NA ABDI SULEIMAN.
WANAWAKE watiania wamesema moja ya changamoto kubwa inayowarudisha nyuma kuwania nasafi za uongozi katika changuzi mbali mbali zinazofanyika ni uwepo wa vitisho wanavyokumbana navyo kutoka kwa wagombea wenzao.
Wamesema vitisho hivyo huwafika wao, pamoja na familia zao na wakati mwengine wagombea hao huwafuata wazazi wao au waume zao ili kukatazwa kuachia nafasi hiyo aliyogombea.
Wakichangia mada mbali mbali wakati wa mafunzo ya siku mbili yaliyoandaliwa na Jumuiya ya PEGAO, kwa Wanawake wanaotarajiwa kugombea nafasi za uongozi na siasa katika mchakato wa Kidemokrasia Kisiwani Pemba, ikiwa ni utekelezaji wa mradi SWILL, unatekelezwa kwa pamoja kati ya TAMWA Zanzibar, ZAFELA na PEGAO kwa ufadhili wa Ubalozi wa Norway nchini.
Mmoja ya watia nia hao Asha Ali Abdalla kutoka chama cha ACT-Wazalendo, alisema suala la vitisho ndani ya vyama vimekua vikiwavunja moyo wanawake wengi na wengine hulazimika kuachia ngazi ili kunusuru maisha yake au familia yake.
“Nilipo tangaza nia ya kuingia jimboni, baadhi ya watu waliweza kunifata na kumtaka kuwamchia mtu kwa mwaka ule, lakini sikurudi nyuma nikachukua fomu, mwisho wa siku walifika mpaka kwa mama yangu na kumwambia anikataze,”alisema.
Naye Asha Said Salum kutoka Chadema, aliwataka viongozi wa juu wa vyama kuacha tabia ya kuwakumbatia wenyefedha na kuwacha wanawake wenye nia thabiti ya kuwasaidia wanawake na watoto.
“Wanawake wengi wanania thabiti ya kugombania nafasi za uongozi, lakini viongozi wa juu wa vyama husika ndio wanaorudisha nyuma na kufuta ndoto, huu ni mfumo dume amboa umezoeleka kwenye baadhi ya vyama,”alisema.
Kwa upande wake Maryam Abdalla Salim kutoka ACT-Wazalendo, aliwataka wanawake wenzake kuwa na uthubutu au utayari, wakati wanapoamua kuingia majimboni.
Stara Khamis Salum kutoka CCM Wilaya ya Chake Chake, alisema bado wanawake wanakumbana na masuala ya ubaguzi wakati wa chaguzi zinapofika, hivyo wanapaswa kushirikiana na kufikia ndoto zao.
Hata hivyo aliwataka wanawake wenzake wenye nia ya kuingia majimboni, kuhakikisha wanatengeneza ngome zao mapema ili wakati utakapofika inakua ni rahisi kwao.
Mwezeshaji wa mafunzo hayo mwanaharakati wa masuala ya wanawake Kisiwanai Pemba Sabahi Mussa Said, alisema lengo la mafunzo hayo ni kuhakikisha wanawake wanachangia kwa kiasi kikubwa katika maendeleo ya nchi.
Alisema wanawake wanaumizwa na suala zima la maendeleo tafauti na wanaume, kwani wao ndio wanaohangaika kwa kutafuta huduma mbali mbali ikiwemo kijamii.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mradi wa SWILL kutoka PEGAO Hafidhi Abdi Said, alisema ni wakati wakubadilika sasa na suala la uongozi sio la mtu mmoja lazima kuwe na mashirikiano ya pamoja.
Alisema PEGAO kupitia mradi wa SWILL wanahitaji mabadiliko makubwa, katika kuwania nafasi za uongozi hususana majimboni ili uchaguzi utakapofika 50% kwa 50%iweze kupatikana.
Naye Mratiba wa TAMWA Pemba Fat-hiya Mussa Said, alisema malengo ya mradi wa SWILL ni kuwawezesha wananchi 6000 na tayari wameshavuka lengo hilo.
Alisema PEGAO imeanza maandalizi mapema ya kuwanoa wanawake kuingia katika uongozi, ili kuweza kufikia malengo yao ya kusimama na kuwania nafasi za uongozi majimboni.
MWISHO