratibu wa klabu za Waandishi wa habari Tanzania yanayoendelea Jijini Dar es salaam.
Deo amesema,klabu za  waandishi wa habari ndio nguzo za kuimarisha UTPC na kuifanya kuwa na   utendaji ulio na tija na kuleta  mabadiliko yanayohitajika katika utekelezaji wa mkakati mpya wa miaka mitatu 2023 hadi 2025.
“Tunatakiwa kuanza safari pamoja na kutokwamishana  na vema fursa hii ya mafunzo iweze kutumika kuitoa taasisi yetu katika hatua nzuri ya mabadiliko yenye tija zaidi”Anasema Deogratius na kuongeza:
“Waratibu ni wakurugenzi wa Klabu za habari huko kwenu, kama ilivyo kwa Mkurugenzi wa UTPC, hamkuajiriwa kwa bahati mbaya ni vyema kutumia nafasi yako vizuri ili kuleta mabadiliko kwa kuwa na ubunifu,uadilifu,nidhamu na kutunza siri za ofisi” Anasema Deogratius.
Kwa upande wake,Mkurugenzi  wa Umoja wa klabu za Waandishi wa Habari Nchini (UTPC),Kenneth  Simbaya amesema safari ya mabadiliko ya UTPC inahitaji ushirikiano wa Hali ya juu.
“Naomba wote mshiriki mafunzo haya kwa manufaa, na kuhakikisha wote tunanufaika nayo kwa taasisi na kwa maisha binafsi, ni vema tuwe katika darasa na kusikiliza kwa umakini,”amesema.
Amesema mafunzo hayo ni mwanzo wa mabadiliko ya mfumo wa utendaji wa UTPC kutoka ilipokuwa hapo mwanzo na kuifanya kuwa Bora zaidi.
Jumla ya waratibu 26 kutoka mikoa ya Tanzania bara na Zanzibar wanashiriki mafunzo hayo ambayo lengo lake kuu ni kuwajengea uwezo kiutendaji.