Friday, October 18

Dk. Hussein Ali Mwinyi :Nitasimamia uwajibikaji na watakoshindwa nitawawajibisha.

MAKAMU Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein, akisalimiana na Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia chama cha Mapinduzi CCM Dk.Hussein Ali Mwinyi, wakati wa mkutano wa ccm uliofanyika katika uwanja wa Mpira wa Gando Star Wilaya ya Wete.(PICHA NA ABDI SULEIMAN, PEMBA)

NA HAJI NASSOR, PEMBA

 

 

NGOMBEA urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema iwapo wananchi wa Zanzibar watampa ridhaa ya kushika nafasi hiyo, atahakikisha, anasimamia uwajibikaji na watakoshindwa atawawajibisha, ili mafanikio ya kweli yapatikane.

Alisema, hayo ndio kipaumbele chake cha kwanza mara atapomaliza kuapishwa, kwani mambo hayo ni miongoni mwa yanadhoofisha kwa kiasi kikubwa maendeleo ya jamii.

Mgombea huyo wa urais, aliyasema hayo Jimbo la Gando wilaya Wete mkoa wa kaskazini Pemba, alipokuwa akizugumza na mamia ya wanaccm na wananchi wengine, kwenye mkutano wa hadhara wa kampeni wa chama hicho.

Alisema kuwa, serikali atakayoiongoza hatopenda hata kidogo kuona ndani yake, mna watendaji wasiopenda kuwajibika, kwani wanakuwa kikwazo kufikia maendeleo yaliokusudiwa.

Alisema, jambo hilo ni adui mkubwa wakufikia maendeleo ya  Zanzibar, na kuendelea kudumaa kwa baadhi ya sekta, jambo ambalo halikubaliki na atalisimamia kwa dhati.

“Mkinichagua kuwa rais wa Zanzibar, pamoja na mambo kadhaa ambayo ntawafanyia, lakini suala la uwajibikaji ndio kipaumbele cha kwanza, na akitokezea mtendaji kushindwa kuwajibika, ntamuwajibisha,’’alieleza.

Aidha mgombea huyo wa urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM Dk. Hussein Ali Mwinyi, amewaahidi wananchi wa Zanzibar kama akipata ridhaa, atahakikisha anaimarisha miundombinu ya barabara, ili iwe ya kisasa zaidi.

Alisema, bara bara ambazo ataanza nazo kwa kisiwani Pemba, ni ile ya Chake Chake – Wete yenye urefu wa kilomita 21, Finya- Kicha yenye urefu wa kilomita 8.8 na zile ndani ya mji wa Wete zenye urefu wa kilomita 9.

Alisema kuwa, ili Zanzibar ipige hatua kubwa kwenye maendeleo ya sekta ya utalii, viwanda, uvuvi inategemea sana uwepo wa barabara za kisasa, katika maeneo yote ya Unguja na Pemba.

Alisema, ingawa tayari rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein anaemaliza muda wake, ameitekeleza kwa kiwango kikubwa Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020, lakini kwa yale maeneo yaliobakia, atayakamilisha.

Alieleza kuwa, barabara za kisasa na zenye kiwango kikubwa, ndio miongoni mwa vilainishi vya kufikia maendeleo makubwa, na sio Zanzibar pekee bali nchi zote duniani.

“Kila mmoja ni shahidi kuwa, Inali ya CCM ya mwaka 2015/2020 Dk. Shein, ameitekeleza kwa karibu asilimia 100, karibu kila sekta na mimi mkinichagua, nitazidi kuziimarisha,’’alifafanua.

Jengine ambalo amewahidi wananchi kuwa atawafanyia, ni kupiga vita suala la udhalilishaji pamoja na dawa za kulevya, ambapo alisema tatizo hilo amekuwa akilishuhudia kila anapopita.

Alieleza kuwa, tatizo hilo linamnyima usingizi na ndio maana mara akichaguliwa. atahakikisha anafanya kila mbinu kuona udhalilishaji na dawa za kulevya, zinakuwa historia Zanzibar.

Aidha mgombea huyo wa urais alisema, kutokana na mengi ambayo aliyafanya rais anayemaliza muda wake, kazi yake itakuwa ndogo mara akiingia madarakani;

Alisema tayari Dk. Shein ameliimarisha zao la karafuu na kusababisha kuvunwa kwa tani 3,321 mwaka 2015 na kufikia tani 8,277 ambazo ni nyingi mno.

Aidha alisema, eneo jengine ambalo limefanikiwa kwa kiasi kikubwa ni sekta ya elimu , kwa kujengwa skuli za ghorofa za Kizimbani, Limbani na ile Chasasa pamoja na chuo cha amali kilichopo Daya wilaya ya Wete.

Kuhusu kuliimarisha zao la mwani, Dk. Mwinyi alisema, tayari serikali ya awamu ya saba, imeshaanza ujenzi wa kiwanda ya kusarifia mwani, eneo la Chamanangwe sambamba na kukabidhi wa vihori 80  wakulima wa mwani wa wilaya ya Wete.

‘’Ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020, lazima nikiri kuwa ilipata msimamizi Dk. Shein, maana hata sekta ya utalii imeimarika kwa kuongeza watalii 53,800 kutoka watalii 37,900 mwaka 2015,’’alifafanua.

Katika hatua nyingine, mgombea huyo wa urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM, amewashauri wananchi wa Zanzibar kuhakikisha kura zao hawazipotezi, kwa kuvipa vyama ambayo havina muelekeo.

Alisema CCM ndio chama kinachojali maisha ya watu wote wakiwemo wanyonge, wakulima na wakwezi hivyo, dhamira hiyo haiwezi kuendelezwa na kiongozi yeyote, isipokuwa wanaotoka CCM.

‘’Tupeni ridhaa sisi wagombea wote wa CCM, ili tuendelee dhamira na ari ya kweli ya kuwatumikia, pasi na kujali maeneo mnayotoka wala rangi, na hii ndio shabaha ya waasisi wa taifa hili,’’alieleza.

Mapema rais wa Zanzibar wa na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, amesema CCM imewaletea kiongozi mchapakazi kwa wananchi wa Zanzibar.

Alisema sifa za Dk. Mwinyi za nidhamu, uhodari wa kazi, kuwajali watu wote na ubobevu wa uongozi, hanazo mgombea mwengine yeyote kwa nafasi yoyote kutoka vyama upinzani.

Alieleza kuwa, Dk. Miwnyi amekuwa anajali sana shida za watu na kupelekea kushika nafasi mbali mbali, kuanzia serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na ile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

‘’Kazi iliyofanywa na mikutano yote ya CCM na kisha kupatikana kwa mgombea huyo Dk. Hussien Miwnyi haikukosea, maana uchapakazi wake unaonekana na kila anapokabidhiwa madaraka,’’alieleza.

Hata hivyo rais huyo wa Zanzibar, alisema kutokana na kuelewa vyema majukumu ya urais kutokana na ugumu wake, na jinsi anavyomfahamu Dk. Mwinyi, basi anauweza bila ya wasi wasi.

Alieleza kuwa, Dk. Mwinyi ndio mgombea pekee ambae anafaa kwa asilimia 100 kuwa rais wa Zanzibar, hasa kwa busara zake na utii wa kazi.

‘’Dk. Mwinyi anafaa kwa asilimia 100 kuwa rais, maana mimi nauwelewa sana na sijaona kiongozi mwengine anaeuweza baada ya mgombea aliyetuliwa na CCM,’’alifafanua.

Hivyo, amewataka wananchi wa Zanzibar kuhakikisha wanawapigia kura viongozi wa majimbo na wadi pamoja na mgombea huyo, ili aendelea kuwatumikia wananchi.

Alifahamisha kuwa, dhamira ya CCM kila siku ni kuona wananchi wake wanaishi kwa amani na utulivu, hivyo ili hilo litekelezeke ni kuwapigia kura wagombea wa CCM.

“Siku ya tarehe 28, Oktoba mwaka huu, siku hiyo ya kupiga kura ikifika, muhakikishe hamfanyi makosa, na muwapigie kura rais John Pombe Magufuli, Dk. Hussein Mwinyi, wabunge, wawakilishi na madiwani wetu wote,’’alieleza.

Naibu Katibu mkuu wa CCM Zanzibar Abdalla Juma Mabodi, alisema, ushindi wa CCM hauna shaka, kutokana na kuitekeleza vyema ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020.

‘’Leo kutoka mjini Wete hadi kijiji cha Gando, unatumia dakika zisizozidi 20, maana barabara imejengwa tena kwa kiwango cha lami, hayo ndio mambo ya CCM,’’alisema.

Wakati huo huo wagombea ubunge, uwakilishi wa Jimbo la Gando pamoja na madiwani, wamewaomba wananchi hao kuwapigia kura ili kuimarisha maendeleo.