Monday, November 25

TUENDELEE KUHAMASISHA UPANDAJI MITI NA UTUNZAJI WA VYANZO VYA MAJI

Hayo yamesemwa leo tarehe 03 Mei 2023 na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2023 Bw. Abdallah Shaib Kaim wakati  wa ukaguzi wa shughuli za uhifadhi katika  Hifadhi ya msitu wa New Kidabaga Ulogambi uliopo Wilayani Kilolo ambapo shughuli mbalimbali za uhifadhi wa vyanzo vya maji unafanyika katika msitu huo

Katika hotuba yake ameendelea kutoa pongezi kwa juhudi za makusudi zinazochukuliwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania katika kuhakikisha suala la uhifadhi linapewa kipaumbele katika maeneo mengi nchini.

Hata hivyo ameongeza kuwa nidhahiri kuwa suala la uhifadhi wa misitu ni kichocheo kikubwa cha uwepo wa vyanzo vya maji vilivyo ndani na visivyo vya  hifadhi.

Amesisitiza kuwa ni wakati sasa wananchi kuhakikisha misitu iliyopo inatunzwa kwa namna mbalimbali ikiwa ni pamoja na uzalishaji wa miche mbalimbali ambayo ni rafiki kwa vyanzo vya maji na kuhakikisha inapandwa kwa wingi na kuitunza.

Amesema kuwa TFS ihakikishe inaendelea na suala la utoaji wa elimu kwa wananchi juu ya uhifadhi na utunzaji wa vyanzo vya maji ili kuhakikisha mazingira yanatunzwa kwaajili ya vizazi vya sasa na baadae.

Naye  Mhifadhi wa Wilaya ya Kilolo Essau Mhonda wakati akiwasilisha taarifa ya msitu uliokaguliwa na Mwenge wa uhuru amesema kuwa TFS kwa kushirikiana na wananchi na wadau mbalimbali wa mazingira wamekuwa wakiendelea kusimamia upandaji wa miti, uhifadhi wa misitu iliyopo kwa kufanya doria za mara kwa mara, kusimamia uundwaji wa vikundi vya miradi rafiki ya mazingira, kupima na kuandaa mpango wa usimamizi wa hifadhi.

Aidha aliongeza kuwa wananchi wa Kidabaga na maeneo mengine wananufaika na uwepo wa hifadhi hiyo ikiwemo kupata fursa za ufugaji nyuki ndani ya msitu, kivutio cha utalii, tafiti mbalimbali na ni chanzo kilicho ndani ya msitu ambacho kinachangia  maji yake katika mradi mpya wa bwawa la Mwl. Nyerere.

Ikumbukwe Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2023 unaongozwa na kauli mbiu isemayo:

“TUNZA MAZINGIRA OKOA VYANZO VYA MAJI KWA USTAWI WA VIUMBE HAI NA KWA UCHUMI WA TAIFA”