NA HANIFA SALIM, PEMBA
MKUU wa Wilaya ya Micheweni Mgeni Khatib Yahya amesema, bado Wilaya yake inauhitaji mkubwa wa kupatiwa misaada mbali mbali ikiwemo chakula hasa katika kipindi hichi cha mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Aliyasema hayo alipokua akizungumza na wananchi wa shehia ya Tondooni kijiji cha Mkia wa N’gombe mara baada ya kumaliza zoezi la kukabidhi wananchi wa shehia hiyo msaada wa chakula, uliotolewa na benki ya watu wa Zanzibar PBZ kwa kushirikiana na taasisi ya Asma Mwinyi Foundation.
Alisema, mahitaji ya wananchi wa Wilaya ya Micheweni ni makubwa hasa katika mwezi huu mtukufu, kwani msaada huo ambao umetolewa kwa wananchi wa Mkia wa N’gombe umeweza kutatua mahitaji ya wananchi hao.
“Napenda kuishukuru taasisi ya Asma Mwinyi Foundation kwa kushirikiana na benki ya PBZ kwa hichi ambacho wamekifanya katika wilaya yangu ya Micheweni, niendelee kuziomba taasisi nyengine ambazo zina malengo ya kuleta msaada wasisite kutufikia”, alisema.
Nae Mkurugenzi mwanzilishi wa taasisi hiyo Zanzibar Asma Hussein Ali Mwinyi alisema, sadaka hiyo ya futari ni kwa ajili ya wanawake, mayatima, wajane, wazee na watoto wenye mahitaji maalumu ukiwa na lengo la kuwasaidia kujikimu hasa katika kipindi hichi cha Ramadhani.
“Futari hii tumetoa kwa upande wa Unguja vifurushi 300 na Pemba vifurushi 300 thamani yake jumla ni milioni 80, tumetoa Mkia wa N’gombe kwa sababu tumeona kwenye hichi kijiji kuna uhitaji mkubwa wa huu msaada, msaada huu tumefadhiliwa na benki yetu ya PBZ ndio wafadhili”, alisema.
Kwa upande wake Meneja wa benki ya Kiisilamu Tawi la Chake chake Said Saleh Rashid alisema, msaada huo umefadhiliwa na PBZ Ikhlasi kwa kushirikiana na taasisi ya Asma Mwinyi Foundation kwa lengo la kuwasaidia wananchi wa shehia ya Tondooni.
Alisema, benki yao inatoa huduma mbali mbali ikiwemo kufungua akaunti kwa ajili ya kuweka akiba, kutoa mikopo ya aina tofauti hivyo, hawana budi kushirikiana na wananchi na hawatoacha kuwaunga mkono katika kuwasaidia kupitia nyanja mbali mbali.
Akitoa neno la shukurani kwa niaba ya wananchi wenzake Maryam Abushiri Hamad aliishukuru taasisi ya Asma Mwinyi kwa kujitokeza kuwasaidia katika kijiji chao ambacho kimekua kikiachwa nyuma na baadhi ya wafadhili alisema, wamefarijika sana kwa kupatiwa msaada huo.
MWISHO.