Thursday, November 14

Vijana Kisiwani Pemba wametakiwa kuendelea kuilinda, kuitetea na kuidumisha amani na utulivu uliopo nchini

BAKAR MUSSA-PEMBA.

Vijana Kisiwani Pemba wametakiwa kuendelea kuilinda, kuitetea na kuidumisha amani na utulivu uliopo nchini kwani ndio njia pekee
inayowawezesha Viongozi wakuu wa Serikali kuwaletea maendeleo Wananchi bila ya ubaguzi wowote.

Hayo yalielezwa na Ofisa Uchechemuzi na Mawasiliano wa kutoka taasisi ya Norwegian Church Aid (NCA) Nizar Seleimani Utanga huko Kisiwani Pemba kwa nyakati tafauti wakati akizungumza na wananchi wakiwemo Vijana katika bonanza la mradi wa ‘Amani yetu, Kesho yangu’lilofanyika katika mikoa miwili Kisiwani humo.

Alisema kuwa Amani ni jambo muhimu katika nchi yoyote kwani kutokuwepo kwake hakuna jambo ambalo linaweza kufanyika , hivyo aliwasihi Vijana na wananchi kwa ujumla kuendelea kuwaunga mkono ili waweze kuwaletea maendeleo kwa faida yao na vizazi vijavyo.

Alifahamisha taasisi yao ya NCA imekuwa ikishirikiana na wadau mbali mbali wa amani ikiwemo taasisi ya Zanzibar Interface, kuihamasisha jamii wakiwemo Vijana juu umuhimu wa kudumisha amani ndani ya nchi.

“ Tumeamuwa kufanya tokeo hili la kuwakutanisha nyinyi Vijana juu ya umuhimu wa kudumisha amani kwani sasa hivi kuna wenzetu hawako salama kutokana na kuivunja amani yao , huku Vijana , wanawake na watoto wakiwa ndio wahanga wakuu wa matokeo hayo”, alisema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Kaskazini Pemba, Hashir Ali Said aliipongeza taasisi ya NCA kwa kuanzisha jambo hilo kwani amani ndio kitu muhimu katika nchi yoyote na kutoweka kwake ni gharama kubwa kuirejesha.

Alisema kama Vijana wataendelea kuitetea , kuilinda na kuidumisha kwa gharama yoyote ile  kwa vile wanaelewa umuhimu wa kuwepo kwake katika nchi .

Aliwataka Vijana kutokubali kushawishiwa kuvunja amani walionayo na watambuwe kuwa wao ndio wahanga wakuu pale panapokosekana amani kutokana na kuwa rahisi kwao kupokea vishawishi vya aiana tafauti.

Mwenyekiti huyo aliwasihi Vijana kujiunga na vikundi vya Uzalishaji mali ili waweze kujipatia vipato vyao vya halali wakati Serikali zote mbili ikiwemo ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na mama Samia na ile ya Zanzibar inayoongozwa na Dk, Hussein Ali Mwinyi wametowa mikopo mbali mbali kwa wajasiriamali ikiwemo na vijana ili waweze kujinasua na Umaskini.

“ Niiombe taasisi ya NCA , muendelee kutupatia hamasa kama hizi kwani itawaweka pamoja Vijana wa maeneo mbali mbali kubadilishana mawazo na kuendelea kudumisha amani iliopo”, alieleza.

Kwa upande wake Ofisa Elimu Wilaya ya Micheweni Ismail Ali Hamad kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Micheweni Pemba aliishukuru taasisi ya Norwegian Church Aid kwa kuandaa Bonanza hilo lenye ujumbe wa amani kwani ndio inayowawezesha Viongozi wakuu wa nchi kufanya shuhuli zao bila ya wasi wasi wowote.

Alisema ni vyema kila mwananchi kuwaunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk, Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  Dk, Hussein Ali Mwinyi  kwa kusimamia amani na utulivu ndani ya taifa hili.

Aidha aliwataka Wananchi wakiwemo Vijana kuungana pamoja juu ya mapambano ya Udhalilishaji kwani ndani ya Wilaya yao ya Micheweni hali haiko salama, sambamba na utoro wa wanafunzi kwani Wilaya hiyo inaongoza kwa Zanzibar.

“ Niwaombe ndugu zangu Vijana kuweni tayari kuungana pamoja tupinge udhalilishaji kwani mambo haya yamekuwa yakiendelea siku hadi siku licha ya Viongozi wa Serikali na taasisi mbali mbali kukemea suala hilo”, alieleza.

Nae Haji Mussa Khatib kutoka Kamisheni ya Wakfu na mali ya amana Zanzibar alisema amani ni suala muhimu katika maisha ya mwanaadamu hivyo ni wajibu wa kila mmoja kuweka mbele Uzalendo kwa kuwa tayari kuilinda na kuitetea ili isitoweke.

Aliwataka Vijana kuelewa kuwa panapokosekana amani wao ndio Wahanga wakuu hivyo wajiepushe na Viashiria vyote vya uvunjifu wa amani ili nchi iendelee kuwa salama na kimbilio kwa watu wengine.

“ Ukosefu wa amani , huzaa vitendo vingi vya kihalifu ikiwemo wizi, uvutaji wa madawa ya kulevya , Udhalilishaji nk, hivyo  musiwe tayari na arahisi kupokea vishawishi kwa watu wasio itakia mema nchi hii”, alieleza.

Aliwapongeza Viongozi wa Vyama vya Siasa na Serikali kwa uamuzi wao wa kuwaweka pamoja Wananchi wa Zanzibar kuwa kitu kimoja jambo ambalo limejenga upendo, mshikamano na kusaidiana na kuweka mbele tafauti zao walizokuwa nazo.

Mussa  aliomba, taasisi hiyo kuendelea kutowa Elimu kwa jamii yote kwa kufanya Bonanza za aina mbali mbali ili ujumbe uweze kufika kwa haraka zaidi sambamba na kuendelea kufadhili vikundi vya uzalishaji Ujumbe wa Bonanza hilo ni AMANI YETU , KESHO YANGU.

MWISHO.